Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kaya 1,404 kufidiwa kupisha uwanja wa ndege Mwanza

Mkuu wa Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza, Hasan Masala akizungumza  kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kata ya Shibula wilayani humo wakati akitatua mgogoro wa ardhi. Picha na Anania Kajuni

Muktasari:

 Mgogoro wa ardhi kati ya wakazi wa Kata ya Shibula wilayani Ilemela mkoani Mwanza na uwanja wa ndege wa mkoa huo umefikia tamati baada ya Serikali kuridhia kufanya tathmini upya kwa wananchi wanaoishi eneo hilo

Mwaza. Mgogoro wa ardhi kati ya wakazi wa Kata ya Shibula wilayani Ilemela mkoani Mwanza na uwanja wa ndege wa mkoa huo umefikia tamati baada ya Serikali kuridhia kufanya tathmini upya kwa wananchi wanaoishi eneo hilo ili walipwe fidia kupisha upanuzi wa uwanja huo. 

Mgogoro huo uliodumu kwa miaka saba tangu 2017, uliibua sintofahamu miongoni mwa wanaomiliki maeneo katika kata hiyo huku wengine wakihofia kukosa stahiki yao ya kulipwa fidia. Hata hivyo, wananchi hao wamechekelea baada ya uamuzi wa fidia kutagazwa. 

Wakielezea mgogoro huo katika mkutano wa hadhara ulifanyika leo Alhamisi Machi 21, 2024 katani hapo na kuongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Hasan Masala, wananchi hao wamesema shauku yao kubwa ilikuwa ni kuona maeneo yao yanafanyiwa uthamini ili kupata fidia na kuondoka.

“Sisi tumechukua viwanja hapa tangu 2012 tukaweka mchanga safari kumi za magari, likaja tamko kwamba tusiendeleze chochote na sisi tukakaa bila kuendeleza lakini tukashangaa mtu mwingine akanunua kiwanja karibu na eneo letu na akaanza kujenga huku akisema hawarudi tena sasa itakuwaje kwa mimi ambaye sikuendeleza kwa sababu ya kutii amri ya Serikali na je yule aliyeendeleza tutalipwa sawa au tofauti," amehoji Vijinia Fredy, mkazi wa eneo hilo

Akiunga mkono hoja hiyo, John Zabron, mkazi wa eneo hilo amesema kutokana na unyeti na ukubwa wa tatizo hilo wananchi hao wanatakiwa kupatiwa fidia haraka ili kupunguza migogoro ya ardhi.


“Mkuu wa wilaya na timu ya viongozi walio chini yako tunapozungumzia ardhi ni suala nyeti sana kwa sababu hicho ndicho kinachowezesha maisha ili mtu aendelee kuwako kwa hiyo sio suala la kuangalia juu juu ndugu zetu Waisrael na Palestina saizi wanapigana lakini chimbuko ni ardhi kwa sababu ni nyeti sana kwahiyo naomba mtutatulie changamoto hii,” amesema.

“Ardhi ni bidhaa adimu sana tunaweza kusema hii ni bidhaa ya kimataifa naomba iende sambamba na fidia tunayostahili na hapo niseme tu fidia ya ardhi haiwezi kufanana na fidia za nyumba za kutolea huduma kama kanisani au shule,” amesema Zabron.

Akizungumza na wananchi hao, Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Hasan Masala amesema pamoja  awali kuwepo na hoja kinzani kuhusu mgogoro huo, Serikali imeona kuna ulazima wa kufanya uthamini wa maeneo hayo kwa manufaa ya wananchi hao na Taifa kwa jumla.

“Maswali mengi yameulizwa hoja ya msingi hapa ambayo mmetamani kujua ni suala la ardhi, sasa suala la ardhi na maendelezo yote yaliyopo naomba tuyafanyie kazi, nyote mliofanya maendelezo, maeneo yaliyoko juu ya ardhi kwa maana ya viwanja vyote vitafanyiwa uthamini," amesema.

“Zoezi hili halihitaji kukwamishwa kwa hali yoyote ile kama kuna kauli chafu zinatolewa, kama kuna matendo yanayoashiria udanganyifu naomba msikae kimya namba mnazo na ofisi mnazijua mimi kama kiongozi ninayeongoza zoezi hili nipo na ofisi ya kamishina ipo wazi,” amesema Masala.

Mthamini Mwandamizi kutoka Ofisi ya Kamishina wa Ardhi Mkoa wa Mwanza, Silas Honga amesema zoezi la uthamini linatarajia kuanza Machi 27 mwaka huu ikiwa ni pamoja na kutambua maeneo yote katika kata hiyo.

"Katika zoezi letu hili tunaenda kufanya kazi ifuatayo kwanza ni kutambua maendelezo yote yaliyopo katika eneo letu kwa maana ya majengo, miti, makaburi na mengine lakini pia tutatoa malipo kwa wananchi ya maendelezo yatakayobainika na hii itakuwa katika awamu ya kwanza," amesema Honga.

Diwani wa kata hiyo, Swila Dede ameshauri suala la uthamini kufanyika kwa hatua katika ngazi ya mtaa ili kuepusha makosa ya kuruka watu na kupunguza migogoro inayoweza kujitokeza.

"Tunatakiwa tuweke vizuri suala hili tunapofika kwenye uthamini, kunatokea migogoro mingi mtaalamu yupo mtaa A anaruka kwenye mtaa F sasa hiyo huwa inaleta changamoto na kupunguza ufanisi wa kazi kwahiyo mimi napendekeza tuende mtaa mmoja tuna maliza baadaye tunahamia mtaa mwingine na mwingine mpaka tunamaliza kwahiyo naomba wekeni ratiba wapi tutaanzia," amesema Dede.