Pasta adai wasanii Bongo Flava hawana nyota ya ndoa

Muktasari:

  • Mhubiri Ezekiel Odero wa Kenya, ametoa mpya katika mahubiri yake yalikuwa mubashara katika moja ya luninga za nchi hiyo, pale aliposema kuwa baadhi ya wanamuziki wa Bongo Flava, huenda wakabaki kuwa watu wa kuwapa wanawake ujauzito bila kuwaoa.

Kenya. Mhubiri Ezekiel Odero wa Kenya, ametoa mpya katika mahubiri yake yalikuwa mubashara katika moja ya luninga za nchi hiyo, pale aliposema kuwa baadhi ya wanamuziki wa Bongo Flava, huenda wakabaki kuwa watu wa kuwapa wanawake ujauzito bila kuwaoa.

Mtandao wa gazeti la Taifa Leo, umebainisha kuwa mhubiri huyo, ameyasema hayo wakati akimwombea mwanaume ambaye alizungumzia jinsi alivyo na mazoea ya kuachana na wanawake wote anaokutana nao hasa baada ya kuwapachika mimba.

Wakati wa mahubiri yake, Mchungaji Ezekiel alitafakari changamoto zinazowakabili wale waliotelekezwa na waume au wake zao na kuachiwa majukumu ya kuwalea watoto.

Papo hapo akamrejelea msanii maarufu wa Bongo Flava bila kumtaja jina.

“Kuna wasanii maarufu wa Bongo ambao wana mazoea ya kuwapa ujauzito wanawake tofauti. Amezaa watoto kadhaa na wanawake tofauti,” mchungaji Ezekiel amesema

Mchungaji huyo alieleza kuwa safari ya maisha ya msanii huyo imemkuta akiwa amezaa watoto na wanawake tofauti na kisha kuwatelekeza.

“Alichukua mmoja kutoka Kenya na kumpachikika mimba kisha kumtupa. Roho ya kuoa hana. Hana roho ya ndoa,” akasema.