'Fomu za Urais, ubunge zitolewe bure'

Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), Profesa Ibrahim Lipumba
Muktasari:
- Ili kutoa ruhusa ya wananchi kushiriki kuwania nafasi za uongozi, wadau wamependekeza fomu za uchaguzi zitolewe bila malipo.
Dar es Salaam. Umefikiria itakuwaje iwapo fomu za kugombea nafasi mbalimbali za uongozi ukiwemo urais, zitatolewa na kurudishwa bila gharama yoyote.
Pengine kichwani mwako, linakuja wazo la kuwepo utitiri wa watakaojitokeza kuwania nafasi za uongozi, lakini hiyo ndiyo demokrasia yenyewe.
Kwa sasa, sheria imataka mtu anayewania nafasi ya urais wa Jamhuri ya Muungano, fomu yake itahesabiwa kuwa imekamilika, iwapo itarudishwa ikiwa imeambatishwa na ada ya Sh1 milioni, huku za ubunge zikihitaji mgombea kulipia Sh100, 000, jambo linalotajwa na wadau wa siasa kuwa kikwazo cha demokrasia.
Hoja kuhusu kutolewa bure kwa fomu hizo, imeibuka kama moja ya maazimio ya mkutano wa kitaifa wa wadau uliojadili kuhusu hali ya demokrasia nchini.
Hayo yameelezwa jijini Dar es Salaam leo, Jumatano Agosti 23, 2023 na Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), Profesa Ibrahim Lipumba aliposoma maazimio ya washiriki wakati wa kuhitimisha mkutano huo.
Profesa Lipumba amesema kulingana na wadau wa demokrasia, katika mabadikiko ya sheria ya uchaguzi, wanapendekeza kuondewa kwa gharama za kuchukua fomu na kurejesha fomu.
"Nakumbuka kwenye urais, inahitajika ukirudisha fomu upeleke na Sh1 milioni, sasa kuna watu wanataka kugombea urais na hiyo hela hawana, wapo wanaosema unawezaje kuwa Rais wakati huna Sh1 milioni.
"Unaweza kuwa huna Sh1 milioni lakini una mawazo mazuri ya kuwaletea Watanzania, kwa hiyo kiondolewe kikwazo hicho," amesema.
Hata hivyo, amesema hatua hiyo itaongeza idadi ya wagombea na hivyo kuimarika kwa demokrasia nchini.