Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Stanbic yaja na mikakati ya kuinua sekta ya kilimo, kuwezesha wakulima

Picha na Mtandao.

Dar es Salaam. Wataalamu wa fedha na kilimo wamesema changamoto inayowakabili wakulima nchini si wingi wa mavuno, bali ni ukosefu wa mpango thabiti wa kibiashara unaounganisha uzalishaji na masoko.

Kwa mujibu wa wataalamu hao, kilimo kitaendelea kuwa nguzo muhimu ya uchumi wa Tanzania, lakini tija yake halisi itaonekana pale uzalishaji utakapounganishwa na masoko imara, uwezeshaji sahihi, na mfumo unaoongeza thamani ya mazao.

Hayo yalielezwa jana, na Mkuu wa Kilimo Biashara wa Stanbic Bank Tanzania, Benifrida Tarimo, wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari.

Alisema changamoto si wingi wa mavuno, bali ni namna mazao yanavyotoka shambani hadi kufika sokoni bila mpango thabiti wa kibiashara.

Alisisitiza kuwa ni muhimu kubadili mtazamo, ili kilimo kisiwe tu shughuli ya kuzalisha mazao, bali biashara kamili yenye mnyororo wa thamani uliopangwa vizuri. Benifrida alisema ili kilimo kiongeze kipato halisi, ni lazima kuangalia zaidi ya uzalishaji.

“Thamani inatengenezwa katika kila hatua, siyo shambani pekee. Kilimo cha kisasa kinapaswa kuanza na soko akilini, kuanzia shambani hadi kwa mlaji,” alisema. Alieleza kuwa wakulima wengi wamekuwa wakikwama kwenye mzunguko wa kuzalisha na kuuza mazao yao haraka baada ya kuvuna kwa bei ya chini.

“Hali hii inachangiwa na ukosefu wa maghala ya kuhifadhi mazao, jambo linalowalazimu kuuza mara moja badala ya kusubiri bei ipande,” alisema.

Aidha, alisema ukosefu wa taarifa sahihi za soko unawanyima wakulima na wanunuzi uwezo wa kupanga bei, huku shinikizo la kupata fedha za haraka likiwafanya wakubali bei ndogo na hivyo kupoteza thamani ya mazao yao.

Benifrida alisema kwa miaka mingi nguvu kubwa imewekwa kwenye kuongeza uzalishaji, lakini kuongezeka kwa mavuno hakujaakisi kuongezeka kwa kipato kwa mkulima.

“Pengo lipo nje ya shamba. Kilimo hakiishii kwenye kupanda na kuvuna. Thamani huongezeka au kupotea katika hatua za uhifadhi, ukusanyaji, usindikaji na usafirishaji,” alisema.

Alisema mnyororo huo ukivunjika, hata kama uzalishaji ni mkubwa, matokeo hubaki kuwa hafifu kwa mkulima.

Alitaja umuhimu wa vyama vya ushirika (AMCOS) na vikundi vya wakulima, mfumo unaowapa nguvu ya majadiliano ya bei, uhakika wa soko kutokana na kuvutia wanunuzi wakubwa, na urahisi wa kupata mikopo kutoka taasisi za kifedha.

Mtaalamu mwingine wa Stanbic Bank Tanzania, Amal Baziad, alisema changamoto si tu upatikanaji wa fedha, bali ni namna zinavyotolewa kulingana na uhalisia wa msimu wa kilimo.

“Ni muhimu kuelewa mzunguko wa bei na mahitaji ya kila mdau katika mnyororo wa thamani,” alisema.

Aliongeza kuwa kuna haja ya kwenda zaidi ya mikopo ya kawaida kwa kuzingatia mkulima, mkusanyaji, msambazaji na msindikaji, ili kuhakikisha kila hatua inawezeshwa ipasavyo.