‘Vijana changamkieni fursa kilimo biashara'

Muktasari:
Pamoja na kuchangamkia sekta hiyo, ili wafanikiwe wametakiwa kuwa na nidhamu ya matumizi ya fedha.
Mwanza. Vijana wametakiwa kuchangamkia sekta ya kilimo biashara ambayo kwa sasa inadaiwa kukua kwa kasi ili wapate ajira, kukuza biashara, uchumi, kuliwezesha taifa, kuwa na akiba ya chakula na kuweza kukopesheka.
Pamoja na kuchangamkia sekta hiyo, ili wafanikiwe wametakiwa kuwa na nidhamu ya matumizi ya fedha.
Wito huo umetolewa leo Ijumaa Novemba 24, 2023 na Ofisa Maendeleo ya Biashara Mwandamizi Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Angelina Nyansambo wakati akiwajengea uwezo vijana 50 waliopo kwenye sekta ya kilimo jijini Mwanza.
Amewambia vijana hao waliowezeshwa na Taasisi ya VSO kupitia mradi wake wa EYEE, kuhusu elimu ya fedha na mitaji ya kukuza biashara na kipato chao kuwa, wengi wao hawana maarifa kuhusu benki hiyo, jinsi ya kuifikia na namna inavyoweza kuwasaidia kuboresha shughuli zao za kilimo biashara.
“Ndiyo maana tumeamua kuwapa elimu ya fursa zilizopo na namna mtakavyonufaika ikiwemo mikopo na uwekezaji kwenye kilimo biashara,”amesema
Angelina amesema katika kipindi cha mwaka mmoja wamewafikia vijana zaidi ya 2,000 katika mikoa ya Kanda ya Ziwa walio kwenye sekta ya uvuvi, kilimo, ufugaji na uchakataji wa mazao, huku lengo likiwa ni kuwafikia 28,000 ndani ya miaka mitano ili kuwajengea uwezo, kuwaonyesha fursa na elimu ya matumizi ya fedha.
“Tunawahimiza vijana wawe na mwamko wa kufanya shughuli za kilimo biashara kuna fursa nyingi kwenye taasisi za kifedha za kuwasaidia kujiendeleza. Tumeona vijana hawana elimu ya kilimo biashara na fedha baada ya mafunzo tutawasaidia kulingana na uhitaji wao kupitia vikundi vyao benki iko tayari kushirikiana nao,” amesema Angelina
Rafidh Rutungo, mfugaji wa kuku jijini Mwanza amesema ndoto yake ni kuanzisha biashara ya uchakataji mazao lakini kutokana na changamoto ya fedha na vifaa ameshindwa kuanza.
Amesema mafunzo hayo yamemfungulia njia na kumuongezea ufahamu wa matumizi sahihi ya mikopo kwa kuandaa mpango mzuri wa biashara kabla ya kuamua kukopa.
“Tumekuwa tukishindwa kuaminika kwenye mikopo kutokana na kuendekeza ujana na starehe badala ya kufanya kazi kwa malengo na mikakati mizuri ya kuinuka kiuchumi na kuwekeza kiuendelevu. Mafunzo haya yamenisaidia namna ya kutumia vyema mikopo kwa kuandaa mpango mzuri wa biashara,”amesema
Akizungumzia umuhimu wa elimu ya fedha na mikopo kwa vijana, Ofisa Biashara na Mikopo TADB Kanda ya Ziwa, Janeth Urio amesema elimu hiyo itawasaidia kufahamu mwingiliano wa biashara za kilimo, shughuli wanazozifanya na mikopo katika sekta za fedha ili iwarahisishie kufahamu aina ya mikopo na namna wanavyoweza kuipata.
“Tumewapa elimu namna wanavyoweza kutunza fedha, kutunza taarifa za fedha, kuweka bajeti ya wanachokifanya na wanachokipata. Tunatamani vijana wengi wapate elimu ya fedha ili kujihusisha na taasisi za fedha, waweze kukopesheka na kukifanya kilimo kuwa ajira kwa sababu sekta ya kilimo inakua kwa kasi na ina fursa nyingi kwa vijana,” amesema Janeth
Mfugaji wa Sungura kutoka kikundi cha Maendeleo Kangaye, jijini hapa kinachojihusisha na ufugaji wa Kuku, Sungura, mapishi na mapambo, Laila Peter amesema vijana wengi wamekuwa wakiamua kufanya biashara na shughuli za kiuchumi kwa kukopa bila ufahamu wa mambo mengi muhimu.
“Bado ufugaji wetu ni duni hivyo semina hizi zitatusaidia kupanua wigo na fursa mpya za biashara,” amesema Laila