Wanne wauawa, Hiace ikichomwa moto tuhuma za wizi wa ng’ombe

Muktasari:
- Jeshi la Polisi lafanya msako kubaini waliohusika kuwaua watuhumiwa.
Dodoma. Watu wanne wameuawa na gari aina ya Totoya Hiace kuchomwa moto na wananchi wa Kijiji cha Chiboli, Kata ya Manzase, wilayani Chamwino mkoani hapa baada ya kudaiwa kuiba ng’ombe wanne.
Pia inadaiwa askari polisi amejeruhiwa kwa kurushiwa mawe na fimbo na wananchi hao alipowazuia kuwadhuru watuhumiwa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Martine Otieno ameiambia Mwananchi Digital kuwa tukio hilo lilitokea Jumamosi, Machi 16, 2024 baada ya watu hao kukamatwa wakiwa na nyama ya ng’ombe hao wanne wanaodaiwa kuwaiba baada ya kuwachinja.
Amesema watu hao wanadaiwa kuiba ng’ombe wanne nyumbani kwa mjane, kuwachinja na kisha kupakia nyama kwenye gari hilo.
Kamanda Otieno amesema baada ya kubainika watu hao walitelekeza gari na kukimbilia porini, ambako wananchi waliwafuatilia na kuwakamata, ndipo walipowaua.
“Tunaendelea kufuatilia ili kufahamu ni kina nani walihusika na mauaji hayo kwa sababu walijichukulia sheria mkononi. Tunasema watu kama hao wakikamatwa, kama ni mwizi ni vizuri kuwafikisha kwenye vyombo vya ulinzi na usalama ili sheria ichukue mkondo wake,” amesema.
Amesema wanaendelea kutoa elimu kwa wananchi ili pale inapotokea matukio kama hayo wahakikishe wanawafikisha katika vyombo vya dola watuhumiwa, ili wachukuliwe hatua za kisheria kuliko kujichukulia hatua za kuondoa uhai wa watu.
Alipoulizwa kuhusu Polisi aliyejeruhiwa katika tukio hilo, Kamanda Otieno amesema vijana wake wako vizuri, hakuna aliyeumia wala kujeruhiwa bali wanaendelea vizuri tu.
“Kazi zetu za purukushani, kwa hiyo kuumia na nini huwa vipo kwenye utekelezaji wa kazi zetu za kila siku, ni vitu ambavyo vinatokea kwa hiyo tunaendelea na uchunguzi ili tuweze kuwabaini watu waliohusika na kadhia hiyo, hatua za kisheria zichukuliwe,” amesema.
Kuhusu sehemu kubwa ya nyama zinazoingia na kuuzwa buchani katika Jiji la Dodoma kuwa zimetokana na wizi wa ng’ombe, Kamanda Otieno amesema taarifa hizo zipo lakini bado hazijathibitishwa ingawa wananchi wanazungumza hivyo.
“Tunaomba wananchi watusaidie tuwang’amue hawa wezi na wanaochinja nyama isivyo halali ili tuweze kuchukua hatua nyingine za kisheria,” amesema.
Hali ilivyokuwa
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino, Edson Sweti amesema taarifa alizopata kutoka kwenye eneo hilo zinaonyesha tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia Jumamosi, Machi 16, 2024.
Sweti amesema watu watatu walienda katika zizi la mjane aliyejulikana kwa jina moja la Veronica katika Kijiji cha Chiboli na kuiba ng’ombe wanne.
Amesema watu hao waliwachinja ng’ombe hao, kuondoa viungo vya ndani na kisha kuondoka na nyama iliyokuwa na ngozi ndani ya gari aina ya Toyota Hiace.
Amefafanua baadhi ya watu waliwaona wakiiba ng’ombe hao, hivyo waliwafuatilia kwa kuwataarifu wenzao walioziba njia kwa kuweka magogo barabarani.
Hata hivyo, watuhumiwa hao waliweza kuyapita nawe na magogo hayo.
Kutokana na hilo, wananchi hao waliweka matoroli yanayokokotwa na ng’ombe barabarani, hivyo watuhumiwa walipoona hawawezi kuendelea na safari, walitelekeza gari na kukimbilia porini.
Amesema wananchi waliwafuatilia na kuwakamata, wakawapeleka kwenye ofisi ya mtendaji.
Sweti amesema baada ya kuwakamata, alifika mfanyabiashara ambaye wananchi wanadai ndiye mnunuzi wa nyama zinazoibiwa akiwa na askari Polisi ndipo zikajitokeza vurugu ambazo zilisababisha watu hao kuuawa na wananchi.
“Ninavyoelezwa na viongozi wa huku ni kuwa askari aliyekwenda na mtu huyo alipiga risasi juu akijaribu kuwatawanya wananchi, lakini hakufanikiwa kutokana na wingi wa watu waliokuwepo katika tukio hilo,” amesema.
Amesema malalamiko ya wizi wa ng’ombe katika eneo hilo ni ya siku nyingi na wameshawasiliana na Mkuu wa Wilaya ya Chamwino kuelezea changamoto hiyo ambayo bado haijapatiwa ufumbuzi.
Mmoja wa wakazi wa eneo hilo, ambaye hakutaka jina lake liandikwe, amesema tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia Jumamosi saa tisa katika nyumba ya Veronica.
Amesema kwa sababu ni wizi uliokithiri kwa muda mrefu, wananchi wa vijiji jirani vinane vya wilaya za Mpwapwa na Chamwino, walijitokeza kuwasaka watuhumiwa kuanzia saa 11.00 alfajiri hadi saa nane mchana walipowakamata.
Amesema kutokana na idadi ya watu waliokuwepo katika tukio hilo, haikuwa rahisi kwa askari mmoja mwenye bunduki kuwazuia wasifanye jambo lolote mahali hapo.
“Vurugu ilipokuwa kubwa sisi tuliamua kuondoka kujinusuru kwa sababu watu walikuwa wakirusha mawe na fimbo,” amesema.