Zuma anavyoonja shubiri kabla ya Uchaguzi Mkuu

Rais Mstaafu wa Afrika Kusini, Jacob Zuma

Wakati Afrika Kusini ikielekea kwenye uchaguzi mkuu Mei 29, mwaka huu, Rais wa zamani wa nchi hiyo, Jacob Zuma anapitia changamoto lukuki tangu alipotangaza kutokiunga mkono chama chake cha zamani cha ANC na kuanzisha chama kipya cha uMkontho weSizwe (MK).

Mambo yanaendelea kumwendea mrama kiongozi huyo mstaafu ambaye licha ya kukulia ndani ya ANC tangu wakati wa harakati za kupambana na sera za ubaguzi wa rangi nchini humo, hata hivyo ameshikilia msimamo wake na kusonga mbele.

Zuma (81) amekuwa akimlalamikia Rais Cyril Ramaphosa na serikali yake kwa kuachana na miiko ya chama hicho, huku akimtuhumu kwa kuwakumbatia matajiri wachache na kuachana na wananchi wengi masikini ambao ndio wenye chama hicho.

Uamuzi wake wa kuachana na ANC unaelezwa kuwa pigo kubwa kwa chama hicho na unatishia ushindi wa chama hicho kutokana na nguvu kubwa ya ushawishi aliyonayo kwa wananchi wa kawaida nchini humo.

Tangu alipolazimishwa kujiuzulu urais mwaka 2018 kwa tuhuma za rushwa, Zuma hajawahi kuwa na uhusiano mzuri na chama chake na hata makamu wake wakati huo, Ramaphosa alipoingia mabadarakani, bado hawakuwa karibu.

Hata hivyo, hatua ambayo haikutarajiwa ni ile ya Septemba 7, 2023 ya Zuma kusajili chama chake cha siasa huku kikitumia jina na nembo za ANC, jambo ambalo linapingwa vikali na viongozi wa chama hicho.

Kadiri siku za uchaguzi zinavyosogea ndivyo kiongozi huyo anavyokumbana na changamoto lukuki mbele yake, huku yeye na wafuasi wake wakiamini viongozi wa ANC wako nyuma yake kwa lengo la kumkwamisha.

Ikumbukwe kwamba Mei 29, Rais Ramaphosa ambaye aliingia madarakani mwaka 2019 baada ya Zuma kujiuzulu, atatetea kiti chake kwa muhula wa pili wakati akikabiliwa na shinikizo kubwa ndani ya chama chake kutokana na tuhuma za ufisadi zinazomwandama.

Licha ya kuwepo kwa vyama vingine vyenye nguvu Afrika Kusini kama cha DA kinachoongozwa na John Steenhuisen na EFF cha Julius Malema, bado ANC kinapambana na MK cha Zuma kutokana na nguvu ya mwanasiasa huyo mkongwe.


Azuiwa kushiriki uchaguzi

Moja ya pigo alilokutana nalo Zuma kuelekea uchaguzi mkuu, ni lile la Tume ya Uchaguzi ya Afrika Kusini kumzuia kugombea katika uchaguzi mkuu wa Mei 29, licha ya kwamba hakuwahi kutangaza nia hiyo hadharani.


“Katika kesi ya Rais wa zamani (Zuma) ndiyo, tulipokea pingamizi ambalo limekubaliwa,” Rais wa Tume ya Uchaguzi, Mosotho Moepya aliwaambia waandishi wa habari, bila kutoa maelezo zaidi.

“Chama kilichomteua kimefahamishwa sambamba na wale wanaopinga hatua hiyo,” aliongeza kiongozi huyo wa Tume. Uamuzi huo ungeweza kukatiwa rufaa ikiwa ungewasilishwa kabla ya Aprili 2, mwaka huu. Zuma anakifanyia kampeni chama cha upinzani cha Umkhonto we Sizwe katika jaribio la kurudi upya kwenye taaluma yake na kukidhoofisha chama chake cha zamani cha ANC.

Uchaguzi mkuu, ambao baada ya mshindi atateuliwa rais, unawekwa kuwa wa mvutano.

Ushindi wa chama cha ANC unatarajiwa kushuka chini ya asilimia 50 ya kura kwa mara ya kwanza tangu kilipoingia madarakani mwishoni mwa enzi za ubaguzi wa rangi.

Hilo litakilazimisha chama hicho kilichowahi kuongozwa na Nelson Mandela, kuunda serikali ya umoja wa kitaifa ili kiendelee kubaki madarakani.

ANC kimepoteza uungwaji mkono kwa kipindi ambacho kuna mdororo wa kiuchumi, madai ya ufisadi na usimamizi mbovu serikali.

Tume ya uchaguzi ilisema katika taarifa yake kwamba kwa mujibu wa katiba, “mtu yeyote ambaye atapatikana na hatia kwa kosa na kuhukumiwa kifungo cha zaidi ya miezi 12 bila chaguo la faini, hawezi kushiriki uchaguzi.”

Zuma alihukumiwa kifungo cha miezi 15 jela Juni 2021, baada ya kukataa kutoa ushahidi kwa jopo lililokuwa likichunguza ufisadi wa kifedha na urafiki chini ya urais wake.

Mbali na hukumu yake kwa kosa la kudharau Mahakama mwaka 2021, anakabiliwa na mashtaka tofauti ya ufisadi katika kashfa ya ununuzi wa silaha katika miaka ya 1990, alipokuwa Makamu wa Rais.


MK kushiriki uchaguzi

Katika mwendelezo wa sarakasi hizo, chama cha ANC kilifungua kesi mahakamani kikitaka chama cha Zuma cha MK kisiruhusiwe kushiriki kwenye uchaguzi ujao kwa madai kwamba jina na nembo zinazotumiwa na chama hicho zinafanana na iliyokuwa jumuiya ya chama hicho.

Chama hicho kilidai jina la “uMkontho weSizwe” lilikuwa likitumiwa na ANC kama moja ya jumuiya zake kabla ya kupigwa marufuku mwaka 1993.

Pia, nembo ya chama hicho ya mtu akiwa ameshika mkuki na ngao, pia ilitumiwa na chama hicho, jambo ambali walidai litawachanganya wapigakura.

Hata hivyo, mahakama ya Johannesburg ilitupilia mbali madai ya ANC ikieleza kwamba hakuna uvunjifu wowote wa sheria uliofanywa na MK katika kusajili chama hicho Septemba 7, mwaka jana.

“Maelezo ya ANC hayana mantiki kwa sababu hayathibitishi sababu za kuchelewa kwao katika kuleta ombi hilo,” alisema Jaji Lebohang Modibale akinukuliwa na AFP.

Kura za maoni za hivi karibuni zinaipa MK asilimia 13 ya kura kitaifa. Chama hicho kinaweza kufanya vizuri hasa katika jimbo analotoka Zuma la KwaZulu-Natal ambalo ni la pili kwa idadi kubwa ya watu nchini Afrika Kusini, na idadi kubwa ya wafuasi wa ANC nchini humo.

MK kilitaka kusajiliwa kama chama cha siasa Juni 2023, lakini Tume ya Uchaguzi ilikataa hatua hiyo kutokana na upungufu uliobainika kwenye alama zake.

Chama hicho kilirekebisha na kuwasilisha tena ombi lake na kilisajiliwa rasmi Septemba, mwaka jana, mahakama ilieleza Jumanne iliyopita.

Miezi minne baadaye, chama cha ANC kilipinga hatua hiyo, kikisema jina la MK lililosajiliwa na alama yake vinafanana na zile za ANC, kwamba zinaweza kuwachanganya wapigakura.

Hata hivyo, Jumanne iliyopita, mahakama ilitoa uamuzi na kusema, ANC ilikuwa imechelewa na sababu ilizozitoa za kufanya hivyo hazikuwa na mashiko.


Akaunti yake yazuiliwa

Katika hatua nyingine, benki moja ya Afrika Kusini ilisema Jumatano iliyopita, mahakama iliamuru kusitishwa kwa malipo yanayotoka kwenye akaunti ya Zuma baada ya mzozo kuhusu mikopo ya uboreshaji wa nyumba yake binafsi akiwa madarakani.

Benki ya First National Bank (FNB) ilisema hatua hiyo ni matokeo ya hatua za kisheria zilizochukuliwa na wafilisi wa benki nyingine inayomdai mwanasiasa huyo mkongwe mwenye umri wa miaka 81.

“FNB iliagizwa na Mahakama Kuu kusitisha malipo yanayotoka kwenye akaunti ya Rais wa zamani, Zuma ya FNB.

Akaunti hizo hazijafungwa, kwani malipo yanayoingia hayaathiriwi,” FNB iliiambia AFP.

“Maagizo haya kutoka mahakamani yanatokana na mchakato unaosimamiwa kwa sasa na wafilisi, benki ya VBS na FNB ilitakiwa kisheria kufuata.

Msaada pekee kwa Zuma, sasa ni Mahakama na wafilisi, VBS.”

Hatua hiyo huenda ikachafua zaidi sifa ya Zuma, anayetuhumiwa kwa ufisadi kabla ya uchaguzi mkuu wa Mei 29.

Zuma, ambaye amekuwa madarakani kati ya mwaka wa 2009 hadi 2018, anaongoza chama kidogo kilichoanzishwa ambacho kinatishia kupokonya kura muhimu za chama mama cha ANC.

Kufungiwa kwa akaunti yake kunahusiana na ukarabati wa nyumba yake uliofanyika katika jimbo lake alilozaliwa la KwaZulu-Natal na kuibua utata, muongo mmoja uliopita.

Mwaka 2016, Mahakama Kuu iligundua kuwa rais wa wakati huo alitenda kinyume na katiba kwa kutumia mamilioni ya dola za serikali kukarabati nyumba yake iliyopo katika kijiji cha Nkandla kwa kile alichokiita “maboresho ya usalama”.