Prime
Safari ya miaka 30 sekta ya vileo inavyoakisi ndoto za Rais Mkapa
Dar es Salaam. Miaka 30 ya uanzishwaji wa sekta binafsi, ubinafsishaji na taasisi za umma nyingi nchini tangu uongozi wa awamu ya tatu wa Benjamin Mkapa imetimia.
Sekta ya vileo na masoko ya mitaji ilizoanzishwa mapema mwaka 1996, imetimiza miaka 30 ya huduma, ikiandika safari ya mafanikio, ukuaji wa mfululizo wa soko nchini na kuendelea kuwa sehemu muhimu ya mageuzi ya uchumi.
Pia inaonesha kwa vitendo namna viwanda, kilimo hasa cha shayiri ambacho ni malighafi muhimu kwa uzalishaji wa bia na masoko ya mitaji vinavyounganishwa katika mfumo mmoja wa uzalishaji unaogusa maisha ya wananchi na kuchangia katika pato la Taifa.
Katika kipindi cha miaka 30 ya maendeleo ya masoko ya fedha nchini, sekta hii imekuwa mfano hai wa mabadiliko ya uchumi unaotegemea uwekezaji wa muda mrefu, uimarishaji wa viwanda na ushiriki wa wananchi katika umiliki wa mashirika makubwa kupitia masoko ya hisa.
Katika mfumo huo, Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) imeendelea kushikilia nafasi ya uongozi wa sekta ya bia na vileo nchini si tu kama mzalishaji mkuu bali pia kama mshiriki muhimu katika mfumo wa masoko ya mitaji kupitia Soko la Hisa la Dar es Salaam.
TBL
Uhusiano huu umeifanya sekta ya bia kuwa sehemu ya mzunguko mpana wa kiuchumi unaounganisha mitaji ya wananchi, uzalishaji wa viwanda na mapato ya Serikali.
Katika robo ya kwanza ya mwaka 2026, kampuni hiyo ilirekodi ongezeko la mapato lililofikia Sh89 bilioni ikiwa ni ukuaji wa asilimia 15 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka uliopita.
Ukuaji huo uliambatana na ongezeko la faida ya uendeshaji kwa asilimia 23, hali inayoonyesha uimara wa shughuli za msingi za uzalishaji na usambazaji.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Fedha wa kampuni hiyo, Avito Swai mafanikio hayo yalitokana na ufanisi wa uzalishaji, ubunifu wa bidhaa na matumizi ya mifumo ya kidijitali katika usambazaji wa bidhaa sokoni, ingawa mazingira ya robo ya pili ya mwaka yalianza kuathiriwa na kupanda kwa gharama za mafuta na usafirishaji.
Sekta ya bia nchini Tanzania imeendelea kuwa moja ya sekta zenye ushindani mkubwa na mchango mkubwa katika uchumi wa taifa.
Kampuni mbalimbali zinashindana kupitia ubora wa bidhaa, nguvu ya chapa, bei na mikakati ya usambazaji lakini TBL imeendelea kushikilia nafasi ya juu kupitia chapa zake zinazotambulika ndani na nje ya nchi, ikiwamo matumizi ya lugha ya Kishwahili ambayo yanatajwa kuongeza ushiriki wa wanahisa.
Ushindani huu umeifanya sekta ya bia kuwa si tu eneo la biashara, bali pia uwanja wa mageuzi ya kiteknolojia na kiuchumi unaoathiri moja kwa moja tabia ya matumizi ya wananchi.
Safari ya milima na mabonde
Safari ya sekta ya bia na masoko ya mitaji nchini Tanzania imekuwa ya kupanda na kushuka lakini yenye mwelekeo wa jumla wa ukuaji endelevu.
Katika upande mmoja, sekta hii imeonyesha mafanikio makubwa katika ongezeko la mapato, upanuzi wa uzalishaji na kuimarika kwa mchango kwa Serikali.
Kwa upande mwingine, imekumbana na changamoto za mabadiliko ya gharama za uzalishaji, ushindani mkali wa soko na mabadiliko ya tabia ya walaji.
Mwenyekiti wa Bodi ya TBL, Balozi Ami Mpungwe anaeleza kuwa uthabiti wa kampuni umetokana na uwekezaji wa muda mrefu katika malighafi za ndani hasa shayiri pamoja na kuimarishwa kwa miundombinu ya uzalishaji ikiwamo Kiwanda cha Kimea cha Kilimanjaro chenye uwezo wa kuzalisha tani 8,000 kwa mwaka.
Anasema hatua hiyo imeiwezesha kampuni kupunguza utegemezi wa uagizaji na wakati huo huo kuongeza ushiriki wa wakulima wa ndani katika mnyororo wa thamani.
Kwa upande wa wachambuzi wa uchumi wanasema sekta ya bia imekuwa kipimo cha moja kwa moja cha mabadiliko ya matumizi ya ndani, ambapo ukuaji wa mapato na mauzo huakisi hali ya kipato na mzunguko wa fedha katika jamii.
Mtaalamu wa masuala ya uchumi Profesa Wetengere Kitojo, anasema kwa kampuni au shirika kuweza kusimama lazima liwe na misingi imara ya kutekeleza ili kufikia mataraji yake. Anafafanua kuwa Mashirika ya Serikali au binafsi yanahitaji kuwekeza katika utendaji wa kiufanisi kuanzia wafanyakazi wake, teknolojia na malengo yake.
“Mashirika ya umma yamekuwa yakiendeshwa kwa kulindwa badala ya kushindana, pia biashara yake inakuwa ya kusuasua kutokana na kuendeshwa na fedha za umma, hivyo kukosa udhibiti imara kwa kuwa hakuna mtu anayepata hasara moja kwa moja na kusuasua kwake,” anasema
Anaongeza kuwa kampuni binafsi, zinakua kwasababu zina ushindani, kutokana na usimamizi imara kufikia malengo yake na yanaendeshwa kibiashara, watu wanakuwa na malengo ya kuzalisha faida.
Mafanikio na changamoto
Katika kipindi cha miaka mitano, TBL imeonyesha mwelekeo wa ukuaji thabiti wa mapato ulioanzia takribani Sh1.13 trilioni mwaka 2022 hadi kufikia zaidi ya Sh1.65 trilioni mwaka 2025.
Ukuaji huu wa karibu asilimia 15 kwa mwaka unaonesha uimara wa sekta ya bia licha ya mabadiliko ya kiuchumi na ushindani wa soko.
Katika kipindi hicho, kampuni imechangia zaidi ya Sh3.2 trilioni kwa Serikali kupitia kodi, hatua inayoifanya kuwa moja ya wachangiaji wakubwa wa mapato ya taifa.
Mchango huu umeongezeka kila mwaka kwa kasi thabiti, ukiakisi kuimarika kwa shughuli za uzalishaji na mauzo.
Ongezeko hilo la kodi linaonyesha sio tu ukuaji wa biashara bali pia uimara wa mifumo ya usimamizi wa kodi na uwazi wa kampuni zilizo kwenye soko la hisa.
Kwa upande wake, uongozi wa TBL unasisitiza kuwa mafanikio haya yanatokana na uwekezaji katika ufanisi wa uzalishaji na ushirikiano na wakulima wa ndani.
Hata hivyo, sekta hii inakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwamo kupanda kwa gharama za nishati, ushindani wa bidhaa mbadala na shinikizo la kodi.
Changamoto hizi zinaifanya sekta ya bia kuhitaji mikakati ya muda mrefu inayojikita katika ubunifu wa bidhaa, uboreshaji wa teknolojia na ufanisi wa ugavi.
Aidha, idadi ya wawekezaji imeendelea kuongezeka ambapo mpaka sasa jumla ya wawekezaji zaidi ya 200 kutoka sehemu mbalimbami nchini kote wamewekeza hisa zao TBL, wakichangia ukuaji wa kampuni hiyo ya vileo nchini.
Mchango wa DSE
Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) limeendelea kuwa daraja muhimu kati ya sekta ya uzalishaji na mitaji ya wawekezaji.
Kupitia mfumo huu, kampuni za viwanda zimeweza kupata mitaji ya kupanua shughuli zao na kuongeza uwazi wa kifedha, jambo linaloimarisha imani ya wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
Takwimu za soko zinaonyesha kuwa thamani ya kampuni zilizoorodheshwa imefikia zaidi ya Sh35 trilioni huku uwekezaji kupitia soko la mitaji ukizidi Sh2 trilioni.
Hali hii inaonyesha kuongezeka kwa nafasi ya masoko ya mitaji kama injini ya ukuaji wa uchumi wa viwanda.
Mkurugenzi Mkuu wa DSE, Peter Nalitolela anaeleza kuwa maendeleo ya soko hilo yamejengwa na mageuzi ya muda mrefu tangu kuanzishwa kwake mwaka 1996 ikiwa ni pamoja na hatua za awali za kuorodhesha kampuni ya kwanza mwaka 1998 na baadaye kuimarika kwa mifumo ya biashara ya kielektroniki.
Kwa mtazamo wake, soko la mitaji limekuwa kiunganishi muhimu kati ya sekta ya fedha na sekta ya uzalishaji.
Mpaka sasa, jumla ya kampuni 28 zimeorodheshwa katika soko hilo zimeongeza uwekezaji wake, zikiwamo benki za National Microfinance Banck PLC (NMB) na benki ya CRDB.
Wito kwa wadau
Waziri wa Fedha, Hamisi Mussa Omar anasisitiza kuwa Tanzania ina mtaji wa kutosha unaoweza kuchochea ukuaji wa uchumi iwapo utatumika kikamilifu kupitia masoko ya mitaji.
Anaeleza kuwa bado kuna taasisi nyingi hazijajiunga na soko hilo hali inayopunguza kasi ya upatikanaji wa mitaji kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda na huduma.
“Ushiriki mpana wa sekta binafsi katika soko la mitaji utaongeza ajira, kupanua wigo wa uwekezaji na kuongeza mapato ya Serikali kwa njia endelevu,” anasema.
Ili kuendelea kuchochea hali hiyo, elimu ya uwekezaji inahitajika zaidi ili wananchi waweze kushiriki kikamilifu katika umiliki wa kampuni kubwa na kunufaika na ukuaji wa uchumi wa soko.