Wafanyabiashara wadogo wawezeshwe kukuza utalii

Muktasari:

Inaelezwa kuwa Ili kuwa na maboresho tunayoyakusudia pamoja na utalii endelevu, ni muhimu kuwawezesha na kuwashirikisha wananchi kuanzia ngazi ya chini kabisa pamoja na wafanyabiashara wadogo na wa kati.

Dar es Salaam. Wakati sekta ya utalii ikitarajiwa kufufuka na kurudi kama ilivyokuwa kabla ya kuibuka kwa janga la Uviko-19, Shirika la Utalii la Umoja wa Mataifa (UNWTO) limeitaka dunia kuwashirikisha wafanyabiashara wadogo na wa kati kuleta maboresho yatakayoongeza tija.

 UNWTO imetoa hamasa hiyo kwenye mkutano wa mataifa 20 yaliyoendelea zaidi kwa viwanda (G20), uliofanyika wiki iliyopita jijini Bali nchini Indonesia.

Katibu Mkuu wa UNWTO, Zurab Pololikashvili alisema kuanzia mtu mmojammoja mpaka biashara ndogo zinapaswa kushirikishwa kwenye mikakati ya kukuza utalii, sekta inayopitia changamoto nyingi zaidi kurudi kwenye hali yake tangu kuibuka janga hilo, lililoisumbua dunia kwa takriban miaka minne sasa.

Pololikashvili alisema biashara ndogo na jamii kwa ujumla zina mchango mkubwa wa kuirudisha biashara ya utalii zaidi ya viwango vilivyokuwapo kabla ya kuibuka kwa Uviko-19, hivyo mikakati ya kuzishirikisha inahitajika ili kufanikisha malengo hayo.

“Kinachotakiwa ni kuwapa ushirikino wanaouhitaji ili kuwa mawakala halisi wa mabadiliko. Ili kuwa na maboresho tunayoyakusudia pamoja na utalii endelevu, muhimu kuwawezesha na kuwashirikisha wananchi kuanzia ngazi ya chini kabisa pamoja na wafanyabiashara wadogo na wa kati,” alisema Pololikashvili.

Katibu mkuu huyo alisema hayo akiujulisha ulimwengu athari zilizoletwa na Uviko-19 kwenye sekta hiyo, bila kusahau changamoto nyingine zinazoendelea kujitokeza ambazo zinaweza kugeuzwa kuwa fursa iwapo kutakuwa na ushirikishaji wa kila mdau wa utalii.

Kati ya changamoto ambazo Pololikashvili anaamini zinaweza kudhibitiwa kwa ushirikishaji ni migogoro kati ya mataifa yanayolumbana, kupanda kwa bei ya mafuta katika soko la dunia na mabadiliko ya tabianchi yanayochangiwa kwa kiasi kikubwa na shughuli za binadamu.

“Ni muhimu kwa mataifa yote kuweka mikakati ya kuwashirikisha wananchi pamoja na wajasiriamali wadogo, tukianza na nchi wanachama wa G20 ambao ushawishi wao ni mkubwa,” alisema Pololikashvili.

Umuhimu wa G20 unatokana na ukweli kwamba mataifa hayo ndiyo yanayounda asilimia 80 ya pato la dunia nzima, huku yakiwa na zaidi ya nusu ya raia wote wa ulimwengu huu. Kwenye sekta ya utalii mataifa hayo 20 yanachangia asilimia 76 ya mapato yote kwa mwaka.

UNWTO inaamini utawala bora wenye mikakati mipya, ushirikiano na diplomasia ya kimataifa ni njia sahihi zitakazosaidia kutatua changamoto zilizojitokeza baada ya janga la Uviko-19, na wanachama wa G20 wana nafasi kubwa ya kuongeza ushawishi wa kutafuta suluhu ya kudumu.

Katika juhudi za kuhakikisha sekta ya utalii inaimarika na mchango wake kuongezeka zaidi kwenye uchumi, ndani ya mwaka huu pekee kikosi kazi kilichoundwa na UNWTO kikiongozwa na Rais wa Indonesia, Joko Widodo na kuratibiwa na Waziri wake wa Utalii na Ubunifu, Sandiaga Uno, kimetoa mwongozo utakaorahisisha ushirikishaji wa jamii na wajasiriamali wadogo kuleta mabadiliko ya kuiboresha sekta ya utalii.

Mwongozo huo uliotolewa Septemba kwenye mkutano wa mawaziri wa utalii kutoka kote duniani, umeelekeza maeneo matano ya kuwekewa msisitizo ili kufanikisha malengo yaliyopo.

Kwanza, mwongozo huo unasisitiza kuwekeza kwa watu kwa kuwajengea maarifa, kisha kuwaruhusu washauri maboresho wanayoona yanafaa kwenye mazingira yao.

Kingine ni ubunifu na matumizi ya majukwaa na fursa za kidijitali kukuza utalii, ushiriki na uwezeshaji wa wanawake na vijana. Eneo la nne ni utunzaji wa mazingira na bayoanuwai na mwisho ni kuongeza uwekezaji na kuimarisha sera na utawala.

“Ongezeni kasi ya mabadiliko na maboresho. Tuko nyuma kuelekea utekelezaji wa Malengo Endelevu ya Maendeleo. Kiuhalisia utekelezaji umehuishwa katika baadhi ya maeneo, mfano usawa wa kijinsia. Utalii unayo nafasi kubwa ya kuturudisha kwenye njia sahihi itakayotuwezesha kuendelea na kasi inayotakiwa, ila ni lazima tuongeze kasi ya ushirikishaji na uwekezaji, kwani hakuna muda wa kupoteza tena,” alisema Pololikashvili.

Mwongozo wa UNWTO umewatanguliza watu katika utekelezaji wa mikakati yote, hasa kipindi hiki ambacho kila Taifa linaboresha mazingira yake ili kuwakaribisha na kuwapokea wageni wengi zaidi watakaosaidia kuimarisha mapato, hivyo kukuza uchumi na kipato cha wananchi.

Takwimu za shirika hilo zinaonyesha idadi ya watalii wa kimataifa imefika asilimia 70 ya kiasi kilichokuwapo kabla ya mwaka 2019, janga la Uviko lilipoibuka na kulazimu masharti kadhaa kuwekwa ili kudhibiti kuenea kwa virusi vyake, ikiwamo kufunga usafiri na kuzuia mikusanyiko ya watu.

Athari za masharti hayo hazikuiacha salama Tanzania, hasa kampuni ndogo za kuongoza watalii, upagazi, hoteli na kila mdau anayejihusisha na utalii kwa namna moja au nyingine.

Kutokana na janga hilo, baadhi ya hoteli zilifungwa, kampuni zilikufa na maelfu ya wafanyakazi kupoteza ajira zao, huku wafanyabiashara wakikabiliwa na madeni makubwa kiasi cha kushindwa kutekeleza mipango yao.

Hata hivyo, juhudi za makusudi zimeendelea kuchukuliwa, huku Serikali ikisisitiza mpango wake wa kuongeza idadi ya wageni wanaoingia nchini kutoka watalii milioni 1.5 walioingia mwaka 2015 mpaka milioni tano mwaka 2025.

Uzinduzi wa filamu ya The Royal Tour iliyoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ni kati ya mikakati ya kuwavutia watalii wengi kutoka kote duniani, lakini ushiriki wa wananchi, hasa wajasiriamali kunasisitizwa zaidi ili kuyafikia malengo hayo kwani mawazo na ubunifu wao utakuwa na mchango mkubwa.

Hiki ni kipindi ambacho Serikali inapaswa kushirikiana na wadau wote wa utalii kuanzia vyama vya watoa huduma wa sekta hiyo, mpaka wananchi wanaozunguka vivutio vilivyopo, watafiti na wengine muhimu ili kuwa na msukumo utakaokuwa na tija kubwa zaidi.