Wafanyabiashara walalamikia ubovu wa masoko

Muktasari:
Mfanyabiashara wa Soko la Ikuti, Atupele Sanga alisema wanahitaji ukarabati wa majengo yote na kupiga mabati mapya.
Mbeya. Wafanyabiashara katika masoko ya Matola, Mabatini na Ikuti jijini hapa, wameitaka halmashauri kuboresha miundombinu ya majengo na mifereji ya maji ili kuwawezesha kufanya biashara zao katika mazingira safi na salama.
Mfanyabiashara wa Soko la Ikuti, Atupele Sanga alisema wanahitaji ukarabati wa majengo yote na kupiga mabati mapya.
Sanga alisema soko halina mifereji ya maji machafu jambo linalosababisha maji hayo kuzagaa eneo lote.
Mamalishe Jane Stephano alisema Soko la Mabatini lina miaka zaidi ya 50 na halijawahi kukarabatiwa.
Alisema pamoja na jitihada za kufanya usafi maeneo ya chakula na kulipa ushuru kila siku , lakini mazingira na miundombinu ya soko hilo yamekuwa kero kubwa.
Mfanyabiashara wa Jarome Mussa wa Soko Matola, alishauri halmashauri kutumia wataalamu wake kufanya tathimini ya kukarabati upya masoko yote yaliyochakaa.
Mstahiki Meya wa Jiji la Mbeya, David Mwashilindi alikiri kuwapo kwa changamoto hizo na kwamba tatizo lililopo halmashauri haina vyanzo vya mapato.