Waliosomea diplomasia wakae mkao wa kula, ajira zanukia wizarani

Waziri wa Mambo ya Nnje ya Nchi na Ushirikiano wa Afria ya Mashariki, January Makamba (katikati) akiteta jambo na Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo (Kulia kwake) na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Jenista Mhagama leo Jumanne, Mei 28, 2024  bungeni jijini Dodoma.

Muktasari:

Wanatakiwa vijana watakaokubali kutumikia wizara kwa  miaka mitatu kwa malipo mazuri baada ya kutahiniwa kwa viwango vya juu sana vya kimataifa.

Dodoma. Wizira ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imesema mwaka ujao wa fedha itaanza kutoa ajira za miaka mitatu kwa waombaji wenye umri wa miaka 40, wakiwamo kutoka sekta binafsi.

Waziri wa wizara hiyo, January Makamba amesema hayo alipowasilisha maombi ya fedha kwa mwaka wa fedha 2024/25 ya Sh242 bilioni ambayo Bunge limepitisha.

Akizungumzia ajira, amesema wataanzisha mpango wa kutafuta vijana wenye vipaji vya juu kwenye masuala ya diplomasia.

“Vijana watakaokubali kutumikia miaka mitatu kwa malipo mazuri na baada ya kutahiniwa kwa viwango vya juu sana vya kimataifa waje kutumika wizarani, lakini na kwenye balozi na kama watafuzu kwenye kipindi cha miaka mitatu watapewa fursa ya kuajiriwa.

“Wanatarajiwa wanaotoka shuleni, hata walio kwenye sekta binafsi, mfano mtu anafanya kazi benki Mtanzania ana miaka 40 ameona abadilishe upepo waingie serikalini kwenye diplomasia anaruhusiwa kwa utaratibu huu maalumu ambao utakuwa ni mtihani mahususi wa kupima kila kitu maarifa yote ya lugha, kuandia na kujieleza,” amesema.

“Imani yetu ni kwamba tukifanya programu hii kwa miaka mitano, sita tutakuwa tumeshaheneza wizara kuwa na wanadiplomasia mahiri wakiwamo watu walitoka kwenye sekta binafsi ambao wanaweza kufanya kazi ya diplomasia,” amesema.

Majengo ya kitegauchumi

January amesema Serikali inakusudia kujenga majengo ya kitegauchumi katika mataifa matatu barani Afrika ili kupunguza mzigo wa gharama kwa balozi nje ya nchi.

Majengo hayo yatajengwa katika majiji ya Kinshasa (Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo-DRC) lenye ghorofa 25, Nairobi (Kenya) lenye ghorofa 22 na lingine litajengwa nchini Uganda.

Amesema Serikali inatumia Sh29.6 bilioni kulipa pango, kwenye balozi zikuhusisha ofisi za ubalozi na makazi ya watumishi.

Amesema Tanzania ina viwanja na nyumba 109 duniani na kwamba, uwekezaji utakaofanyika kwa mwaka utaingiza Sh692 bilioni, ambazo mapato kwa mwezi yatakuwa Sh36 bilioni.

Akieleza hayo, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama katika maoni yaliyosomwa na mjumbe wa kamati hiyo, Joseph Tadayo imesema miradi yote ya maendeleo itagharimu Sh343.1 bilioni.

“Taarifa iliyowasilishwa na wizara ilionyesha imepanga kutekeleza miradi ya maendeleo yenye thamani ya Sh343.1 bilioni kutoka vyanzo mbadala ikiwamo ubia na taasisi za umma na binafsi za nchini.”

“Miradi hiyo inakusudiwa kutekelezwa katika balozi za Nairobi (Kenya), Kinshasa (DRC) na Lusaka (Zambia). Ni matarajio ya kamati kuwa miradi ya ubia itazingatia masilahi, faida na manufaa kwa Taifa,” amesema.

“Wizara inaendelea na maandalizi ya utekelezaji wa miradi ya majengo ya wizara pamoja na vitega uchumi katika viwanja vya Serikali vilivyopo katika balozi za Tanzania Kampala (Uganda), Abuja (Nigeria) na Lusaka (Zambia)” amesema January.

“Katika utekelezaji wa miradi hiyo, wizara inakamilisha taratibu za kupata washauri elekezi, kufanya upembuzi yakinifu, kupima udongo, kufanya marejeo ya michoro ya majengo husika, kupata vibali vya ujenzi kutoka mamlaka za miji hiyo na kuanza ujenzi,” amesema.

Amesema katika mpango madhubuti wa kuendeleza viwanja na milki zake zilizoponje ya nchi, Serikali imeunda timu ya wataalamu, ikiwa na jukumu la kuishauri Serikali namna bora ya kuendeleza na kusimamia milki hizo nje ya nchi.

“Maandalizi yanaendelea ya kumpata mshauri elekezi mwenye uzoefu wa kimataifa katika masuala ya milki atakayeandaa nyaraka mbalimbali za uwekezaji, miongozo na kuishauri Serikali namna bora ya uendelezaji wa milki hizo kulingana na maeneo ya balozi husika,” amesema.

“Kwa sasa timu hiyo imeendelea na ukamilishaji wa nyaraka za ununuzi ili kumpata mshauri elekezi huyo,” amesema.

Amesema picha za majengo ya Nairobi na Kinshasa zipo tayari huku akieleza za majengo mengine ya kitegauchumi katika majiji ya Maputo (Msumbiji), Bujumbura (Burundi), Kigali (Rwanda) na Lilongwe (Malawi) nazo zimewekwa wazi.

Kwa mujibu wa January, Serikali ina nyumba na viwanja 109 duniani kote na kodi ya pango wanayolipa ni Sh29.6 bilioni kwa mwezi.

“Wizara imeingia makubaliano ya ubia na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kwa ajili ya ujenzi wa jengo la kitegauchumi katika ubalozi wa Tanzania Nairobi.

Amesema mradi huo unahusu kuendeleza kiwanja kilichopo eneo la Upperhill jijini Nairobi kwa kujenga majengo pacha ya ghorofa 22.

Makamba amesema wizara imekamilisha taratibu za kisheria za makabidhiano ya nyaraka na kuhamisha rasmi majukumu ya ujenzi wa mradi kwenda NSSF.

“Wizara pia kwa kushirikiana na NSSF imekamilisha maandalizi ya nyaraka za kisheria kwa mradi wa ujenzi wa jengo la kitegauchumi Kinshasa.”

“Utekelezaji wa mradi huo unafanyika katika kiwanja cha ubalozi kilichopo Mtaa wa Boulevard de 30 Juin jijini Kinshasa, utahusisha ujenzi wa jengo la ghorofa 25,” amesema.

Amesema pia wizara inaendelea na maandalizi ya utekelezaji wa miradi ya majengo ya wizara na vitegauchumi katika viwanja vya Serikali vilivyopo.

Maoni ya Kamati

Tadayo akiwasilisha maoni ya kamati kuhusu utekelezaji wa miradi ya vitegauchumi, amesema wizara iongeze mawanda na kushirikisha kampuni binafsi na za umma katika nchi ambazo miradi hiyo inatekelezwa.

“Serikali iweke mkakati wa makusudi wa kuutangaza mpango wa ujenzi wa majengo ya kitegauchumi na ofisi za ubalozi katika nchi ambazo miradi hiyo inatekelezwa,” amesema.

“Kufanya hivyo kutasaidia kuvutia wabia kutoka sekta binafsi na umma katika nchi hizo, hivyo kurahisisha utekelezaji wa mpango huo na kupata wawekezaji wenye uwezo na sifa,” amesema.

Tadayo amesema kamati imeshauri mikataba ya ujenzi wa miradi ya kitega uchumi na ofisi za ubalozi katika nchi mbalimbali baina ya sekta binafsi na umma, na mikataba ya uendeshaji wa miradi hiyo, iandaliwe kwa umahiri na kuzingatia masilahi mapana ya nchi.

Upimaji utendaji wa mabalozi

Akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2024/25, January amesema wana mpango wa kuanza kupima utendaji kazi wa mabalozi nje.

“Serikali iandae mpango wa kuweka vigezo vya utendaji kwa kila balozi kwa kuzingatia nchi ambayo ubalozi upo. Vitumike katika kupima utendaji kazi wa balozi,” amesema Tadayo.

“Kufanya hivyo kutasaidia mabalozi kufanya kazi kwa malengo na kuzingatia vipaumbele vilivyoanishwa, hivyo nchi yetu kunafaika zaidi katika eneo la diplomasia ya uchumi na sekta nyingine kwa ujumla,” amesema.

Kamati imeshauri upimaji huo uende sambamba na kuboresha mazingira ya kazi katika balozi.

Mbunge wa viti maalumu, Catherine Magige ametaka suala hadhi maalumu kwa diaspora liongezwe kasi ya kuwasilisha muswada wa mabadiliko bungeni.

Pia, ameshauri mabadiliko ya sheria akitaka Diaspora waruhusiwe kumiliki ardhi kwa utaratibu utakaotolewa ili wapate haki na upendeleo walioupoteza kwa muda mrefu.