Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Idadi ya vifo tetemeko Venezuela yaongezeka, Papa Leo asema…

Baadhi ya mjengo yaliyoharibiwa kutokana na matetemeko ya ardhi yaliyolikumba eneo la La Guaira, Venezuela.

Muktasari:

  • Idadi ya waliokufa kutokana na tetemeko la ardhi nchini Venezuela imefikia 1,450 huku waokoaji wakiendelea kusaka manusura, Serikali ikitangaza hali ya dharura na maelfu wakibaki bila makazi.

Dar es Salaam. Idadi ya watu waliopoteza maisha kutokana na matetemeko mawili makubwa ya ardhi yaliyoikumba Venezuela mapema wiki iliyopita imeongezeka na kufikia 1,450, ongezeko la vifo 20 ndani ya saa 24 baada ya vifo 1,430 kuripotiwa jana.

Vifo hivyo vimeripotiwa huku juhudi za uokoaji zikiendelea katika maeneo yaliyoharibiwa hususan jimbo la La Guaira, ambako mamia ya majengo yameporomoka na maelfu ya wananchi kuachwa bila makazi.

Kwa mujibu wa Idhaa ya Kiswahili ya DW, vikosi vya uokoaji Venezuela na mataifa mbalimbali vinaendelea kuchimba vifusi kwa kutumia mitambo maalumu na mbwa waliofunzwa kutafuta manusura, huku matumaini ya kuwapata walio hai yakizidi kupungua kadiri muda unavyosonga tangu matetemeko hayo yatokee.

Reuters imeripoti Rais wa mpito wa Venezuela, Delcy Rodríguez amethibitisha idadi hiyo ya vifo na kusema watu 3,150 wamejeruhiwa huku wengine 12,721 wakilazimika kuyahama makazi yao kutokana na uharibifu mkubwa wa miundombinu.

Aidha, majengo 774 yameripotiwa kuporomoka kabisa na mamia mengine kuwa katika hatari ya kuanguka, ambapo Rodríguez ameangaza hali ya dharura ya kitaifa na kusema Serikali itaelekeza nguvu zote katika kuokoa maisha ya wananchi na kuwahudumia waathirika.

Ametoa pia wito kwa madaktari, wauguzi na watumishi wa afya kuripoti mara moja kwenye vituo vyao ili kuongeza nguvu katika kuwahudumia majeruhi, akisema serikali inasisitiza kuhakikisha kuwa walionaswa chini ya vifusi wanaokolewa na waathirika wanapata huduma zote muhimu.


Chanzo cha tetemeko

Kwa mujibu wa U.S. Geological Survey (USGS), matetemeko hayo yenye ukubwa wa takribani 7.2 na 7.5 yalitokana na kusogea ghafla kwa mabamba ya tektoniki katika ukanda wa kaskazini mwa Venezuela.

Wataalamu wa taasisi hiyo wanasema nguvu kubwa iliyotokea chini ya ardhi ilisababisha mtikisiko mkali ulioangusha majengo mengi, kuharibu barabara, madaraja, hospitali, shule na miundombinu mingine muhimu.

Mbali na maelfu ya waliopoteza makazi, mashirika ya misaada yanasema maelfu ya wananchi wanahitaji chakula, maji safi, dawa na malazi ya muda. Wachambuzi pia wanaonya kuwa janga hilo linaweza kuongeza shinikizo kwa uchumi wa Venezuela ambao tayari ulikuwa ukikabiliwa na changamoto za kisiasa na kiuchumi.


Papa Leo awaombea waathiriwa

Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Leo XIV amewaombea waathiriwa wa matetemeko hayo, akieleza mshikamano wake na familia zilizopoteza wapendwa wao na maelfu ya wananchi walioathirika. Pia amezipongeza timu za uokoaji na wote wanaoendelea kutoa misaada kwa manusura.

Papa alitoa ujumbe huo mjini Roma, Jumapili Juni 28, 2026, kabla ya sala ya Angelus, wakati idadi ya vifo ikizidi kuongezeka huku ikiripotiwa kuwa zaidi ya watu 50,000  hawajulikani walipo na maelfu kupoteza makazi yao.

Aidha, mataifa mbalimbali yameanza kutoa misaada ya kibinadamu ikiwemo Umoja wa Ulaya (EU) ambao umetenga zaidi ya Sh15 bilioni kusaidia operesheni za uokoaji na kuwahudumia waathirika.

Tetemeko hilo linaorodheshwa miongoni mwa majanga makubwa ya karne hii duniani, likikumbusha tetemeko la Haiti mwaka 2010, lililosababisha vifo vya mamia ya maelfu ya watu, tetemeko la Japan mwaka 2011 lililoambatana na tsunami na ajali ya nyuklia ya Fukushima, pamoja na matetemeko ya Turkiye na Syria mwaka 2023 yaliyosababisha zaidi ya watu 59,000 kupoteza maisha na uharibifu mkubwa wa mali na miundombinu.