Msemaji: Rais Ramaphosa hana mpango wa kung’atuka

Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa

Muktasari:

Licha ya kashfa ya wizi wa fedha inayomkabili Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, mkuu huyo wa nchi hana mpango wa kung’atuka katika nafasi hiyo.

Dar es Salaam. Licha ya kashfa ya wizi wa fedha inayomkabili Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, mkuu huyo wa nchi hana mpango wa kung’atuka katika nafasi hiyo.

  

Katika siku za hivi karibuni, ziliibuliwa tuhuma dhidi yake kwamba ameficha wizi wa fedha katika shamba lake la Phala Phala lililopo Kaskazini Mashariki mwa nchi hiyo.


Jopo la wataalamu lililoundwa kuchunguza tuhuma hizo, lilibainisha mkuu huyo wa nchi, alificha wizi wa Dola za Marekani 4 milioni (zaidi ya Sh8 bilioni) na kuhitimisha ana kesi ya kujibu mbele ya Bunge.


Kiongozi huyo aliyetwaa wadhifa wa urais kwa tiketi ya chama cha ANC, yupo katika tumbo joto na kwamba, hatma ya nafasi yake serikalini itatokana na kile kitakachoamuliwa na uongozi wa chama chake ulioanza kuketi leo na kesho kwa hatua zaidi.


Lakini, Msemaji wake, Vincent Magwenya amesema kiongozi huyo hatajiuzulu na atawania muhula mwingine wa urais kama mkuu wa ANC.


“Rais Ramaphosa hajiuzulu kutokana na ripoti mbovu, wala hatakaa pembeni,” amesema Vincent.


Hata hivyo, ameonyesha kupinga ripoti ya timu ya wataalamu iliyoundwa kuchunguza tuhuma hizo, akisema ina dosari.


Kashfa hiyo ilizuka Juni 2022, wakati mkuu wa zamani wa ujasusi wa Afrika Kusini, Arthur Fraser alipowasilisha malalamiko kwa polisi akimshutumu kuficha wizi huo mwaka 2020.


Ramaphosa alikiri fedha ziliibwa lakini ni Dola za Marekani 580,000 (zaidi ya Sh1.2 bilioni) na sio dola za Marekani 4 milioni kama inavyoelezwa.


Amesema fedha hizo zilitokana na mauzo ya nyati, lakini timu hiyo ya wataalamu iliyoongozwa na mwanasheria huyo ilishuku mauzo hayo kufanyika.


Tayari kamati hiyo imekabidhi matokeo ya uchunguzi wake kwa Bunge litakalochunguza kisha kuamua iwapo litaanzisha au kutoanzisha kesi ya kumuondoa madarakani Ramaphosa.


Shinikizo la kuondoka madarakani kwa mkuu huyo wa nchi, linasukumwa pia kutoka kwa wafuasi wanaomuunga mkono Rais wa zamani wa nchi hiyo, Jacob Zuma ambaye pia anatokana na ANC.


Hii inatokana na kile alichokiapa Ramaphosa wakati anaingia madarakani kwamba, ataumaliza ufisadi wote uliokuwepo nchini humo wakati wa mtangulizi wake, Zuma.


Bado chama hicho kwa sasa kimegawanyika katika makundi mawili, kati ya wanaomuunga mkono Ramaphosa na wale wa Zuma.