CAG ataka tume huru Plea Bargaining

Mdhibiti na Mkaguzi wa Serikali, Charles Kichere.
Dar es Salaam. Juzi Mdhibiti na Mkaguzi wa Serikali, Charles Kichere alisema kunahitajika tume huru ya kuchunguza matumizi mabaya ya ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Serikali (DPP), akisema pamoja na mengineyo, fedha zilizotaifishwa kupitia utaratibu wa Plea Bargaining, ziliwekwa kimakosa katika akaunti ya makubaliano ya hiari, badala ya akaunti ya utaifishaji mali.
Alisema fedha zilitaifishwa na kukabidhiwa hazina bila kupitia akaunti maalum ya utaifishaji mali.
Kichere alipendekeza kuundwa tume huru ya uchunguzi wa matumizi mabaya ya madaraka ya ofisi hiyo.
Akizungumzia hilo, Rais Samia alisema tayari uchunguzi huo unafanywa chini ya Tume ya kurekebisha mfumo wa haki jinai.
Mashirika ya umma
Rais Samia aliiagiza Wizara ya Fedha na Mipango kusimamia mashirika yote ya umma yasiyolipa kodi ya zuio na yale yaliyokata lakini hayajawasilisha, kuhakikisha yanatekeleza hilo.
“Zilipwe na kuwe na nidhamu ya kufanya kazi, hata kama ni majeshi hata wao kama wanataka kulipa kodi ya zuio walipe, wote waliotakiwa kulipa walipe na kuwe na nidhamu katika maeneo hayo,” alisema.
Samia aliyasema hayo wakati akijibu kile kilichobainishwa na CAG Charles Kichere kuwa mashirika 21 hayakukata na kuwasilisha kodi ya zuio kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kiasi cha Sh749.53 milioni.
Kati ya taasisi hizo, alisema 15 hazikukata kodi ya zuio na sita zilizuia, lakini hazikuwasilisha TRA kiasi cha Sh35 milioni, kinyume na sheria ya kodi.
Alizitaja taasisi hizo ni kuwa ni Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) ambayo haikukata Sh442 milioni, Kampuni ya Ujenzi ya Jeshi la Kujenga Taifa Sh162 milioni, Ruwasa Sh56 milioni, Wakala wa Huduma za Ununuzi Serikalini (GPSA) Sh34 milioni.
Bima ya afya
Katika upande wa bima ya afya, uchunguzi huo wa CAG ulibaini huduma kwa wanachama wa mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ni kubwa ukilinganisha na michango yao.
CAG Kichere alisema katika mwaka 2021/2022, mfuko umepata hasara ya Sh189.65 bilioni ikilinganishwa na Sh93.6 ilikuwapo mwaka uliotangulia.
“Pia mfuko umekuwa na mtiririko hasi wa fedha katika shughuli zake za uendeshaji, mwenendo huu unaonyesha kuwa michango inaongezeka kwa asilimia 12.9 wakati matumizi yanaongezeka kwa asilimia 24.6 mara mbili,” alisema Kichere.
Alisema makadirio ya uwezo wa mfuko kujiendesha kwa Juni 30, 2021, unaonyesha kuwa mapato yake yataendelea kuwa chini ya matumizi kwa siku zijazo na utatumia ziada iliyokusanywa jambo ambalo litasababisha ukwasi kuwa hasi ifikapo mwaka 2025.
“Napendekeza kufanyiwa kazi kwa mapendekezo ya ripoti ya wataalamu na kutekeleza yaliyohitajika ili kurekebisha nakisi kama vile kuimarisha usimamizi wa utoaji huduma za afya.
Ukaguzi wa udhibiti wa malipo ya Mfuko wa Bima ya Afya ulibaini madai yasiyostahili kutoka vituo vya huduma vya afya kati ya 2019/20 na 2021/22 yalisababisha malipo ya Sh10.3 bilioni kwa vituo binafsi, Sh1.58 bilioni vya Serikali na Sh2.49 kwa taasisi za kidini.
Akizungumzia hilo, Rais Samia alisema atalitengea siku rasmi ya kuliongelea kwani kwa hali ilivyo mfuko unaweza usifike mwaka 2025.
Bwawa la Nyerere
Kuhusu mradi wa Bwawa la Nyerere, alisema kuchelewa kwa mradi huo, kunatokana na haja ya kupitiwa upya kwa mikataba kwani masharti ya awali yasingeweza kutekelezeka.
“Imebidi tukae tupitie upya na tusogeze muda wa kutekeleza miradi, kwa hiyo wakati tunaingia mikataba na wajenzi tunapaswa kuwa makini,” alisema.
“Bora tuchelewe lakini ukamilike kwa uhakika, mbele huko likibomoka mimi sina cha kuwaambia wananchi,’’ alisema.