Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

‘Kigoma kufunguliwa na miradi ya maendeleo'

Muktasari:

  • Wananchi wa Kakonko walikuwa wakipata huduma za afya kutoka Hospitali ya Bugando na Geita, imeelezwa uwepo wa hospitali hiyo sasa unasaidia kupunguza gharama ya kufuata huduma hizo nje ya wilaya na mkoa wao.

Kigoma. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko amesema Serikali imedhamiria kuipatia Kigoma miradi ya maendeleo na fursa mbalimbali, ili kuufungua mkoa huo kiuchumi.

Akihutubia katika mkutano wa hadhara katika Kata ya Kasanda Wilaya ya Kakonko leo Jumatano Septemba 18, 2024, Dk Biteko amesema Serikali imetekeleza miradi mingi ya maendeleo, ikiwamo ya hospitali na barabara mkoani humo ikilinganishwa na kipindi kilichopita.

Amesema wananchi walikuwa wakitembea umbali mrefu kufuata huduma mbalimbali za kijamii.

“Halmashauri hii (Kakonko) imeanzishwa mwaka 2013, maeneo mengi yalikuwa mapori, lakini leo tumetembelea Hospitali ya Wilaya ya Kakonko hali halisi ya maendeleo inaonekana. Rais wetu anataka Kigoma ifikike na watu wakae kwa amani na kufurahia kuwapo Kigoma, nimefurahi sana kuona majengo ya hospitali ya wilaya,” amesema Dk Biteko.

Awali, wananchi wa Kakonko walikuwa wakipata huduma za afya kutoka Hospitali ya Bugando na Geita, imeelezwa uwepo wa hospitali hiyo sasa unasaidia kupunguza gharama ya kufuata huduma hizo nje ya wilaya na mkoa wao.

Akizungumzia barabara ya Kakonko hadi katika mpaka wa Tanzania na Burundi, Naibu Waziri Mkuu Biteko amesema maisha ya wananchi ni kipaumbele kwa Serikali.

"Hatutaki maigizo kwenye maisha ya watu, tunataka kuwahakikishia kuwa hata barabara ya Nyakanazi–Kasulu hadi Kigoma itaunganishwa kwa lami. Rais Samia anataka kuona tunafanya biashara na majirani zetu na mtu kukaa mpakani si laana, bali ni fursa,” amesisitiza.

Amesema milango ya biashara itafunguliwa, na barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 48 kutoka Kakonko hadi mpakani itasimamiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads).

Amewapongeza wananchi wa Kakonko kwa kuzalisha chakula cha ziada tani 81,000, wakati mahitaji ya eneo hilo ni tani 76,000, hivyo kufanya akiba ya tani 157,000.

Katika hatua nyingine, Dk Biteko ametoa wito kwa viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kuhakikisha mchakato wa kura za maoni katika uchaguzi ujao wa serikali za mitaa unaendeshwa kwa uwazi na haki na kuwachagua wagombea wenye sifa, badala ya kutumia rushwa.

Awali, Naibu Waziri wa Tamisemi, Zainabu Katimba alisema Serikali imewekeza zaidi ya Sh4 bilioni kwa ajili ya majengo na vifaa tiba katika Hospitali ya Wilaya ya Kakonko.

“Napenda kutoa maelekezo kwa hospitali zote za wilaya nchini, ziwe na wodi za watoto ili kupunguza vifo vya mama na mtoto,” amesema Katimba.

Hata hivyo, amesema vifo vya watoto wachanga vimepungua kutoka 556 hadi 104 kwa kila vizazi hai 100,000 na mafanikio hayo ni kutokana na jitihada za Rais Samia na Serikali yake.

Akizungumzia uwekezaji mkubwa katika barabara, amesema Wilaya ya Kakonko ilikuwa ikipokea Sh700 milioni kutoka serikalini kwa ajili ya ujenzi wa barabara.

Amesema baada ya Serikali ya Awamu ya Sita kuingia madarakani, fedha hizo zimeongezeka na kufikia Sh2.2 bilioni kwa barabara za dharura.

“Hivi ninavyozungumza tumetenga Sh450 milioni kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya kilomita moja kuelekea hospitali ya wilaya, ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma vizuri,” amesema.

Naibu waziri huyo naye amewahimiza wananchi wa Kakonko kujiandikisha kwenye daftari la wapigakura na kushiriki katika uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 27, 2024.

Mmoja wa wakazi wa Kakonko, Maita Paschal amesema kuwepo kwa hospitali ya wilaya ya Kakonko kumewasaidia kupata huduma karibu zaidi. "Huduma sasa ni nzuri na zipo karibu na nyumbani," amesema Maita.