Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

‘Tozo mpya za hoteli kuathiri utalii Zanzibar’

Unguja. Wafanyabiashara wa hoteli na wadau wa utalii visiwani Zanzibar, wamesema kuanzishwa kwa tozo ya dola 5 (Sh11,750) kwa kila chumba cha hoteli kinachotumika usiku mmoja katika bajeti iliyosomwa Juni 15, mwaka huu, itathiri sekta hiyo.

Katika mahojiano na gazeti dada la The Citizen mwishoni mwa juma, Waziri wa Fedha wa Zanzibar, Saada Mkuya Salum alisema tozo hizo mpya zitaanza kutekelezwa mara moja kuanzia Julai Mosi.

“Wafanyabiashara wa hoteli itabidi waone jinsi ya kutekeleza hili na sidhani kama litaathiri biashara zao kwa kiasi hicho, tunachofanya ni kuweka mazingira mazuri ya kibiashara, kwa mfano, kuhusu suala la umeme tumeondoa VAT kwenye paneli za sola," Mkuya alisema.

Aliongeza; “Tozo ya $1 (Sh2300) imekuwapo kwa miaka minane, na ilikuwa ada ya kawaida kwa kila mtu, lakini sasa tumeainisha kulingana na nyota.” alisema.
Utekelezaji huo uliopangwa sasa unaacha wadau wa hoteli mikononi mwa Baraza la Wawakilishi linaoanza kujadili bajeti hiyo leo.

Wakizungumza na Mwananchi kwa vipindi tofauti, wafanyabiashara hao walisema hatua hiyo inaifanya Zanzibar kuwa sehemu ya gharama kubwa na isiyotabirika kufanyia biashara.

"Hoteli tayari zinatoza asilimia 15 kama kodi ya ongezeko la thamani (VAT) sasa ukiongeza hili la dola 5; hii inaenda kwa wateja ambao wanaweza kulazimika kutafuta mahali pengine," alisema mfanyabiashara mmoja wa hoteli huko Stone Town ambaye hakutaka jina lake litajwe.

Rahim Bhaloo, ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wawekezaji wa Utalii Zanzibar (ZATI), alisema jambo hilo limewashangaza wadau wa sekta hiyo. Hivyo, alisema kuna haja ya kushughulikiwa mapema kutokana na mienendo na aina ya biashara.

Kwa upande mwingine Chama cha Waendeshaji biashara yawatalii Tanzania (Tato), William Chambulo, alisema pamoja na kwamba mabadiliko mapya yatakayoanza kutumika Julai Mosi yapo Zanzibar lakini kuna uwezekano mkubwa yakaathiri Tanzania Bara kwa sababu asilimia 40 ya wageni wanaokwenda Zanzibar pia hutembelea Bara kuangalia vivutio mbalimbali.

Katika hotuba yake ya bajeti ya Alhamisi, Juni 15,2023 ndani ya Baraza la Wawakilishi, Waziri wa Fedha wa Zanzibar, Saada Mkuya Salum alisema mabadiliko hayo hayaepukiki kwa sababu kiwango cha dola moja (Sh2,350) iliyopo haiendani na mazingira ya leo.