Sababu Tanzania kuwa nyuma mauzo ya Tanzanite yake duniani
Tanzanite ni jiwe adimu linalopatikana katika milima ya Mirerani nchini Tanzania pekee, karibu na Mlima Kilimanjaro, lina thamani kubwa duniani kutokana na upatikanaji wake pamoja na rangi yake ya kipekee ya buluu ya zambarau.
Licha ya kuwa chanzo pekee cha Tanzanite, Tanzania inashika nafasi ya pili kwa kiasi cha usafirishaji wa jiwe hilo nje ya nchi, ikitanguliwa na India na kufuatiwa na Vietnam.
Kwa mujibu wa ripoti ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), mauzo ya Tanzanite kutoka Tanzania nje ya nchi yalifikia thamani ya Dola za Kimarekani 19.2 milioni, mwaka 2024.
Kwa kulinganisha, takwimu zinazopatikana mtandaoni zinaonyesha kuwa mauzo ya Tanzanite kutoka India katika mwaka huohuo yalifikia takribani Dola 80 milioni.
Pamoja na jitihada za Serikali ya Tanzania kudhibiti sekta hiyo, ikiwemo ujenzi wa ukuta wa urefu wa kilomita 24 kuzunguka eneo la machimbo ya Mirerani mwaka 2018 ili kudhibiti utoroshaji na uchimbaji haramu, bado haijaweza kuongoza sokoni.
India inaendelea kutawala soko hilo kwa kuongoza na usafirishaji wa shehena 19,641 ikilinganishwa na shehena 6,956 kutoka Tanzania, hiyo ni kwa mujibu wa mtandao unaojihusisha na ufuatiliaji wa taarifa za biashara za kimataifa (Volza, Juni 2024).
Tofauti hii kubwa inazua maswali muhimu kuhusu uwepo wa mianya ya mtiririko haramu wa fedha (IFFs), magendo, na namna ambavyo nchi inapoteza mapato ya mabilioni kutokana na rasilimali yake ya kipekee.
Tanzania inapoteza mapato makubwa kwa kutonufaika na mnyororo wa thamani wa madini hayo, kulingana na wachambuzi mbalimbali uwezo wa kuongeza thamani ndani unatajwa kuwa unaweza kupindua meza.
Mmoja wa wauzaji wa Tanzanite jijini Arusha, Amir Mohammed anasema Tanzania inashindwa kutamba kwa kuwa uongezaji wa thamani haufanyiki kwa wingi hapa nchini.
“Mara nyingi sisi tunauza madini ghafi, kiwango kidogo sana kinauzwa hapa, kikiwa ni bidhaa ya mwisho, raia wengi wa India wananunua hapa na kwenda kuongeza thamani kwao, wakiuza wao wanauza kwa gharama kubwa,” anasema Mohammed.
Yahaya Samamba, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini anasema ukiachilia mbali utoroshaji, kuna uwezekano wa madini hayo yakawa yanatoka kihalali nchini, lakini kutokana na teknolojia na utaalamu wa kukata madini hayo yakawa na thamani kubwa India kuliko Tanzania.
“Kutokana na teknolojia kubwa iliyopo India ukilinganisha na Tanzania, wao wana uwezo wa kukata hadi yale mawe yenye thamani ya chini kabisa na kuyaongezea thamani kisha kuyasafirisha, hivyo kuonekana export (uuzaji wao) yao ni kubwa na gharama kubwa ikilinganishwa na sisi,” anasema Samamba.
Anasema Tanzania itaendelea na hatua ya kujenga uwezo wa ndani wa vifaa na utaalamu ili kufikia teknolojia ya juu ili kupata manufaa zaidi ya madini ya Tanzanite tofauti na sasa.
Aidha, Mei 2, 2025 wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka 2025/26, Waziri wa Madini, Antony Mavunde alisema Wizara yake inakusudia kudhibiti utoroshaji wa madini ya Tanzanite kwa kuweka ulazima wa wakaguzi na wathamini wa madini hayo kuvaa kofia ngumu zenye kamera.
Mavunde alisema lengo ni kurahisisha usimamizi na ufuatiliaji wa mwenendo kwenye Eneo Tengefu la Mirerani na masoko kunakofanyika biashara ya madini hayo. “Kutokana na mafanikio yatakayopatikana, utaratibu huu utatumika kwenye madini mengine ya vito.”
Waziri huyo alidokeza kuwa kuanzia Julai 2024 hadi Machi 2025 Wizara kwa kushirikiana na mamlaka nyingine za serikali imefanikiwa kukamata madini ya aina mbalimbali yenye thamani ya Sh17.75 bilioni katika mikoa ya kimadini 12.
Mikoa hiyo ni pamoja na Geita, Ruvuma, Kahama, Mwanza, Shinyanga, Kagera, Dar es Salaam, Mirerani, Simiyu, Singida, Chunya, Arusha na Lindi.
Alisema madini hayo yaliyokamatwa yalitaifishwa na watuhumiwa 75 walifikishwa kwenye vyombo vya Sheria.
“Ni rai yangu kwa wachimbaji na wafanyabiashara wa madini kujiepusha na utoroshaji wa madini ili kuepuka hasara kwenye biashara zao na Taifa kwa ujumla,” alisema.
Mwenyekiti kamati ya Tanzanite, Yusuf Money yeye anasema Tanzania bado ni kinara wa kuuza Tanzanite, lakini kwenye kunufaika ndiyo iko nyuma, kwani uongezaji wa thamani haufanyiki hapa kwa kiwango kikubwa.
“Ukiangalia katika mikoa miwili ya Arusha na Manyara kuna kituo kimoja tu cha kuongeza thamani katika madini hayo, hivyo kiasi kikubwa kinapelekwa nje ya nchi, ikiwemo India na Kenya kwa ajili ya kukatwa,” anasema.
Anasema ndiyo maana soko kubwa la madini hayo lipo India kwa kuwa wao ndio waongezaji thamani wakubwa, hata vitu vinavyovaliwa hapa kwa asilimia kubwa havijaongezewa thamani hapa.
Money anasema kwa kutoongeza thamani, Tanzania inapoteza mabilioni ya fedha katika mnyororo wa thamani wa madini hayo, kwani yakiwa ghafi yanauzwa Sh200,000 hadi Sh300,000 kwa gramu moja, lakini yaliyokatwa yanauzwa kwa dola 300 kwa karate moja.
Anasema gramu moja ghafi hutoa karate 2 hadi 2.5 hivyo waongezaji thamani wananufaika zaidi kuliko anayeuza ghafi, lakini pia kuna ajira zinapotea za ukataji na usafishaji.
Kuhusu utoroshaji wa madini hayo baada ya kujenga ukuta, anasema bado upo (bila kutaja kiwango) na kila siku watoroshaji wanakuja na mbinu mpya.
Hata hivyo, anaamini kuwa uongezaji thamani ukifanyika hapa nchini, vitendo vya kutorosha vitapungua, kwani mtu atakuwa na uhakika wa kupata thamani kubwa zaidi, akisema Tanzania hakuna utaalamu mkubwa wa kuongeza thamani madini hayo na mengine ya vito.
“India na Kenya walitutangulia katika uongezaji wa thamani na kwa ujumla utoroshaji una athari kubwa, lakini watu wanapeleka huko Kenya na India kwa kuwa wanajua wanapata thamani kubwa zaidi, lakini pia kuna wengine wanafanya tu kwa tabia na tamaa ya kupata faida zaidi,” anasema.
Hata hivyo, anaamini ujio wa masoko ya kidijitali na kuendelea kutoa ujuzi wa kuongeza thamani ya madini hayo hapa nchini kunaweza kupunguza utoroshaji na kuongeza thamani ya madini hayo katika uchumi wa Tanzania.
“Matamanio ni watu kuja kununua Tanzanite hata Tanzania kwa kuwa na minada kama ilivyokuwa zamani, tunataka watu waje kuchukua Tanzanite hapa, siyo kusubiri wapelekewe na Wahindi. Mapinduzi ya kidijitali nayo yanatusaidia, pengine watoto wetu watafanya vizuri zaidi,” anasema.
Akizungumzia sababu za Tanzania kutoongoza katika soko la Dunia, Money anasema wakati madini hayo yanavumbuliwa mwaka 1967, India na baadhi ya nchi nyingine ziliona thamani yake mapema na kuhifadhi na sasa wanayauza.
“Wao waliijua thamani yake kabla yetu, wakayanunua na kuyahifadhi, sasa wanauza kwa bei kubwa, licha ya kuwa waliyachukua kwa bei ndogo. Unajua Tanzanite ni mbadala wa Blue Suphire ambayo inauzwa pesa nyingi karibu mara 10, hivyo watu wasio na uwezo mkubwa wanakimbilia Tanzanite,” anasema.
Mhadhiri wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm), Profesa Abel Kinyondo anasema bila shaka kuna utoroshaji wa madini hayo ndiyo maana mzalishaji mkubwa sio muuzaji mkubwa.
“Kwenye kuongeza thamani tunapoteza zaidi pengine kuliko hata kwenye utoroshaji. Tatizo letu kubwa tunasafirisha madini ambayo hayajaongezwa thamani, hivyo tunapata manufaa kidogo na watoroshaji wanaweza kupata manufaa zaidi,” amesema Profesa Kinyondo.
Anasema ni muhimu kuwekeza kwenye viwanda vya ndani vya kuongeza thamani ya madini hayo ili yasaidie kuinua sekta nyingine muhimu ili kutoa manufaa mapana ya kiuchumi.
Mhadhiri Mwandamizi wa Shule Kuu ya Biashara, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Thobias Swai anasema muhimu sasa ni kuvutia uwekezaji wa uongezaji wa thamani katika madini hapa nchini, ili kunufaika na mnyororo wa thamani.
“Bila kuwekeza katika mnyororo wa thamani tutapoteza pesa nyingine, hata kampuni nyingi za huduma tunazotumia kama Bolt, Air BnB zote thamani kubwa inaenda nje badala ya kubaki,” anasema Dk Swai.
Maoni tofauti
Miaka miwili iliyopita wadau wa madini ya Tanzanite waliiomba Serikali kutumia taasisi zake kudhibiti watu wanaoeneza taarifa za upotoshaji kwamba madini hayo yanaendelea kutoroshwa kwa wingi licha kuwepo kwa udhibiti.
Januari 16, mwaka huu, Mwenyekiti wa Chama cha Wanunuzi na Wauzaji Madini Tanzania (TAMIDA), Sammy Mollel aliwaambia waandishi wa habari kuwa athari za kuendelea kufumbia macho upotoshaji huo ni kubwa na licha ya kuendelea kudumaza soko la madini hayo.
Mollel alisema kuwa wao kama wadau sekta hiyo wamesikitishwa na taarifa hizo na amewataka Watanzania kutoa ushirikiano ukiwemo wa kuwabaini watu wanaoeneza taarifa hizo.
“Tangu kujengwa kwa ukuta katika eneo hilo mwaka 2017 na kufungwa kwa mitambo ya kielektroniki ya ulinzi kumesaidia kuondoa mianya ya utoroshaji wa madini na kwa hali inayoonekana hapa hakuna utoroshaji unaoweza kufanyika kutokana na udhibiti mkubwa uliopo,” alisema Mollel.
Aliongeza kuwa kama mtu ana uhakika na taarifa hizo ni vizuri akatoa ushirikiano kwa kutoa ushahidi namna madini hayo yanatoroshwa pamoja na kuonyesha mianya yote inapopitia ili wanaohusika wachukuliwe hatua.
Ofisa Madini Mkazi Mirerani, Menard Msengi aliyekuwepo wakati huo, alisema kuwa serikali imeweka ulinzi wa kutosha na mazingira mazuri kuanzia kwenye miradi hadi kufikia sokoni katika kuhakikisha sheria zote zinafuatwa na kwa ulinzi uliopo swala la utoroshaji haliwezi kufanyika hata kidogo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Wanunuzi Wadogo wadogo wa Madini Tanzania (CHAMATA), Jeremia Kituyo anasema taarifa za kuwepo kwa utoroshaji wa madini zinasababisha washindwe kufanya biashara, kwani zinawaondolea uaminifu kwa wateja wao na wamesisitiza umuhimu vyombo vinavyohusika kufuatilia na kudhibiti tatizo hilo.
“Tunasikitika sana na matamko yanayotolewa yasiyo na ushahidi kwamba madini yanatoroshwa, ambapo yanatufedhehesha na kutuvunja moyo na kuharibu sura ya biashara ya madini nchini, ambayo matamshi hayo wanaweza kusababisha mataifa mengine kuona kama madini yetu yana migogoro kitendo ambacho sio kweli,” anasema Kituyo.
Habari hii ilipata ufadhili wa Taasisi ya Thomson Reuters Foundation kupitia Wakifu wa Vyombo vya Habari Afrika Magharibi (MFWA), ufadhili huo haujaingilia uhuru wa mwandishi wala kushawishi aina ya maudhui.