Mradi wa maji wa Sh119 bilioni chanzo cha Mto Kiwira waanza

Muonekano wa chanzo cha maji katika Mto Kiwira Wilaya ya Rungwe Mkoa wa Mbeya kitakachozalisha lita 117 milioni kwa siku. Picha na Hawa Mathias
Muktasari:
- Mradi wa kimkakati wa maji una uwezo wa kuzalisha lita 117 milioni za maji kwa siku
Mbeya. Zaidi wakazi milioni moja wanatarajiwa kunufaika na mradi mkubwa wa kimkakati wa maji kutoka chanzo cha Mto Kiwira Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya ifikapo Machi 31,2025.
Mradi huo utakaozalisha maji lita 117 milioni kwa siku, kwa sasa uko kwenye hatua za ujenzi na usanifu kwa asilimia 98
Akizungumza na Mwananchi Digital Leo Jumamosi ,Mei 18,2024 Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira, Mhandisi Gilbert Kayange amesema utekelezaji wa mradi huo unakwenda kwa kasi kubwa.
"Mradi huu unatekelezwa na mamlaka kwa kushirikana na Wizara ya Maji, tunarajia ifikapo Mei 31,2024 saa 12.00 za jioni wananchi wataanza kupata majisafi na salama,"amesema Kayange.
Mhandisi Kayange amesema katika hatua nyingine wanaendelea na ujenzi wa banio kwa kuhamisha mto litakalokuwa na uwezo wa kukusanya lita milioni 12 kwa siku.
"Katika kuhakikisha mradi huu unakamilika kwa wakati, tunaendelea na ujenzi wa tenki kubwa la kuhifadhi maji eneo la New Forest litakalochukua maji zaidi ya lita milioni tano yaliyotibiwa tayari kwa ajili ya matumuzi kwa wateja,"amesema Mhandisi Kayange.
Pia, amesema kukamilika kwa mradi huo itakuwa mwarobaini wa changamoto ya huduma ya maji kwa wananchi Mkoa wa Mbeya.
Akizungumzia uwepo wa mradi huo, Mstahiki Meya wa Jiji la Mbeya, Dourmihamed Issa amesema utakuwa na tija sambamba na kuchochea shughuli za kiuchumi kwa wananchi kutotumia muda mwingi kusaka maji
"Kwanza niishukuru Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan na Mbunge wa Mbeya mjini na Spika wa Bunge,Dk Tulia Ackson kuweka msukumu kuwezesha mamlaka hiyo kupata fedha,"amesema.
Mkazi wa Mamlaka ya Mji wa Mbalizi, Mawazo Adamson amesema hali ya upatikanaji wa huduma ya maji ni changamoto.