Ndugu, majirani aliyempondaponda nyeti mtoto wa mkewe wafurahia hukumu

 Mohamed Salange (37) (mwenye pingu) akipelekwa jela baada ya kuhukumiwa kifungo cha miaka 30 jela na Hakimu Mkazi,  Lameck Mwamkoa. Picha na Johnson James

Muktasari:

  • Mohamed Salange alihukumiwa jana kwenda jela miaka 30 baada ya kukutwa na hatia ya kumfanyia ukatili mtoto wake wa kufikia mwenye umri wa miaka tisa.

Morogoro. Siku moja baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro kumhukumu kifungo cha miaka 30 jela Mohamed Salange (37) kwa kosa la kumfanyia ukatili mtoto wake wa kufikia mwenye umri wa miaka tisa, baadhi ya wananchi na ndugu wa mkewe wamepongeza hatua hiyo.

Hukumu ya Salange ambayo ilisomwa jana  Alhamisi Mei 2, 2024 na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Lameck Mwamkoa, ilieleza kuwa  mahakama imejiridhisha pasipo na shaka kwamba mshtakiwa ana hatia kwa kosa aliloshtakiwa nalo.

Katika kesi hiyo, Salange alishtakiwa kwa makosa sita ya ukatili dhidi ya mtoto wake huyo wa kufikia kinyume cha kifungu cha 167 (1) na (2) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu (PC) na kumsababishia madhara makubwa kimwili.

Akizungumza leo Ijumaa Mei 3, 2024, mwenye nyumba aliyokuwa amepanga Salange, Tanasha Milomo amesema amefurahishwa na hukumu hiyo kwa kuwa inatoa funzo kwa wazazi wanaowafanyia ukatili watoto.

“Binafsi nimefurahi sana kuona Mohamed (Salange) amehukumiwa miaka 30 kwenye shtaka moja, maana roho iliniuma baada ya kugundua alikuwa anawafanyia ukatili wale watoto wa mke wake,” amesema Milomo.

Amesema alimpangisha nyumba Salange na familia yake baada ya jirani yake kumweleza kuna mpangaji anahitaji nyumba nzima ya kupanga.

“Sikujua kwamba nampangisha baba mkatili kama huyu, mimi nilikuwa naishi kijijini, sikuwa naona kinachoendelea, lakini baada ya tukio la mauaji ya mkewe na kumzika ndani kufichuka, ndipo nikapata picha sasa, hivyo ninaipongeza Mahakama kwa uamuzi ule, ninatamani adhabu ingekuwa zaidi ya hii,” amesema Milomo.

Mama huyo amesema anajipanga kuifanyia ukarabati nyumba yake ili aendelee kuipangisha.

Kwa upande wake Sarah Onesmo mkazi wa Kimamba A Kilosa jirani yake na Salange, amesema wengi wao walitarajia kesi hiyo ingechukua muda mrefu lakini  kitendo cha Mahakama kuisikiliza haraka na kutoa hukumu kali kwa mshtakiwa ni jambo la kupongezwa.

“Tulitaka kuona haki ikitendeka, mimi nilikuwa jirani yake, wale watoto alikuwa anawafungia ndani, walikuwa hawaruhusiwi kucheza na wenzao hapa mtaani, lakini hata yeye alikuwa hana ushirikiano na sisi majirani, kwa ufupi nimefurahi kusikia amefungwa,” amesema Onesmo.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Kimamba A, wilayani Kilosa, Edehati Haule amesema;

“Mwanzo nilimuona mtu wa maana, hata alivyokuja kwangu kujisajili kwenye daftari la mtaa alijisajili kwa jina la Yusuph Khalfani, kumbe aliamua kubadili majina ili asifahamike kiurahisi kutokana na tabia zake mbaya.”

Mwenyekiti huyo ametoa wito kwa viongozi wa Serikali za mitaa, kuwa makini na wageni wanaohamia mitaani kwao.

“Watu wote si wema, anaweza kuja akiwa mstaarabu kama huyu niliyempokea mimi, kumbe ni chui aliyejivisha ngozi ya kondoo,” amesema mwenyekiti huyo.

Alipotafutwa kwa simu babu wa aliyefanyiwa ukatili, Taris Ngongolwa ambaye kwa sasa yuko Moshi mkoani Kilimanjaro, amesema taarifa za kifungo cha Salange amezipata kupitia redio.

“Ni kweli taarifa za hukumu ya kesi ya ukatili wa mjukuu wangu nimezipata leo asubuhi kupitia redio wakati wanasoma magazeti, nilipigiwa simu pia na majirani zangu kuniambia kuhusu hili, binafsi nimefurahi, naamini Mahakama itaendelea kutenda haki dhidi yetu, maana ametusababishia maumivu makubwa,” amesema Ngongolwa.

Hata hivyo, Ngongolwa amesema alitamani kuona Salange naye anahukumiwa kifo kwa sababu ameua.

“Hata wakati tunamzika mtoto wangu kule Iringa, niliwaambia waandishi wa habari kwa kuwa ameua natamani na yeye ahukumiwe kunyongwa, lakini Mahakama ina sheria zake, tunashukuru hata kwa uamuzi huu,” amesema.