Wenye viwanda wang’atwa sikio

Muktasari:

Maonesho ya saba ya bidhaa za viwanda Tanzania yenye kauli mbiu ya ‘Nunua bidhaa ya Tanzania jenga Tanzania’ yameanza Jumamosi ya Desemba 3 hadi 9, 2022 katika Viwanja vya Sabasaba, jijini Dar es Salaam

Dar es Salaam. Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar, Omar Said Shaaban amesema licha ya Taifa kutokupiga hatua katika  kuzipa thamani bidhaa zinazozalishwa nchini, amewataka Watanzania kutumia fursa za majukwaa yaliyopo kutangaza teknolojia ya sekta hiyo kuwavutia walaji.

  

Shaaban amesema hayo leo Jumapili, Desemba 04, 2022 kwenye hafla ya uzinduzi wa Maonesho ya saba ya bidhaa za viwanda Tanzania yenye kauli mbiu ya ‘Nunua bidhaa ya Tanzania jenga Tanzania’ yanayofanyika kwa siku sita kwenye Viwanja vya Sabasaba, jijini Dar es Salaam.


“Tanzania ipo katika nafasi nzuri ya kiushindani ndani na nje ya nchi kutokana na fursa za soko la pamoja ikiwemo ya kikanda, soko huru la Afrika na nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na soko la Ulaya sehemu zote zinahitaji bidhaa hivyo washiriki yatumieni maonesho haya kutangaza teknolojia ya viwanda iliyopo,” amesema 


Aidha, amesema Serikali inatambua changamoto zinazowakumba wenye viwanda nchini na Serikali inaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa maendeleo ya uwekezaji kwa kufanya mageuzi ya kisera, sheria na miundo ya taasisi zake.


“Msisitizo wa Serikali ni kuendelea kuboresha mazingira ya viwanda ikiwa ni pamoja na uimarishwaji wa upatikanaji wa nishati ya umeme wa uhakika na bei na fuu kujenga barabara,reli ,bandari na viwanja vya ndegei ili kuwezesha ukuaji wa sekta,” amesema


Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade), Latifa Khamis amesema licha ya maonesho hayo kufikisha miaka saba tangu kuanzishwa lakini hamasa ya kuongezeka idadi ya washiriki imekuwa ikijitokeza kila mwaka.


“Mfano safari hii tunawashiriki  502 ukilinganisha na mwaka uliopita 2021 tulikuwa na washiriki 121 jambo linaloleta chachu na tija kwa Serikali inayoandaa kuona washiriki wanaongezeka na tunaahidi kuendelea kuwaunga mkono kwa kuwaunganisha na wafanyabiashara wakubwa kutoka nje ya nchi,” amesema Latifa


Hata hivyo, Mwakilishi wa Wamiliki wa Viwanda Tanzania, Amir Hamza amesema mikataba mbalimbali ambayo nchi imesaini ambayo haiwezi kuvunjwa bado kwao ni changamoto ya kushindana na wazalishaji wa bidhaa nje ya nchi.

“Kuna bidhaa kutoka jumuiya mbalimbali zinazoingia kila siku biashara imekuwa soko huria serikali yetu inatakiwa itulinde na kutupatia mazingira ya kuweza kushindana na washindani wetu inatakiwa tuwazidi kidogo kwa sababu bidhaa zetu ni bora na zinapekekwa njena tukiziongezea thamani zitaenda juu sana,” amesema

Maonesho hayo yanaendelea kesho kwa kufanyika mdahalo ambao wamiliki wa viwanda nchini watakuwa wanabainisha changamoto zinazowakumba na kutafuta mbinu ya kuzitatua na kuangali fursa zingine.