Sababu watalii kufanya utafiti wa mimea, viumbe hai Rungwe

Muonekano wa Ziwa Kisiba ambalo limeelezwa kuwa kivutio kwa watalii kufanya tafiti za viumbe hai.
Muktasari:
- Mlima Rungwe una vivutio vingi vya utalii likiwamo daraja la Mungu, Ziwa Ngozi na maporomoko.
Mbeya. Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe Mkoa wa Mbeya imesema kuna ongezeko kubwa la watalii wanaotembelea Hifadhi ya Mlima Rungwe na Ziwa Kisiba kufanya tafiti mbalimbali za mimea na viumbe hai.
Idadi hiyo imetajwa kuongeza kutoka wastani wa watalii 1,000 hadi kufikia 4,000 kwa kipindi cha mwaka 2020/2024.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumatano Februari 19, 2025, Ofisa Utalii wilayani Rungwe, Numwagile Bughali amesema ongezeko hilo ni baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kucheza Sinema ya Royal tour.

Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, Jafal Haniu (wa kwanza kushoto) akiwa amembata na watalii akihamasisha utalii wa ndani wa kupanda hifadhi ya Mlima Rungwe.
"Rungwe kuna vivutio vingi vya utalii kama daraja la Mungu, Ziwa Ngozi na maporomoko, lakini watalii wengi hutembelea zaidi vivutio hivyo viwili kwa lengo la kufanya tafiti za mimea na viumbe hai,” amesema Bughali.
Amesema licha ya ongezeko hilo, bado kuna changamoto ya miundombinu ya barabara ambayo husababisha baadhi ya vyombo vya usafiri kushindwa kuyafikia maeneo hayo sambamba na kukosekana kwa vituo vya kupumzika.
"Kwa magari yaliyo chini, kuna baadhi ya maeneo sio rahisi kuyafikia, lakini pia ukosefu wa miundombinu ya huduma muhimu kama vinywaji, chakula na maradhi,” amesema ofisa huyo.
Amesema kutokana na changamoto hizo, halmashauri imeanza kujiwekea mikakati ya kutangaza fursa za uwekezaji wa migahawa ya vyakula na maeneo ya kulala wageni.

Kwa upande wake, Bahati Longopa mdau wa utalii mkoani Mbeya, ameshauri Serikali kuwekeza nguvu kwenye ujenzi wa vituo vya kupumzika watalii na kujenga migahawa, nyumba za kulala ili kuongeza mapato ya halmashauri.
"Mlima Rungwe wenye urefu wa mita 2,981 ukiwa wa pili kwa urefu Tanzania, kuna njia pacha kabla haujafika kileleni, lakini hakuna kituo cha kupumzikia watalii, kuna haja ya kufanya tathimini ya kina itakayolenga kuboresha ili kuvutia watalii wengi zaidi kuja kufanya tafiti kwenye maeneo haya,” ameshauri.
Longopa amesema Serikali ya wilaya inapaswa pia kutenga bajeti kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya barabara sambamba na kutangaza fursa za uwekezaji kwa wazawa na wageni kutoka mataifa mbalimbali nchini kwenye maeneo ya vivutio hivyo vya utalii.