'Ukosefu wa taarifa chanzo vijana kutochangamkia fursa za mikopo'

Baadhi ya vijana walioshiriki kongamano la uwezeshaji kiuchumi mkoani Mwanza.
Muktasari:
- Inakadiriwa kati ya zaidi ya Sh40 bilioni zinazotolewa kwaajili ya vijana kukopa kwenye halmashauri zote nchini kwa mwaka, wakati mwingine hawachukui hata nusu ya fedha hizo wakati wana uhitaji wa mitaji.
Mwanza. Vijana nchini wametajwa kutochangamkia fursa za mikopo inayotolewa na Serikali licha ya wengi wao kuhitaji mitaji ya kufanya ujasiriamali, ukosefu wa taarifa sahihi ukitajwa kuwa chanzo.
Akizungumza Machi 29, 2025 kwenye kongamano la uwezeshaji kiuchumi kwa wanawake na vijana lililoandaliwa na kampuni ya Victory Auditors and Business Consoltant, Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la uwezeshaji wananchi kiuchumi (NEEC), Beng'i Issa amesema licha ya Serikali kutoa zaidi ya Sh40 bilioni kwa mwaka kwaajili ya vijana, lakini fedha wanazokopa hazifiki hata Sh20 bilioni.
"Mpango wa halmashauri wa asilimia 10, ukiangalia pesa zinazotolewa kwa mwaka na halmashauri zote Tanzania zinafika zaidi ya Sh80 bilioni mpaka Sh100 bilioni...sasa ukichukua asilimia nne ya zile fedha vijana wanatakiwa wachukie karibu Sh40 bilioni lakini hawachukui, hamfiki mara nyingi hata Sh20 bilioni,"amesema
Nakuongeza kuwa,"Fedha hizi zinachukuliawa sana na wanawake na zinachukuliwa na wanawake kwa sababu wanachukua na wanarudisha kwahiyo ukiishajenga jina zuri kwa mtu anayekukopesha atapenda kukukopesha kila mwaka kwa sababu anataka pesa yake irudi,"

Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), Beng’i Issa akizungumza na vijana kwenye kongamano la uwezeshaji kiuchumi kwa vijana na wanawake Kanda ya Ziwa lililofanyika jijini Mwanza.
Amesema serikalini kuna programu nyingi za kusaidia vijana kupata mitaji ikiwemo mifuko zaidi ya 20 inayotoa mikopo, kati yake mifuko 14 inatoa mikopo kupitia mabenki kwa dhamana ya Serikali, huku akiwatahadharisha wanaochukua mikopo na kukimbia kulipa.
Amesema Serikali inafanya kazi kidijtali, akiwakumbusha wakimbia madeni kuanzia usajili wa biashara, kuomba namba ya mlipa kodi, mkopo na hata kufungua akaunti benki kitambulisho cha Taifa kinatumika hivyo ni rahisi wanaokopa na kukimbia kukamatwa kwakuwa kila kitu kimeunganishwa.
"Tupo connected (tumeonganishwa) ukichukua mkopo kwenye simu unajulikana wewe umechukua mkopo kwenye simu..ukienda kuchukua mkopo benki na unamkopo kwenye simu wanajua unamkopo... wewe katika maisha yako ya ujanja ujanja mtu akitaka kukulipa kwenye biashara yako akakwambia nakulipa kwa lipa namba au nakutumia pesa unamwambia usitumie hii namba tumia ingine unaogopa ule mkopo wako utakatwa lakini ipo siku utashikwa,"amesema
Amewambia vijana wanaotaka kufanya ujasiriamali, wakiweka uaminifu mbele kwenye biashara watafanikiwa na siyo lazima wakope hasa kama hawajui wanataka kufanyia nini mikopo hiyo.

Baadhi ya vijana walioshiriki kongamano la uwezeshaji kiuchumi mkoani Mwanza.
Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Victory Business Consoltant, Albert Gilenga amesema kongamano hilo ni kurudisha kwa jamii ambapo zaidi ya vijana 1,000 kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa wamekutanishwa kujadili, kutatua changamoto zao pamoja na kuoneshwa fursa zinazopatikana Serikalini na sekta binafsi.
"Kwa mujibu wa Sensa asilimia kubwa ni vijana na wanawake lakini pia ndiyo wanahusika sana na mambo ya biashara..ndiyo kundi ambalo lipo katika uzalishaji. Tukaona tukiwawezesha vijana na wanawake kwa kutatua changamoto zao na kuwaonesha fursa zinazotolewa na Serikali na sekta binafsi tukaona kwamba hiyo tunaweza tukawa tumerudisha kwa jamii kwa kiwango kikubwa zaidi,"amesema
Amesema kupitia kongamano hilo wanaenda kufungua kituo atamizi cha kulea, kuwakuza na kuwasaidia vijana kibiashara.
Mkurugenzi wa Mipango wa kampuni hiyo, Dk Boniphace Nyabweta amesema wameratibu kongamano hilo kwakuwa kuna changamoto kubwa ya vijana hasa wa Kanda ya Ziwa kutochukua fursa mbalimbali zinazotolewa na Serikali pamoja na sekta binafsi.
“Kwa mfano Serikali ina fursa za mitaji kama mikopo ya asilimia 10 lakini bado vijana wengi hawachangamkii lakini baraza lenyewe (NEEC) lina fursa za mitaji lakini taarifa zimekuwa hazifiki hivyo tumeona tuilete Serikali kupitia Katibu Mtendaji ili vijana wa Kanda ya Ziwa waweze kupata taarifa sahihi za fursa za kiuchumi,”amesema Dk Nyabweta
Mkazi wa Sengerema mkoani Mwanza, Janeth Emmanuel amesema amefahamu mambo mengi kupitia kongamano hilo ikiwemo fursa ya asilimia 30 zinazotengwa na taasisi za Serikali kwenye bajeti zao za manunuzi ya umma kwaajili ya vijana, wanawake na wenye ulemavu kupitia mfumo wa NeST.