‘Wanaopata huduma za dharura Muhimbili afya zao huimarika’

Mkuu wa Idara ya Tiba ya Magonjwa ya Dharura Hospitali ya Muhimbili, Dk Juma Mfinanga( kulia) akizungumza na mgonjwa Nyanya Pischedda. Picha na Hadija Jumanne
Muktasari:
- Mkurugenzi wa Huduma za Tiba Hospitali ya Taifa, Dk John Rwegasha amesema hayo katika maadhimisho ya miaka 10 ya ushirikianao baina ya hospitali hiyo na Mfuko wa Abbott Tanzania
Dar es Salaam. Imeelezwa kuwa asilimia 99.5 ya wagonjwa wote wanaopokewa katika Idara ya Tiba ya Magonjwa ya Dharura (EMD), Hospitali ya Taifa Muhimbili(MNH) wana uhakika wa kupatiwa huduma za matibabu kwa wakati na afya kuimarika.
Mkurugenzi wa Huduma za Tiba Hospitali ya Taifa, Dk John Rwegasha amesema hayo mwanzoni mwa wiki katika maadhimisho ya miaka 10 ya ushirikianao baina ya hospitali hiyo na Mfuko wa Abbott Tanzania.
Lengo ni kusaidia kuboresha huduma za tiba ya magonjwa ya dharura hospitalini hapo.
Dk Rwegasha amesema uhusiano huo umesaidia kuboresha huduma hizo na kupunguza vifo hadi kufikia chini ya asilimia 0.5.
“Zamani ulikuwa ukisikia watu wakilalamika kuwa wagonjwa wa dharura wakifika hapa wanapoteza maisha ila kwa sasa malalamiko hayo hakuna tena, kwa kuwa huduma zimeboreshwa,”amesema Dk Rwegasha.
Mkuu wa Idara ya Tiba ya Mgonjwa ya Dharura Muhimbili, Dk Juma Mfinanga amewashauri ndugu wanaopeleka wagonjwa katika idara yake wawe na subra na utulivu kwa sababu madaktari na wataalamu wanakuwa wamejikita kumhudumia mgonjwa huyo.
“Moja ya changamoto tunayokutana nayo ni baadhi ya ndugu wa wagonjwa kutokuwa na subra, unakuta ndugu wapo 20 kila mmoja anataka kuwa ndugu wa karibu wa mgonjwa huyo, kila mmoja anataka kufuatilia taarifa ya mgonjwa mmoja, sasa unashindwa kumhudumia mgonjwa kwa sababu ndugu wana wanakuvuruga, hivyo ni vizuri ukileta mgonjwa wako tuachie sisi tumhudumie halafu tutakupa ripoti na uzuri katika idara yetu kuna sehemu ya maalumu tumetenga kwa ajili ya ndugu kukaa na kusubiria ripoti ya mgonjwa, ” amesema Dk Mfinanga.
Amesema idara hiyo inatoa huduma muhimu ikiwamo ya upasuaji, hivyo mgonjwa atakayepokewa katika idara hiyo anapatiwa huduma zote za awali kabla ya kupelekwa wodini.
“Tunataka jamii ituamini, sisi tupo hapa kwa ajili ya kuwasaidia na tumejipanga kutoa huduma hii ili kuhakikisha tuna mhudumia kila mmoja anayefikishwa katika idara yetu,” amesema Dk Mfinanga.
Pia, amesema hiyo ndiyo idara ya mfano kwa hospitali zote nchini na imekuea ikitumika kama mfano wa tiba za dharura kwa nchi nyingine barani Afrika.
Ametaja wagonjwa wanaongoza kufikishwa katika idara yake kuwa ni wagonjwa wanaotokana na ajali mbalimbali, wagonjwa wenye shida ya upumaji na magonjwa mengine.
Ujenzi Idara ya EMD
Mkurugenzi Mtendaji Mfuko wa Abbott Tanzania, Profesa Hendry Sawe, amesema mfuko huo kwa kushirikiana na Serikali wanatambua kuna watu wengi wanaoishi vijijini wanahitaji huduma za magonjwa ya dharura na watendelea kushirikiana katika kuwafikia.

Mkurugenzi Mtendaji wa mfuko wa Abbot Tanzania, Profesa Hendry Sawe akizungumza na waandishi wa habari wakati wa maadhimisho ya miaka 10 ya ushirikiano baina ya Hospitali ya Taifa na mfuko huo. Picha na Hadija Jumanne
Profesa Sawe amesema miaka 14 iliyopita, Tanzania haikuwa na hospitali hata moja yenye kitengo maalumu cha kutoa huduma za tiba ya dharura na ajali, vifo katika Hospitali ya Taifa vilikuwa takribani asilimia 14.
Amesema wakati mwingine, wagonjwa waliohitaji huduma muhimu za kuokoa maisha, walilazimika kusubiri saa kadhaa kabla ya kuonwa na madaktari bingwa ambao hawakuwa na utaalamu wa kutosha katika kutoa tiba za dharura.
“Kupitia ushirikiano na Serikali ambao umedumu kwa zaidi ya muongo mmoja, mwaka 2010 mfuko wa Abbott, ulisaidia kuanzisha idara ya tiba za Dharura katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa kutoa Sh37 bilioni pamoja na kuanzishwa kwa mafunzo ya madaktari bingwa wa tiba ya dharura katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili - zote zikiwa za kwanza Afrika Mashariki,” amesema Profesa Sawe.
Pia, amesema fedha hizo zilihusisha katika ujenzi wa idara hiyo, uwekaji vifaa tiba, kianzishwa na uendeshaji wa mafunzo ya fani ya udaktari bingwa wa tiba ya dharura, udhamini wa kufundisha watoa huduma mbalimbali wanaokuja Muhimbili na programu ya kujengea uwezo Hospitali nyingine zilizoanzisha idara ya tiba ya dharura.
Profesa Sawe amesema jitihada hizo zilipata matokeo ya haraka, vifo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili vilipungua kwa takribani asilimia 40 katika kipindi cha miaka miwili ya kwanza.
Mkurugenzi wa Huduma za Tiba ya Dharura Wizara ya Afya, Dk Erasto Sylvanus amesema wizara hiyo imekuwa na jukumu la kuhakikisha wananchi wote wanapatiwa huduma bora zaidi.
Cuthbet Mariki ni baba mzazi wa mtoto Dorcus (8) ambaye alilazwa katika idara hiyo baada ya kupata ajali ya pikipiki miaka miwili iliyopita na kuvunjika mguu na kupinda kiuno, ameshukuru idara hiyo kwa kusaidia mwanaye kupona, japokuwa bado hajaanza kutembea.
"Kwa sasa mwanangu anaendelea vizuri na anakuja hospitali hapa mara 14 kwa mwezi kwa ajili ya kufanyiwa mazoezi ya viungo na matibabu mengi, niseme tu wakati namleta hapa hospitali mwanangu alikuwa amepoteza fahamu na ulimi ulikuwa umetoka kwa nje na damu zilikuwa zinatoka, nilichanganyikiwa nilijua Dorcus ameshafariki, lakini huduma alizopewa hapa pamoja na kulazwa ICU kwa siku 25 zilinipa matumaini na kunitia moyo" amesema Mariki.
Amesema katika ajali hiyo, iliyotokea Mei 15, 2022 ilisababisha mwanaye huyo anayesoma Shule ya Golden Light iliyopo Mbezi Msakuzi, kupata kiharusi cha kichwa japokuwa kwa sasa ameimarika.
kwa upande wake, Nyanya Pischedda(55) ambaye alilazwa katika idara hiyo baada ya kupata shida ya upumuaji katika mfumo wa fahamu, anaishukuru idara hiyo kwa kupatia matibabu ya kibingwa hadi kupona na kurudi katika hali yake ya kawaida.