‘Mti wa mtandao’ unavyokusanya wanakijiji kutuma, kupokea ujumbe
Muktasari:
Ule utani wa “kama mtandao unasumbua panda juu ya mti” si wa kubuni; wakazi wa kijiji cha Matuli, Ngerengere mkoani Morogoro wanauelewa vizuri.
Morogoro. Ule utani wa “kama mtandao unasumbua panda juu ya mti” si wa kubuni; wakazi wa kijiji cha Matuli, Ngerengere mkoani Morogoro wanauelewa vizuri.
Na kwao si kila mti unaweza kurahisisha mawasiliano; ni mmoja tu ambao hukusanya kila mwanakijiji anayehitaji mawasiliano kama ya kupokea ujumbe mfupi, fedha, kutuma ujumbe, kuzungumza au shughuli nyingine za mawasiliano.
“Usifikiri tunapenda kukusanyika hapa, tuna changamoto kubwa,” alisema mkazi wa kijiji hicho, Mohamed Rashid.
“Sijui lini kijiji hiki tutapata mawasiliano ya uhakika. Tunaziomba kampuni za simu zitufikirie.
“Ukija kuzungumza hapa hakuna siri. Aliye jirani yako atasikia kila unachozungumza. Kwa kweli hata kiuchumi ni ngumu kufanya biashara ikizingatiwa huku tunalima sana mpunga.’’
Eneo hilo ambalo lina mti mkubwa unaelezwa kuwa ndio sehemu ambayo mitandao mbalimbali ya simu inapatikana.
Ili kupunguza maumivu ya kunyanyua simu juu ili kusaka mtandao, vijana wa kijiji hicho wametengeneza makopo yanayoning’inia kwa ajili ya kuweka simu.
Mwenye simu katika kijiji hicho chenye watu takriban 5,000 huenda eneo hilo na kusubiri mtandao wake uunganishe na baadaye kufanya mawasiliano anayotaka, iwe ni kupiga simu au kusoma ujumbe.
Hali hiyo inawakosesha raha wakazi wa kijiji hicho wanaopaza sauti zao kuomba kusaidiwa kupata mawasiliano ya uhakika kutoka kampuni za huduma za simu za mkononi ambazo hutumia minara kwa ajili kuwezesha kupatikana maeneo mbalimbali.

Mgunduzi wa eneo
Eneo hilo halikugundulika kwa kutumia sayansi kubwa.
Yusuph Athuman, aliyetoka Dar es Salaam na kuwa na haja ya kufanya mawasiliano, ndiye aliyegundua kuwa eneo hilo lina mtandao kampuni tofauti za simu kabla ya kuwajulisha wengine.
“Mimi nilitoka Dar na simu. Nilipofika Ngelengele mawasiliano yakakata. Nikiwa nazunguka kutafuta mtandao, nikaona hapa chini ya mti angalau mnara unasoma,” alisema Athuman.
“Kuanzia hapo nikawa nakuja hapa kupiga simu zangu au kutuma ujumbe, na taratibu watu waliokuwa na simu wakaanza kupatumia hapa.”
Mkazi mwingine wa kijiji hicho, Seleman Mkomwa ambaye ni wakala wa huduma za fedha, alisema kutokana na hali hiyo hana sababu ya kuwa na kibanda kwa kuwa miamala yote anaifanyaa chini ya mti huo.
Alisema mara nyingi anakuwa jirani na mti huo au wakati mwingine wateja wanaohitaji kutoa au kuweka fedha humfuata nyumbani kwake na kuambatana nao hadi chini ya mti huo wa mtandao.
“Haya ndio maisha yetu na tumezoea. Wateja wananitafuta nilipo na ninakuja nao hadi hapa. Nafanya miamala na kuwapatia fedha au kuweka kwenye simu zao,” alisema.
Wapo wanaoniamini na kunipa simu na namba zao za siri na simu ili shughuli zote nifanye na kumpelekea pesa. Nimefanya uwakala kwa miaka sita sasa kwa kutumia mtandao unaopatikana eneo hili.”
Mbunge wa jimbo la Morogoro Kusini Mashariki, Hamis Taletale alisema anatambua kuwepo kwa changamoto hiyo na tayari ameanza kufanyia kazi.
“Kuna changamoto ya mawasiliano, si hapa tu bali katika maeneo kadhaa ya jimbo langu,” alisema Taletale.
“Nimezungumza na kampuni za simu na wametaka kujua idadi ya watu huku. Bado tupo katika mazungumzo, lakini ahadi iliyopo ni ndani ya miezi mitatu mawasiliano yatapatikana.”