Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

‘Muwaamini makandarasi wazawa, wapeni mikopo’

Utiaji saini mkataba wa ujenzi wa majengo ya chuo kikuu cha Dodoma kampasi ya Njombe uliofanyika mkoani Njombe.

Muktasari:

  • Ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Kampasi ya Njombe awamu ya kwanza, utajumuisha ujenzi wa miundombinu sita ya msingi ndani ya kipindi cha mwaka mmoja na kugharimu Sh17.2 bilioni.

Njombe. Taasisi za kifedha nchini zimeshauriwa kuwaamini na kuwapa kipaumbele wakandarasi wazawa kwa kuwapatia mikopo, ili watekeleze miradi ya Serikali kwa ufanisi na kwa wakati, bila vikwazo vya kifedha.

Wito huo umetolewa leo, Jumatatu Mei 12, 2025 na Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka, wakati wa hafla ya kusaini mkataba wa ujenzi wa majengo ya Kampasi ya Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) mkoani Njombe.

Ujenzi huo unafanyika chini ya Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET).

Mtaka amesema ili uchumi wa Taifa ujengwe kwa misingi imara, kunahitajika kuaminiana kati ya taasisi za kifedha na Watanzania, ambapo benki ziwe tayari kutoa mikopo kwa wakandarasi wazawa na makandarasi hao wawe waaminifu katika kurejesha mikopo hiyo.

Mkuu wa mkoa wa Njombe Anthony Mtaka akizungumza mara baada ya kushuhudia utiaji saini mkataba wa ujenzi wa majengo chuo kikuu cha Dodoma kampasi ya Njombe.

Ameongeza kuwa Serikali ina miradi mingi ya ujenzi inayoendelea, hivyo ni muhimu kwa taasisi za fedha kutoa mikopo yenye masharti nafuu na kupunguza urasimu, ili kuwawezesha wakandarasi wa ndani kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa miradi hiyo.

"Endapo wakandarasi wazawa wataaminiwa na kufanya kazi kwa viwango vinavyotakiwa, wataendelea kuaminiwa zaidi na kupewa miradi mingine kutoka katika wizara mbalimbali," amesema Mtaka.

Aidha, amewasihi makandarasi kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa ubora unaotakiwa ili kujenga uaminifu kwa Serikali.

“Tuanze kuwaamini watu wetu. Hapa mkandarasi mshauri ni Mtanzania, anayejenga ni Mtanzania, na vifaa kama saruji atanunua madukani hapa hapa kwetu. Hii ni fursa kwa Watanzania kupata ajira,” amesema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Dodoma, Profesa Rwekaza Mukandala amesema uamuzi wa Serikali wa kuanzisha vyuo vikuu katika mikoa mbalimbali nchini unaonesha jinsi inavyozingatia mazingira halisi ya kila eneo.

"Chuo hiki kizingatie mazingira ya hapa Njombe, kama ni eneo la parachichi au uchimbaji, viwe vipengele vya kuzingatiwa katika mitaala, lakini bila kupoteza mwelekeo wa kitaifa na kimataifa," amesema Profesa Mukandala.

Naibu Mratibu wa Mradi wa HEET, Dk Happiness Nnko amesema Sh17.2 bilioni zimetengwa kwa ajili ya awamu ya kwanza ya ujenzi wa miundombinu ya kampasi hiyo.

Amesema ujenzi huo unatarajiwa kukamilika ndani ya siku 365, sawa na mwaka mmoja.

Mkandarasi anayesimamia ujenzi huo, Dickson Mwipopo, akizungumza katika hafla hiyo, amesema iwapo makandarasi wazawa wataendelea kupewa fursa na kuungwa mkono na Serikali, wataweza kujitegemea na kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya taifa.

"Tukipata viongozi kama Mtaka wanaotutetea, hata wakifika kumi tu, tunaweza kulijenga taifa kwa nguvu zetu wenyewe," amesema Mwipopo.

Baadhi ya wadau walioshiriki hafla ya utiaji saini mkataba wq ujenzi wa majengo ya chuo kikuu cha Dodoma kampasi ya Njombe.

Kwa niaba ya wananchi wa Njombe, Frank Msuya ametoa shukrani kwa Serikali kwa kusikia kilio cha muda mrefu cha wananchi wa mkoa huo waliotamani kuwa na chuo kikuu.

"Ndoto yetu sasa inatimia. Kupitia elimu tutakayopata hapa, tutajenga maarifa yatakayochochea maendeleo ya uchumi wa mkoa na taifa kwa ujumla," amesema Msuya.