Utata kifo cha mfanyabiashara akiwa mapumziko na mpenzi wake

Australia. Familia ya mfanyabiashara raia wa Uingereza aliyefariki akiwa mapumzikoni na mpenzi wake wa miaka 25, inataka majibu ya kina kuhusu kifo chake, wakisema hawana ufahamu wowote kuhusu alikozikwa wala chanzo halisi cha kifo chake.
Allen McKenna, 47, alizirai ghafla na kufariki katika Jiji la Casablanca Februari,2025, akiwa na mpenzi wake wa Morocco, Majda Mjaoual.
Baba wa marehemu, Alan Moorhead, anayeishi Adelaide, Australia, amesema alipokea simu ya video kutoka kwa Mjaoual Februari 22, 2025 kuhusu kifo chake, huku akiona mwili wa mwanaye ukiwa pembeni ya Majda wakati wa mazungumzo hayo.

Ingawa inadaiwa McKenna alifariki kutokana na mshtuko wa moyo, familia yake haijapatiwa hati rasmi ya kifo wala taarifa ya daktari wa uchunguzi wa vifo.
Inasemekana McKenna alizikwa siku mbili tu baada ya kifo chake, kabla ya mpenzi wake kusafiri kuelekea Uingereza kwa ajili ya kushughulikia masuala ya marehemu, lakini mpaka sasa hajawafahamisha familia mahali ambako amezikwa.
McKenna, mzaliwa wa Harrogate, North Yorkshire, alisoma katika Chuo Kikuu cha Australia na wakati wa kifo chake alikuwa akiendesha kampuni tatu za Kiingereza, ikiwamo kiwanda cha pombe.
Familia yake, inayohangaika kwa huzuni, sasa inataka kufahamu mahali alipozikwa mwanafamilia huyo.
“Inavunja moyo, sijui niende wapi, sijui nifanye nini,” amesema kwa uchungu Moorhead wakati akizungumza na kituo cha habari cha 9News.
“Alistahili heshima, alistahili kurudishwa hapa Australia ili familia nzima ipate faraja na hitimisho la maisha yake.

“Ni jambo lisiloaminika. Hajibu ujumbe wowote wala simu, amekaa kimya kabisa. Ninachotaka ni kumrudisha mwanangu nyumbani,” amesema.
Rafiki wa karibu wa marehemu, Mark Parsons, pia ameiambia 9News: “Bado siamini kama ni kweli ... Sitapata tena rafiki kama McKenna maishani mwangu.”
Akaongeza: “Ni muhimu sana, nataka kuwa na kumbukumbu ya pamoja, mazishi na mahali pa kwenda kumtembelea.”
Taarifa kutoka mitandao ya kijamii zinaonesha kuwa McKenna alikuwa pia mpenzi wa mazoezi ya viungo na alishiriki mashindano ya kujenga mwili.
Moorhead amekuwa akieleza machungu yake waziwazi kupitia mitandao ya kijamii, akiomba msaada na majibu kuhusu kifo cha mwanaye.
Katika moja ya machapisho yake, alijieleza kama “baba mwenye majonzi” ambaye anahangaika kujua mahali mwanaye alipozikwa.
Moorhead, ambaye sasa anaishi Adelaide, anasema anataka kuurudisha mwili wa mwanaye nyumbani Australia nchi aliyokulia.
Msemaji wa Ofisi ya Mambo ya Nje ya Uingereza ameliambia Daily Mail: “Tunaendelea kuisaidia familia ya raia wa Uingereza aliyefariki huko Morocco na tuko katika mawasiliano na mamlaka za eneo hilo.”
Wakati huo huo, Jeshi la Polisi la North Yorkshire, Idara ya Mambo ya Nje ya Australia, na Shirika la Polisi wa Kimataifa (Interpol) wanaripotiwa kuendesha uchunguzi kuhusu tukio hilo.