'Wahuni' wafyeka ekari 25 za mahindi

Bwana shamba wa shamba la Efatha lililopo Sumbawanga, Simon Jacob, akionyesha mahindi yaliyofyekwa na watu wasiojulikana na kusababisha hasara ya mamilioni ya fedha. Picha na Mpigapicha Wetu
Muktasari:
Watu wasiojulikana, wamevamia na kufyeka ekari 25 za mahindi katika shamba linalomilikiwa na Kanisa la Efatha la Sumbawanga.
Watu wasiojulikana, wamevamia na kufyeka ekari 25 za mahindi katika shamba linalomilikiwa na Kanisa la Efatha la Sumbawanga.
Tukio hilo lilitokea wiki iliyopita na eneo lililofyekwa ni sehemu ya ekari 96 za shamba hilo.
Akizungumzia tukio hilo, Meneja wa shamba hilo, Peter Kibona, alisema liligunduliwa na vijana wake walipokuwa wanakwenda shambani kwao.
“Walipofika katika eneo hilo, vijana walishangaa kukuta mahindi yakiwa yamefyekwa katika eneo kubwa, kwa kweli inasikitisha sana,” alisema Kibona.
Meneja huyo alisema waliofanya kitendo hicho, wameteketeza kiasi kikubwa na chakula ambacho kingesaidia jamii katika siku zijazo.
“Ekari moja inazalisha gunia 20 na kwa hesabu hizo, ekari 25 tungepata magunia 500 ya mahindi,” alisema Kibona.
Alisema tayari uongozi wa shamba hilo umetoa taarifa za tukio hilo.
Meneja huyo wa shamba, alisema kumekuwa na mfululizo wa matukio katika shamba hilo linalomiliki kihalali na kanisa.
“Wananchi waliwahi kuchoma matrekta mapya mawili yanayomilikiwa na Efatha jambo ambalo ni hasara kwao,” alisema.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Rukwa, Jacob Mwaruanda, alisema polisi wana taarifa za tukio hilo na kwamba tayari wameanza kufanya upelelezi ili kujua wahusika na lengo lao.