Museveni, Janet kusherehekea miaka 50 ya ndoa

Muktasari:
- Maandalizi yamepamba moto kuelekea sherehe za maadhimisho ya miaka 50 ya ndoa ya Rais Yowel Museveni na mke wake Janet Museveni, ambayo yanatarajia kufanyika Wilaya ya Ntungamo, nchini Uganda.
Uganda. Maandalizi yamepamba moto kuelekea sherehe za maadhimisho ya miaka 50 ya ndoa ya Rais Yowel Museveni na mkewe Janet, ambazo zinatarajia kufanyika Wilaya ya Ntungamo, nchini Uganda.
Wanandoa hao watafanya maombi ya kuadhimisha miaka 50 katika ndoa na baadaye kuwakaribisha wageni nyumbani kwao kijijini Irenga katika Parokia ya Kikoni siku ya Jumamosi.
“…Rais na Mama Janet Museveni na familia yao kwa furaha kubwa wanakualika katika ibada ya shukrani kwa heshima ya maadhimisho ya jubilee ya dhahabu, itakayofanyika Agosti 26 katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Mathayo Kyamate saa 10 alfajiri na baadaye, chakula cha mchana nyumbani kwao Irenga. , Ntungamo,” inasomeka sehemu ya kadi ya mwaliko.
Kadi za mialiko ambazo zilichapishwa kwa rangi tofauti, zinasambazwa kupitia kanisa kama ilivyothibitishwa na katibu wa Dayosisi ya Ankole Kusini, Mchungaji Can Arthur Twinamatsiko.
"Kanisa linasimamia kila kitu," amesema.
Mkuu wa Wilaya ya Ntungamo (RDC), Geofrey Mucunguzi na mwenyekiti wa Wilaya ya Ntungamo Samuel Rwakigoba, wamethibitisha kupokea mwaliko wa hafla hiyo.
“Tumepokea mialiko binafsi tukiwa viongozi wa wilaya; tunachosubiri ni siku ya tukio. Kama wakazi wa Ntungamo, tunajisikia heri kuwa familia namba moja inatoka katika eneo letu, ambao wamechagua kusherehekea pamoja nasi,” amesema Rwakigoba na kuongeza;
“Ndiyo, wamezaliwa hapa, lakini wangeweza kuchagua kufanya sherehe hiyo mahali popote na sehemu yeyote nchini, hivyo tuna furaha kubwa sana kwa wao kurudi nyumbani na kusherehekea pamoja nasi.”
Hata hivyo alipotafutwa, kiongozi wa Kanisa la Anglikana Uganda, Dayosisi ya Ankole Kusini, Askofu Nathan Ahimbisibwe, amesema hilo ni jambo binfsi la familia namba moja nchini.
“Hii ni hafla ya kibinafsi…Lakini ninafahamu itafanyika katika wilaya hii," amesema.
Hadi jana, mazingira yaluwekwa safi, huku majengo ya zamani yanapakwa rangi, na mahema kwa ajili ya wageni kujengwa.
Kulingana na kitabu cha Mama Janet Museveni kiitwacho safari ya maisha yangu (My life's journey), wanandoa hao walifunga ndoa katika kanisa dogo huko London, Uingereza na baadaye walifanya tafrija ndogo ya wanafamilia katika Hoteli ya Kensington Hilton jijini London mnamo Agosti 24, 1973.
Mama Janet ameeleza katika kitabu hicho kuwa ilikuwa ndoto yake kupanga harusi kubwa ya kanisani, nyumbani lakini hali za wakati huo hazikumruhusu. Kwani ni kipindi ambacho Idi Amin Dada alikuwa Rais wa Uganda na Waganda wengi walikuwa wamekimbilia uhamishoni.