Wadau: Ushuru mpya wa Trump, uiamshe Tanzania

Muktasari:
- Ushauri kutoka kwa mchumi Lipumba, Profesa Anna Tibaijuka, na January Makamba kwa wataalamu wa maendeleo na uchumi kwa Serikali kuhusu mikakati ya kukabiliana na viwango vipya vya ushuru wa forodha vilivyotangazwa na Rais wa Marekani, Donald Trump.
Dar es Salaam. Kuimarisha diplomasia ya kiuchumi na kushirikiana na mataifa yaliyo tayari, kama vile China ni miongoni mwa ushauri uliotolewa na wataalamu wa uchumi nchini Tanzania.
Ushauri huo ulitolewa kwa nyakati tofauti na maprofesa wa uchumi, Ibrahim Lipumba na Anna Tibaijuka, pamoja na Mbunge wa Bumbuli na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba.
Wataalamu hao wamependekeza hatua hizi kwa Serikali kama njia ya kukabiliana na viwango vipya vya ushuru wa forodha vilivyowekwa na Rais wa Marekani, Donald Trump.
Rais Trump mwishoni mwa wiki alitangaza hali ya dharura ya kiuchumi na kuweka viwango vipya vya ushuru wa forodha, ambapo bidhaa kutoka Tanzania zitatozwa asilimia 10, ikilinganishwa na asilimia 54 inayotozwa kwa bidhaa kutoka China.
Hayo yanajiri wakati Sheria ya Ukuaji na Fursa Afrika (AGOA), ambayo imezipa nchi nyingi za Afrika upendeleo katika soko la Marekani, inatarajiwa kumalizika Septemba 2025.
Akizungumza na vyombo vya habari ofisini kwake leo Jumapili Aprili 6, 2025, Profesa Lipumba, ambaye aliwahi kuwa mshauri wa Rais wa awamu ya pili, hayati Ali Hassan Mwinyi katika masuala ya uchumi, anasema ni muhimu kuwekwa mikakati madhubuti, ikiwemo kuimarisha diplomasia ya kiuchumi na kushirikiana na mataifa yaliyo tayari, kama vile China na baadhi ya nchi za Ulaya.
“Pia, nashauri kukaribisha uwekezaji katika viwanda na kununua madini ya dhahabu. Tukifanya hivyo, hasa katika nyakati hizi ambapo uchumi wa mataifa mengi unayumba, tunaweza kupata msaada mkubwa," anasema Profesa Lipumba, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF).
Profesa Lipumba ambaye amewahi kufanya kazi na Profesa Hernando de Soto, mchumi maarufu wa Peru, amesisitiza kuwa vivutio vya uwekezaji katika viwanda vitakuwa na manufaa, kwani watu kutoka mataifa kama China, wanaotaka kuuza bidhaa zao Marekani na sehemu nyinginezo, watatamani kuanzisha viwanda nchini ili kutumia fursa ya ushuru mdogo.
“Sababu kuu ya mataifa kutoka nje kukimbilia kwetu kujenga viwanda ni ushuru wetu wa forodha kuingia Marekani ni mdogo, na kwa kuwa tunauza bidhaa kidogo, hii itakuwa chachu pia ya kuongeza ajira kwa vijana wetu ambao wanalia kwa ukosefu wa fursa,” anasema Profesa Lipumba ambaye amewahi kufanya kazi na baadhi ya wachumi maarufu duniani, wakiwemo Profesa Joseph Stiglitz aliyekuwa mshauri wa uchumi wa Rais Bill Clinton na baadaye mchumi wa Benki ya Dunia.
Anasema sera za Marekani zimechangia kuporomoka kwa bei ya hisa duniani kote tangu kutangazwa kwa viwango vya forodha kwa mataifa yote.
Anaongeza kuwa wachumi wanatabiri kutakuwa na anguko kubwa la uchumi duniani.
“Bidhaa nyingi tunazouza nje zinaweza kuporomoka bei, isipokuwa dhahabu, ambayo inatarajiwa kuongezeka. Hii ni kwa sababu wakati wa matatizo katika soko la mitaji, watu wenye akiba zao wanakimbilia kununua dhahabu ili kulinda utajiri wao,” anasema.
Profesa mwingine wa uchumi na Waziri wa zamani wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Anna Tibaijuka, alielezea wasiwasi wake kuhusu kuongezeka kwa mvutano wa kibiashara kupitia jukwaa lake la X na kupendekeza kuwa Afrika inahitaji jibu la kimkakati na la umoja kuhusu ushuru wa Marekani.
Profesa Tibaijuka ambaye amewahi kuwa Mshauri wa Tume ya Dunia ya Kuwawezesha Maskini Kisheria alionya kuwa mmomonyoko wa faida za AGOA na kupungua kwa biashara ya kikanda kunaweza kudhuru mataifa maskini ambayo hayana uwezo wa kulipiza kisasi.
"Ni muhimu kuitisha mkutano wa dharura wa biashara wa AU kushughulikia masuala haya na kulinda masilahi ya kiuchumi ya Afrika," aliandika Profesa Tibaijuka ambaye amewahi kuwa Katibu Mkuu Mwandamizi wa Umoja wa Mataifa na Mkurugenzi Mtendaji Shirika la Makazi Duniani (UN-HABITAT).
Kwa upande wake, Mbunge wa Bumbuli na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba, alitoa maoni yake kupitia jukwaa lake la X kuhusu sera ya ushuru ya Marekani.
Aliandika kuwa ingawa soko la Marekani ni kubwa, athari za ushuru huo kwa Afrika zinaweza kuwa ndogo.
Makamba alibainisha kuwa mwaka uliopita, Marekani iliagiza bidhaa zenye thamani ya dola bilioni 40 kutoka Afrika, sawa na uagizaji wa mwezi mmoja kutoka Mexico.
Aliongeza kuwa AGOA, katika kilele chake, ilichangia takriban asilimia 15 tu ya biashara ya Marekani na Afrika, na hivyo kufanya mchango wake kuwa mdogo kuliko wengi wanavyofikiri.
Makamba alisisitiza umuhimu wa kuimarisha biashara ya ndani ya Afrika, ambayo kwa sasa inachangia asilimia 15 tu ya biashara nzima ya bara hilo. "Biashara ya ndani ya kanda ya Ulaya ni asilimia 60 na Asia ni asilimia 50.” Alifafanua kuwa ikiwa Afrika itaongeza biashara yake ya ndani kufikia kiwango cha Asia ifikapo mwaka 2040, Pato la Taifa linaweza kutengeneza mamilioni ya kazi na kupunguza umaskini kwa kiwango kikubwa.