Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Namibia, Tanzania zatia saini mkataba kukuza ufugaji nyuki na utalii

Mjasiriamali kutoka Namibia na Meneja wa Okongo Conservancy, Hilya Nghiwete katikati wakisaini hati ya makubaliano na Mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa Kijiji Cha Nyuki, Philemon Kiemi (kulia) katika kongamano la Biashara kati ya Tanzania na Namibia lililofanyika jana Juni 20, 2026.

Muktasari:

  • Makubaliano hayo yalisainiwa jana wakati wa kongamano la biashara la marais wa Tanzania na Namibia lililofanyika sambamba na ziara ya kitaifa ya Rais wa Namibia, Dk Netumbo Nandi-Ndaitwah.

Dar es Salaam. Tanzania na Namibia zimeingia mkataba wa ushirikiano wa miaka mitano wa kuendeleza ufugaji nyuki na utalii, huku kukiwa na mpango wa kuanzisha taasisi ya utafiti na mafunzo ya ufugaji nyuki nchini Namibia.

Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa leo, Juni 21, 2026, ushirikiano huo unahusisha kampuni ya kizawa ya Tanzania, Kijiji Cha Nyuki Company Limited.

Makubaliano hayo yalisainiwa jana, Jumamosi, Juni 20, 2026, wakati wa Kongamano la Biashara la Marais wa Tanzania na Namibia lililofanyika sambamba na ziara ya kitaifa ya Rais wa Namibia, Dk Netumbo Nandi-Ndaitwah.

Ushirikiano huo unazikutanisha Kijiji Cha Nyuki Company Limited, Chuo cha Jamii cha Nknongo na Apimondia, shirikisho la kimataifa la vyama vya wafugaji nyuki, katika mpango unaolenga kuimarisha ushirikiano katika ufugaji nyuki, uhifadhi wa mazingira, utafiti, huduma za uchavushaji wa mazao kibiashara, maendeleo ya ujuzi na utalii.

Chini ya makubaliano hayo, vijana kutoka nchi zote mbili watanufaika na programu maalumu za kubadilishana maarifa, ambapo Tanzania itashiriki uzoefu wake katika ufugaji nyuki huku Namibia ikitoa uzoefu wake katika maendeleo ya utalii unaoshirikisha jamii.

Akizungumza baada ya utiaji saini huo, mjasiriamali wa kijamii kutoka Namibia na Meneja wa Okongo Conservancy, Hilya Nghiwete, amesema mafanikio ya Tanzania katika kubadilisha maisha ya jamii za vijijini kupitia ufugaji nyuki ndiyo yaliyomhamasisha kuanzisha ushirikiano huo.

Amesema kwa miezi sita iliyopita amekuwa akishirikiana na wadau mbalimbali wa sekta ya ufugaji nyuki nchini Tanzania, ikiwemo Kijiji Cha Nyuki kilichopo Singida, ili kujifunza namna ambavyo mfano huo unaweza kuigwa nchini Namibia.

“Nimefuatilia kwa karibu maendeleo ya sekta ya ufugaji nyuki nchini Tanzania na jinsi miradi ya ufugaji nyuki ilivyobadilisha vijiji kuwa vituo vya ajira na uzalishaji wa kipato,” amesema.

Nghiwete amesema mradi huo unalenga kutengeneza fursa endelevu za kujikimu kwa jamii za asili, hususan jamii ya Wasan pamoja na wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

“Mpango huu umeundwa si tu kwa ajili ya kuunda fursa za kipato, bali pia kukuza utu, ushirikishwaji na matumizi endelevu ya rasilimali za asili,” amesema.

Kwa upande wa Tanzania, Mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa Kijiji Cha Nyuki, Philemon Kiemi, amesema makubaliano hayo ni hatua kubwa kwa sekta ya ufugaji nyuki nchini.

Kiemi amesema mkataba huo wa miaka mitano utaiwezesha kampuni hiyo kusaidia kuanzishwa kwa taasisi ya utafiti wa ufugaji nyuki nchini Namibia huku ikipanua mfano wa Tanzania wa ufugaji nyuki katika nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

“Haya ni mafanikio makubwa kwa sababu sasa tunapanua sekta ya ufugaji nyuki katika nchi za SADC kupitia mfano ambao tayari umeonyesha mafanikio nchini Tanzania,” amesema.

Amesema kampuni hiyo imekua kwa kiasi kikubwa na sasa inazalisha bidhaa mbalimbali zinazotokana na nyuki huku ikiendelea kupanua shughuli zake katika vijiji vingi zaidi nchini.

“Namibia ina uzoefu mkubwa katika utalii, wakati Tanzania ina utaalamu katika ufugaji nyuki. Kupitia ushirikiano huu, vijana wa nchi zote mbili watapata fursa ya kujifunza kutoka kwa wenzao,” amesema.

Kiemi ameongeza kuwa mpango huo unaendana na jitihada pana za kuunganisha biashara za ndani na washirika wa kimataifa ili kukuza uwekezaji, ubunifu na uhamishaji wa ujuzi.

Amesema ushirikiano kama huo tayari unaendelea nchini Zimbabwe na kuna mipango ya kuupeleka katika nchi nyingine za Afrika.

Kamishna wa Kanda wa Afrika wa Apimondia, David Mkoma, ameeleza makubaliano hayo kuwa hatua muhimu katika juhudi za kupanua mifano ya maendeleo iliyoanzishwa na Waafrika na ambayo imeonyesha mafanikio barani humo.

Amesema vijiji vya ufugaji nyuki vya Tanzania vimeonyesha jinsi sekta hiyo inavyoweza kubadilisha uchumi wa vijijini kwa kuunda ajira huku ikichangia uhifadhi wa mazingira.

“Ninafurahi sana kuona ushirikiano huu sasa ukianza kutekelezwa nchini Namibia, ambako kuna dhamira thabiti ya kuhakikisha jamii zinanufaika na ufugaji nyuki kama shughuli endelevu ya kiuchumi,” amesema.