Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tanzania yajipanga kunufaika na gesi trilioni 57.54

Mitambo mbalimbali katika eneo la kiwanda cha kuchakata gesi asilia cha Mnazi Bay, mkoani Mtwara.

Muktasari:

  • Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli Nchini (PURA) imesema Tanzania imegundua futi za ujazo trilioni 57.54 za gesi asilia katika maeneo mbalimbali nchini, huku asilimia 35 ya gesi hiyo ikitumika kuzalisha umeme unaotumika nchini.

Mtwara. Tanzania imeingia katika hatua mpya ya maendeleo ya sekta ya gesi asilia kufuatia kuthibitishwa kwa uwepo wa akiba kubwa inayokadiriwa kufikia futi za ujazo trilioni 57.54, hatua inayotarajiwa kubadilisha mwelekeo wa uchumi wa Taifa.

Ugunduzi wa rasilimali hiyo unaifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zenye fursa kubwa zaidi za uwekezaji katika nishati barani Afrika.

Hayo yameelezwa leo, Ijumaa Juni 12, 2026, wakati Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) pamoja na kamati zake walipotembelea miradi ya gesi asilia katika eneo la Mnazi Bay, mkoani Mtwara kwa lengo la kujifunza na kujionea maendeleo ya shughuli za utafutaji, uzalishaji na uchakataji wa gesi asilia.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa PURA, Charles Sangweni amesema gesi hiyo hutumika kwa takribani asilimia 35 kwa ajili ya kuzalisha umeme unaotumika hapa nchini.

Ameeleza kuwa maeneo yote yaliyogunduliwa kuwa na gesi asilia yanaendelea kufanyiwa kazi ili rasilimali hiyo iweze kuzalishwa na kutumika kwa manufaa ya Taifa.

“Sasa tukaona ni vyema kuongeza idadi ya visima ili kuongeza uzalishaji wa gesi asilia. Gesi nyingi huzalishwa na kupelekwa katika mitambo ya Madimba inayomilikiwa na TPDC, ambako hutumika kuzalisha umeme,” amesema Sangweni.

Mitambo mbalimbali katika eneo la kiwanda cha kuchakata gesi asilia cha Mnazi Bay, mkoani Mtwara.

Kwa upande wake, Mhandisi Mwandamizi wa Petroli wa PURA, Fabian Mwose, ameeleza hatua za awali za utafutaji wa gesi asilia katika visima vitatu vipya vilivyopo eneo la Mnazi Bay.

Amesema kisima cha Kasa, ambacho ni cha tatu katika kampeni ya uchimbaji wa visima vitatu vya gesi asilia, kilianza kutobolewa Juni 1, 2026, na kinatarajiwa kuchukua takribani siku 55 kukamilika.

Mwose amesema baada ya uchimbaji kukamilika, tathmini na maandalizi ya uzalishaji yatafanyika endapo uwepo wa gesi asilia utathibitishwa katika kisima hicho.

“Kwa mujibu wa tafiti za awali zilizofanyika, kisima hicho kinakadiriwa kuwa na takribani futi za ujazo bilioni 167 za gesi asilia, ambazo zinaweza kuzalishwa kwa wastani wa futi za ujazo milioni 35 kwa siku,” amesema Mwose.

Ameongeza kuwa uzalishaji wa gesi kutoka katika kisima hicho utaongeza kiwango cha gesi asilia kinachozalishwa nchini, jambo litakalosaidia kukidhi mahitaji ya nishati katika sekta mbalimbali, hususan viwandani.

Amesema hatua hiyo pia itachochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi na kuongeza fursa za ajira kwa Watanzania kupitia maendeleo ya viwanda vinavyotegemea gesi asilia.

Mwenyekiti wa Bodi ya PURA, Halfani Halfani, amesema ziara hiyo imewapa fursa ya kuelewa kwa undani mchakato wa utafutaji, uchimbaji na uzalishaji wa gesi asilia nchini.

Ameongeza kuwa wananchi, hususan wa Mkoa wa Mtwara, wanaendelea kunufaika na uwekezaji katika sekta hiyo kupitia ongezeko la shughuli za kiuchumi, mzunguko wa fedha pamoja na maendeleo ya miundombinu kama barabara na huduma nyingine za kijamii.

Katika ziara hiyo, wajumbe walitembelea kisima cha utafutaji wa gesi asilia cha Kasa kilichopo Mnazi Bay pamoja na Kiwanda cha Kuchakata Gesi Asilia cha Madimba.