Nini kifanyike kuongeza miamala ya pesa kidijitali

Fikiria dunia ambayo kutuma pesa ni rahisi kama kuweka chumvi kwenye chakula. Hii inawezekana kupitia mifumo ya malipo ya kidijitali inayoweza kusomana, ambapo watumiaji wanaweza kutuma pesa kwa mitandao tofauti ndani ya dakika chache.
Mwingiliano wa mifumo ya malipo (interoperability) ni dhana muhimu sana katika maendeleo ya teknolojia ya malipo ya fedha kidijitali. Inawawezesha watumiaji wa huduma za kifedha kutuma na kupokea miamala kwa urahisi, haraka, na bila matatizo kutoka kwenye mifumo tofauti ya malipo mfano kibenki, mitandao ya simu, bila ya kulazimika kubadili mtoa huduma.
Kwa mfano, mtu anaweza kutuma pesa kutoka benki moja kwenda nyingine, au kufanya miamala ya pesa kupitia simu za mkononi kutoka kampuni moja kwenda nyingine, bila kuhitaji kuwa wateja wa benki moja au kubadili laini ya simu ili kufanikisha muamala.
Ni sawa na kusema kuifanya mifumo ya malipo kuongea “lugha moja,” ingawa kila mfumo umeundwa na unajiendesha kivyake. Inaleta wepesi mkubwa wa kutuma na kupokea pesa kwa kuondoa vikwazo vya kuingiliana kiufundi.
Hapa nchini utumaji wa miamala kati ya mifumo tofauti ya malipo umekua kwa kasi tangu kubuniwa kwa mfumo wa Benki Kuu Tanzania unaowezesha mifumo ya malipo kidijiti kusomana na kufanya malipo kwa haraka, ujulikanao kama TIPS (Tanzania Instant Payment System).
Takwimu kutoka ripoti ya mwaka ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) zinaonesha kuwa mwaka 2023, mfumo wa TIPS ulisajili miamala milioni 235 yenye thamani ya Sh12.27 trilioni, wastani wa miamala 650,000 ikifanyika kila siku. Pia, kulikuwa na watoa huduma za malipo kidijitali 45 waliotumia mfumo huu.
Hii inaonyesha kuwa TIPS, kama daraja linalounganisha mifumo tofauti ya malipo, imewezesha watumiaji wengi “kuvuka”, kwa kuongezeka idadi ya miamala, na kuleta urahisi wa kutuma na kupokea fedha kutoka mifumo mbalimbali.
Kwa mfano, ufanyaji malipo kwa njia ya Lipa Namba umeleta faida kwa kuongeza idadi ya miamala ya malipo kutoka mteja kwenda biashara kwa asilimia 83, kutoka miamala milioni 153.73 hadi milioni 280.79 mwaka 2023. Hii ina maana kuwa wateja sasa wanaweza kulipia bidhaa kwa urahisi na haraka kutoka mtandao wowote wa simu, bila kubeba fedha taslimu au kadi nyingi za malipo.
Vilevile, urahisi wa kutumiana fedha kati ya watu binafsi (P2P) umeongezeka kwa kiasi kikubwa. Taarifa zinaonesha thamani ya malipo baina ya watu binafsi imefikia Sh11.32 trilioni mwaka 2023. Kuingiliana kwa mifumo ya malipo imerahisisha kulipia bidhaa za nyumbani, au kutuma pesa kwa ndugu na jamaa, bila kikwazo chochote katikati.
Hata hivyo, ili kuongeza matumizi ya kutuma miamala kati ya mifumo ya malipo, ni muhimu kuangalia ada za utumaji. Ipo dhana kuwa ada za kuhamisha fedha kutoka mfumo mmoja wa malipo kidijitali kwenda mwingine ni kubwa, hasa kwa watumiaji wa kipato cha chini na wale wanaofanya miamala midogo. Kupunguza ada hizi kunaweza kusaidia kujenga imani na kuhamasisha matumizi zaidi ya mifumo hiyo.
Vilevile, licha ya kuwepo kwa mifumo ya malipo, watu wengi bado wanaweza wasielewe jinsi ya kuitumia, labda kutokana na ujuzi mdogo wa masuala ya teknolojia na huduma za kifedha. Hii ni hasa katika maeneo ya nje ya miji au yale yasiyofikiwa vizuri na huduma za intaneti. Wadau wanapaswa kuongeza juhudi za kuelimisha jamii kuhusu masuala haya ili kuongeza matumizi ya mifumo ya malipo.
Aidha, malipo ya kidijitali yanavyozidi kuongezeka, hatari ya udanganyifu na matapeli pia imeongezeka. Kwa hiyo, ni muhimu kuwafundisha watumiaji jinsi ya kujilinda dhidi ya udanganyifu wa kifedha. Pia, juhudi za kudumu za kuboresha usalama ni muhimu ili kujenga imani katika mifumo hii.
Mafunzo endelevu kwa mawakala wa fedha ni muhimu. Mawakala, kama kiungo muhimu kwa watumiaji wengi wa huduma za kifedha mitaani, wanapaswa kuelewa vizuri mifumo ya malipo, njia za usalama, taratibu za kuhifadhi taarifa, na mengine. Hii itawasaidia kuwapa wateja elimu bora na kuhamasisha matumizi makubwa ya mifumo ya malipo.