Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Abiria 1,200 wa treni wakwama saa 18 Morogoro, Dodoma

Baadhi ya abiria wakiwa wamejipumzisha katika stesheni ya reli Morogoro wakitokeaDar es Salaam kwenda mikoa ya Bara kukwama tangu jana saa 2 asubuhi kutokana na njia ya reli kipande cha Morogoro-Kilosa kuharibika na mvua zinazoendelea kunyesha. Picha na Juma Mtanda.

Muktasari:

  • TRC imeandaa mabasi yatakayosafirisha kutoka stesheni ya Dodoma na kuwafikisha Morogoro ili waendelee na safari, huku mabasi mengine yakichukua abiria waliokwama Morogoro kupelekwa stesheni ya Dodoma kuwawezesha kuendelea na safari zao.

Morogoro. Abiria 1,200 waliokuwa wakisafiri kwa treni ya Shirika la Reli Tanzania (TRC) kutoka Dar es Salaam kwenda mikoa ya bara wamekwama katika stesheni ya Morogoro kwa saa 18 baada ya mvua zinazoendelea kunyesha kuharibu njia ya reli kipande cha Morogoro - Kilosa mkoani hapa.

Akizungumza na Mwananchi leo Ijumaa Januari 12, 2024 katika stesheni ya Morogoro, Kaimu Stesheni Masta Morogoro, Herman Ngonyani amesema kipande cha njia ya reli Morogoro hadi Kilosa kimehabiriwa na mvua zilizonyesha juzi usiku na njia ya Mpwawa na Chamwino imeharibiwa na mvua zilizonyesha usiku wa kuamkia leo.

Kutokana na mkwamo huo, Ngonyani amesema wameandaa usafiri mwingine wa mabasi 48 yatakayoanza safari jioni ya leo Januari 12, 2024.

“Abiria 1,200 wamekwama tangu jana saa 2 asubuhi wakitokea Dar es Salaam kwenda mikoa ya bara kwa sababu mvua zinazoendelea kunyesha zimeharibu njia ya reli kutoka Morogoro-Kilosa.

 “Abiria waliokuwa wakitoka mikoa ya bara kwenda Dar es Salaam na wenyewe wamekwama kutokana na kipande cha njia ya reli Mpwapwa-Chamwino na njia ya reli nayo imeharibiwa kipande hicho,” amesema Ngonyani.

Ngonyani amesema mabasi yatawasafirisha abiria kutoka stesheni ya Dodoma na kuwafikisha Morogoro ili waendelee na safari kwa treni iliyokwama Morogoro na abiria waliokwama Morogoro watapanda mabasi hayo na kupelekwa stesheni ya Dodoma na kuendelea na safari zao.

Wakati huohuo, amesema mafundi wanaendelea kupambana kurejesha miundombinu haraka, ili ipitike bila vikwazo.

Baadhi ya abiria wameitaka TRC wajikite kuimarisha miundombinu ya reli hasa maeneo korofi kwa kujenga madaraja au makaravati makubwa yatayowezesha kupitisha maji maeneo hayo bila kuathiri njia ya reli.

“Nimetoka Dar es Salaam naelekea Nzega, Tabora na tangu tumeanza safari treni imekuwa ikisimama muda mrefu katika stesheni za njiani.

“Tulipofika hapa Morogoro ndio tunaambiwa wasafiri kuwa njia ya reli ina shida kipande cha Morogoro-Kilosa na tumekwama tangu jana saa 2 asubuhi,” amesema Rajabu Shabaan.

Kwa upande wake, mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika Shule ya Nyakitundu Kigoma, Vaileth John amesema alitarajia kuwahi shuleni kuanza masomo, lakini amekwama.

“Wanafunzi wenzangu wameanza masomo na mimi nimekosa masomo ya mwanzo . Nilitegemea Jumatatu nikaripoti shule na treni ndio imekwama hapa na sijui kama naweza kuripoti shule wiki ijayo,” amesema Vaileth.

Naye Dafroza Rashid, amesema kukwama kwa treni hiyo Morogoro kumewasababisha kuingia kwenye matumizi yasiyo ya lazima.

“Bajeti yangu ya matumizi ya njiani kutoka Dar es Salaam nilipanga iwe ya siku mbili ama tatu, hii kulingana na ratiba ya treni, lakini kwa kadiri tunavyoendelea kukaa eneo moja kwa muda mrefu ndivyo matumizi ya fedha inavyozidi kutumika,” amesema Dafroza.