Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hatima kaya 171 zilizokataa uthamini Kigoma kujulikana Aprili 25

Baadhi ya wakazi wa kijiji cha Kalilani mkoani Kigoma walioridhia kufanyiwa uthamini wakikabidhiwa hundi ya malipo.

Muktasari:

  • Tayari Serikali imelipa Sh1.68 bilioni kwa Kaya 205 zilizoridhia kufanyiwa uthamini na kupisha eneo hilo, huku hatima ya kaya 171 zilizotajwa kukataa kuhama ikiwa haijulikani hadi itakapofika Aprili 25, 2025, tarehe ambayo ni ya mwisho kwa wana kijiji hao kuhama kwa hiari.

Kigoma. Serikali Wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma imesema haitofanya uthamini kwa kaya 171 zilizogomea kwa awamu mbili tofauti ili kupisha upanuzi wa hifadhi ya milima ya Mahale inayoendeshwa na Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa), utakaosaidia kulinda ikolojia ya wanyama aina ya sokwe wanaopatikana katika hifadhi hiyo.

Pia, imesisitiza kuwachukulia hatua za kisheria wananchi ambao hawatahama katika maeneo ya hifadhi hiyo ifikapo Aprili 23, 2025 ikiwa ni tarehe ya mwisho katika siku 60 walizopewa kuondoka eneo hilo.

Kwa zaidi ya miaka 30, kumekuwa na mgogoro wa kubishania mipaka kati ya Tanapa na wananchi wa Kijiji cha Kalilani na vitongoji vyake.

Tanapa wanadai kuwa wananchi wanaishi ndani ya hifadhi ya milima ya Mahale, huku wananchi wakihoji kuwa wapo nje ya hifadhi, kulingana na tangazo la Serikali Namba 263 la mwaka 1985 kuhusu uanzishwaji wa hifadhi hiyo.

Kijiji cha Kalilani kilianzishwa rasmi Juni 15, 1995, miaka kumi baada ya tangazo hilo, chini ya usajili wa Mamlaka ya Serikali za Mitaa (KGM-182-09003026).

Hata hivyo, baada ya uthaminishaji ulioanza Agosti 3, 2025 pamoja na vikao na Serikali kaya 205 zilikubali kufanyiwa uthamini na kaya 171 zilikataa zikidai wao ni wakazi halali wa kijiji hicho na hawako tayari kupisha upanuzi huo, huku Tanapa ikiwataka kuondoka kutokana na kujenga ndani ya hifadhi hiyo.

Akizungumza na Mwananchi leo Aprili 3, 2025 Mkuu wa Wilaya ya Uvinza, Dinah Mathamani amesema kuwa waliazimia kutofanya uthamini kwa mara ya tatu na  waliogomea huenda si wenyeji wa Tanzania.

"Tulifanya uthamini mara mbili; awamu ya kwanza mwitikio ulikuwa mdogo, lakini awamu ya pili mwitikio ulikuwa mzuri na jumla ya kaya 205 walikubali kufanyiwa uthamini na wameshalipwa fedha zao.

“Baadhi yao wameshaanza kuhamisha vitu vyao. Hata hivyo, familia 171 waligomea na walieleza kuwa wako tayari kwa lolote. Tulipofanya uchunguzi, tuliona kuwa pengine baadhi yao si raia wa Tanzania, kwani ikiwa wengine wameshalipwa, wao kwa nini wakatae?" amesema Mathamani.

Ameongeza; “Pengine hawana sifa za kuwa raia walivamia tu, unajua maeneo yale ni karibu na kuelekea Congo, kwa hiyo kuna watu walikuja kwa njia isiyo halali wanakaa pale ni wavuvi wanaendelea na shughuli zao, kwa hiyo wale ambao wamekataa hatuna muda tena wa kubembeleza.”

Amesema kaya 205 zilizofanyiwa uthamini na kulipwa zimeanza kutafuta makazi mapya katika vijiji jirani.

Mathamani Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Dunia ikiahidi kuboresha na kujenga miundombinu muhimu kama shule, barabara na huduma za afya ili kuwasaidia wakazi hao katika maeneo walikohamia.

"Tulikubaliana kuangalia vijiji jirani kuboresha huduma kupitia wenzetu wa Benki ya Dunia itawasaidia wale ambao wamehama katika vipengele vidogovidogo ili waboreshewe maisha yao kwa kuwajengea shule, hospitali,” amesema.

Kaimu Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Milima ya Mahale, Haridi Mgofi amesema kuwa wananchi wameanza kuondoka baada ya kulipwa fidia.

Hata hivyo, amesema baadhi ya wale waliogomea kufanyiwa uthamini sasa wameonyesha nia ya kufanyiwa uthamini ili wapishe upanuzi wa hifadhi hiyo.

Ameongeza kuwa zimesalia wiki chache kabla ya kumalizika kwa kipindi cha siku 60 kilichotolewa na Serikali, ambapo tarehe ya mwisho ni Aprili 25, 2025.