Hamas: Msaada wa Marekani kwa Israel ni sawa na uchokozi kwa Palestina

Muktasari:
- "Tangazo la Marekani la msaada wa ziada wa kijeshi kwa Israel ni ushiriki wa kweli katika uchokozi dhidi ya raia wetu”.
Gaza. Kufuatia tangazo la Marekani kutuma msaada wa kijeshi kwa Israel, Kundi la wanamgambo la Hamas la Palestina limesema kitendo hicho ni sawa na uchokozi dhidi ya nchi yao.
"Tangazo la Marekani la msaada wa ziada wa kijeshi kwa Israel ni ushiriki wa kweli katika uchokozi dhidi ya raia wetu," imesema taarifa ya Hamas na kuongeza…
"Vitendo hivi haviwatishi watu wetu wala harakati ambazo zitaendelea kuwatetea," Hamas imeongeza katika taarifa yake.
Gazeti la New York Times limeandika kwamba Marekani inajitahidi kutimiza maombi kadhaa maalumu kutoka kwa Israel ya usaidizi wa kijeshi kufuatia shambulio la Hamas, alinukuliwa Waziri wa Mambo ya Nje, Antony Blinken.
Blinken alisema kuwa serikali ya Israel imeomba msaada maalumu wakati nchi hiyo inajiandaa kwa kile Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu ameonya kuwa huenda ukawa mzozo wa muda mrefu.
Wakati huo maofisa wa Ikulu ya Marekani walisema Rais Biden alimwambia Netanyahu jana Jumapili Oktoba 8, 2023 kwamba usaidizi wa kijeshi uko njiani kuelekea Israel na mwingine zaidi utafuata katika siku zijazo.
Usaidizi huo ni meli nyingi za kijeshi na ndege ikiwa kama ishara ya uungaji mkono kufuatia shambulio la kushtukiza la Jumamosi lililofanywa na kundi la wapiganaji la Palestina Hamas ambalo limezua mapigano yaliyosababisha maelfu kuuawa hadi sasa.
Imeandaliwa kwa msaada wa mtandao