‘Bye Dad, Bye mum’

Muktasari:
- “Bye dady, bye mamy.” Hayo ndio maneno ya mwisho ambayo watoto wawili kati ya tisa wa familia moja waliofariki dunia katika ajali ya basi la shule, waliyatoa wakiwaaga wazazi wao kabla ya kuondoka nyumbani kwenda shule.
Mtwara. “Bye dady, bye mamy.” Hayo ndio maneno ya mwisho ambayo watoto wawili kati ya tisa wa familia moja waliofariki dunia katika ajali ya basi la shule, waliyatoa wakiwaaga wazazi wao kabla ya kuondoka nyumbani kwenda shule.
Watoto hao, Johari (7) na Emmanuel (5) waliwaaga wazazi wao Simon Joel na Stella Yohana kwenda kuungana na wenzao, wakiwemo tisa ambao pamoja na nao, walipoteza maisha katika ajali iliyotokea jana asubuhi.
Ajali hiyo ilitokea eneo la Mjimwema, Kata ya Mikindani, Mtwara Mjini na kusababisha vifo vya watu 13, kati yao ni wanafunzi 11 wa Shule ya Msingi ya King David na watu wazima wawili, akiwemo dereva wa gari hilo aina ya Toyota Hince na mwanamke mmoja aliyekuwa amepewa rifti. Ajali hiyo ilisababisha majeruhi 17.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Nicodemus Katembo akizungumza katika Hospitali ya Rufaa Ligula alisema chanzo cha ajali hiyo ni kufeli kwa breki za gari lililokuwa limewabeba wanafunzi hao.
Katembo alisema baada ya gari kufeli breki limemshinda dereva na kuingia kwenye korongo na kusababisha wanafunzi wanane na watu wazima wawili kufa papohapo.
Hata hivyo, baadaye wakati wa shughuli ya kuaga baadhi ya miili ya wanafunzi watatu na wakubwa wawili, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Brigedia Jenerali Marco Gaguti aliwaeleza waombolezaji kuwa wanafunzi wengine wawili wamefariki dunia na kufanya idadi ya waliokufa kufikia 13.
Gaguti alisema majeruhi watano walipelekwa Hospitali ya Rufaa ya Ndanda mkoani humo kwa matibabu na majeruhi wote 15 Serikali itawagharamia huku ikitoa ubani wa Sh300,000 kwa kila mfiwa.
Alisema katika miili ya marehemo ipo itakayosafirishwa na itakayozikwa mkoani humo na Serikali itasimamia maziko hayo.
“Siku ya leo ilianza kama siku nyingine zozote kulikuwa na jua upande wa magharibi kukiwa na nuru lakini nuru hiyo haikuwa endelea, Mkoa wa Mtwara umefunikwa na giza kwa siku nzima,” alisema Gaguti wakati wa shughuli ya kuaga miili katika Hospitali ya Rufaa ya Ligula.
Awali, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Dk Hamad Nyembea alisema majeruhi 18 kati yao 12 ni wa kike na sita wa kiume.
Mashuhuda wa ajali hiyo, Waziri Masoud alisema alikuwa wa kwanza kufika eneo la ajali na kusaidia katika uokoaji.
Alisema wakati akiendelea kufanya usafi shambani kwake, alishtuliwa na sauti ya gari ambayo ilikuwa ikishuka kwa kasi na kuingia shimoni kisha watoto wakaanza kupiga kelele.
Baada ya kusikia kelele hizo, alikwenda pamoja na kijana aliyekuwa naye akikata kuni wakaanza kuwatoa majeruhi lakini ilifika wakati wakashindwa na kuamua kupiga simu mjini ili kupata msaada wa polisi.
“Barabara inatakiwa kuboreshwa, hapa kungekuwa na hali nzuri kungepunguza ukali wa ajali, lakini hivi ilivyo ndiyo kumeifanya ajali iwe hivi ilivyo,” alisema Masoud huku Raymond Simon, shuhuda mwingine akitoa wito kwa Serikali kuboresha barabara hiyo ikiwemo kuwekwa mitaro ili kusaidia maji ya mva yasiiharibu.
Ni ajali iliyozua simanzi maeneo mbalimbali ikiwemo mitandaoni na Rais Samia Suluhu Hassan akitumia ukurasa wake wa twitter dakika chache baada ya kutokea akisema, “nimesikitishwa na vifo vya wanafunzi 8 wa Shule ya Msingi King David na watu wazima wawili vilivyotokea leo eneo la Mjimwema, Mikindani, mkoani Mtwara.”
“Natoa pole kwa wote waliopoteza jamaa zao. Mungu azilaze roho za marehemu mahali pema na awajalie majeruhi wapone haraka.”
Simulizi ya mama
Si kama ilivyozoeleka kwa wazazi kuachana na watoto wao asubuhi kwenda shule na wao kazini kisha kukutana tena jioni. Familia ya Simon Chogwe, mfanyakazi wa Benki ya NMB ni miongoni mwa familia za watoto 11 ambazo hali kwa sasa ni tofauti.
Furaha ya watoto wao pekee, Johari (7) wa darasa la kwanza na Emmanuel (5) anayesoma awali imefutika. Hawana tena watoto na mama yao, Stella Yohana anasimulia jinsi ambavyo wamekuwa wakiagana.
Anasema ilikuwa tabia yao baada ya kuwaandaa, kama ilivyokuwa jana, kabla ya kuondoka asubuhi, kwenda kumuaga baba yao na mama yao kuwapeleka kwenye gari.
Akishindwa kujizuia, alijikuta akilia na kukumbuka namna alivyoagana na watoto wake pekee kwa mara ya mwisho asubuhi baada ya kuwaandaa.
“Huwa wakiwa wanaondoka huwa wanasema bye dady, bye mamy (kwaheri baba, kwaheri mama) hivyo ndivyo wamezoea. Siwezi kuelezea, uchungu wa mwana aujuaye mzazi,” alisema
Anasema watoto hao huchukuliwa na gari kati ya saa 12 asubuhi hadi saa 12:15 asubuhi jambo ambalo humfanya kuwaamsha na kuwaandaa mapema zaidi.
Anasema hadi ajali hiyo inatokea hakuwa na malalamiko juu ya ubovu wa gari wanalotumia watoto, ingawa kwa siku za nyuma suala hilo liliwahi kutokea.
Wakati kwa Stella akilia upweke aliobaki nao, Monica Jacob yeye anaangua kilio baada ya mtoto wake kunusurika. Mtoto wake pia alitakiwa kuchukuliwa na gari hilo.
“Kabla hawajapata ajali ndiyo walikuwa wanataka waje kumchukua mtoto wangu, kwa kawaida dada ndiye humleta mtoto barabarani lakini aliniambia mama mbona hawamfuati mtoto, nikasema ngoja nimpigie dereva,” anasimulia.
“Nilipompigia dereva simu yake haikuwa inapokelewa, ndipo bodaboda mmoja akaniambia gari inayompitia mwanao imepata ajali. Nimetoka nyumbani kuja hapa nakuta watoto wengine wamepoteza maisha na wegine wamejeruhiwa,” alisema Monica huku akishindwa kuzuia machozi.
Tutafunga kwa huzuni
Kwa mujibu wa ratiba, shule zote nchini zitafungwa kesho na Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Daniel Msilu akizungumza na gazeti hili alisema, “huu ni msiba mkubwa kwetu. Tunafunga shule Julai 28 (kesho) lakini kwa mazingira yalivyo tumesimamisha kuendelea na masomo kuanzia leo (jana).”
Mwalimu huyo alisema, “shule zilikuwa zinafungwa keshokutwa (kesho) lakini sisi tutafunga kwa stahili ya huzuni.”
Alisema shule hiyo yenye madarasa ya awali hadi darasa la saba imechukua uamuzi wa kuwarejesha nyumbani ili kutoa fursa ya kuomboleza msiba huo mkubwa.
Tatizo liko wapi?
Ajali za magari ya shule zinazua maswali mengi. Miongoni mwayo ni je, mamlaka zimekosa ufumbuzi?
Maswali hayo yanaendelea kuumiza vichwa vya Watanzania wakati basi la Shule ya Msingi King David limepata ajali jana na kusababisha vifo vya watu 11 na kujeruhi wengine 18 mkoani Mtwara.
Wakati Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Nicodemus Katembo akieleza chanzo cha ajali hiyo ni kufeli kwa breki, Kamanda wa kikosi cha Usalama Barabarani nchini Wilbroad Mutafungwa alisema basi hilo ni miongoni mwa mabasi 34 kati ya 49 yaliyokaguliwa na kuonekana hayana tatizo.
Mutafungwa alisema basi hilo lilikaguliwa Juni 13, mwaka huu ikiwa ni sehemu ya operesheni ya ukaguzi wa mabasi ya shule zote ulioanza Juni 4, mwaka huu na unaendelea katika mikoa 31 ya kipolisi nchini ili kuepuka ajali ambazo zimekuwa tishio kwa maisha ya wanafunzi.
Kumbukumbu mbaya
Ajali hii imeibua kumbukumbu mbaya ya ile ya Mei 6, 2017 iliyotokea baada ya basi la Shule ya Msingi Lucky Vincent kupinduka katika eneo la Rhotia, Karatu mkoani Arusha na kusababisha vifo vya wanafunzi 32.
Ajali nyingine kama hiyo ilitokea Machi 17, 2019 na kusababisha kifo cha mwanafunzi wa kidato cha nne Shule ya Sekondari Horten, Ramadhan Fikirini baada ya basi aina ya Toyota Coaster kugonga treni katika eneo la Dolphine jijini Tanga. Wanafunzi wengine 27 walijeruhiwa katika ajali hiyo.
Kufuatilia ajali hizo za mara kwa mara, Kamanda Mutafungwa alisema:
“Nimetuma maofisa Mtwara kwa ajili ya uchunguzi, ukikamilika ndiyo tutajua chanzo cha ajali lakini basi hilo lilikaguliwa na likaonekana kuwa na ubora, walitakiwa marekebisho kidogo kama wipper (vifuta vioo), nasisitiza mabasi yote ya wanafunzi yaletwe vituoni ili kujiridhisha na ubora wake,” alisema Mutafugwa.
Ukaguzi wenyewe
Kwa mujibu wa jeshi hilo, takwimu za ukaguzi uliofanyika kwa wiki mbili baada ya uzinduzi wa Juni 4, mwaka huu zinaonyesha jumla ya mabasi 2, 090 yalikaguliwa na kati yake 1,594 yalionekana mazima. Mabasi 359 yalikutwa na matatizo madogo, 137 yalikutwa na matatizo makubwa na kung’olewa namba.
Mutafungwa alisema ukaguzi huo umekuwa pia ukigusa ubora wa madereva, na wengi waliokaguliwa hawana uwezo wa kuendesha masafa marefu.
Licha ya hayo, baadhi ya wazazi jana walishauri Serikali ilazimishe wamiliki wa mabasi hayo kufunga mfumo wa GPS, unaofuatilia mabasi hayo mahali yalipo na mwendo wake ili kudhibiti ajali zinazotokana na makosa ya madereva.
“Wafunge GPS tu na polisi wazifuatilie wenyewe, kama wanaweza kusimamia mabasi mengi ya mikoa, hawawezi kushindwa mabasi haya kidogo, pia waondoe tozo ya uagizaji wa mabasi hayo ili kila shule iwe na mabasi yenye ubora,” alisema mkazi wa Segerea, jijini Dar es Salaam, Abdulfatah Lyeme.
“Kwa sasa hivi (mabasi) ni mabovu na wanarundika watoto kama nyanya, mie watoto wangu ninawapeleka shuleni na kuwarudisha, kwanza gharama kubwa, mizunguko inakuwa mingi mtoto anaingia darasani amechoka na wanarundikana sana kwenye basi,” alisema.
Hoja ya kufungwa mfumo wa GPS iliungwa mkono na Mutafungwa aliyeshauri mamlaka husika kusimamia suala hilo.
Nyongeza na Kelvin Matandiko
Ufuatiliaji, usajili
Hata hivyo, Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu (LATRA) imesema huwa inajiridhisha na ubora wa basi na dereva husika kupitia ripoti kutoka Jeshi la Polisi huku basi husika likitakiwa tayari kuwa na rangi ya njano.
Mkurugenzi wa udhibiti na usafiri wa huduma za barabara alisema baada ya hatua hiyo mamlaka hiyo itatoa leseni kwa basi husika chini ya Kanuni za Leseni za za usafirishaji wa abiria za mwaka 2020.
“Lakini dereva asiwe chini ya miaka 35, aje na ripoti ya ukaguzi wa jeshi la Polisi, tukishatoa leseni bado tutaendelea kuwafuatilia huko barabarani na kanuni zinamtaka mmiliki kulinda ubora wa gari lake linapokuwa na abiria (wanafunzi),” alisema Kahatano.