Mramba: Kununua umeme Ethiopia kuna faida kuliko hasara

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Felchesmi Mramba.
Muktasari:
- Rais Samia Suluhu Hassan alisema Serikali ipo katika mchakato wa kununua umeme kutoka nje ya nchi kama suluhisho la kudumu kwa changamoto ya kukatika kwa umeme mara kwa mara katika Kanda ya Kaskazini.
Dar es Salaam. Kauli ya Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu mchakato wa kununua umeme kutoka Ethiopia, imeendelea kuwaibua maofisa wa Serikali kuifafanua kwamba kuna manufaa kwa nchi na sio hasara kama inavyodhaniwa na baadhi ya watu.
Miongoni mwa wengine, waliotoa ufafanuzi huo ni pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Felchesmi Mramba na Gerson Msigwa, msemaji mkuu wa Serikali
Jana, Rais Samia Suluhu Hassan alizungumza na wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Kiwanja cha CD Msuya, kilichopo Wilaya ya Mwanga, baada ya kuzindua mradi mkubwa wa maji wa Same-Mwanga-Korogwe, ambao umegharimu Shilingi bilioni 400.
Katika hotuba yake, Rais Samia alisema Serikali ipo katika mchakato wa kununua umeme kutoka nje ya nchi kama suluhisho la kudumu kwa changamoto ya kukatika kwa umeme mara kwa mara katika Kanda ya Kaskazini.
“Lakini, Serikali yetu inachukua hatua ya kununua umeme nje, maalumu kwa ajili ya mikoa hii ya kaskazini ili umeme upatikane saa 24, muda wote bila kukatika," alisema Rais Samia.
Alisema upatikanaji wa umeme wa uhakika unachochea maendeleo ya nchi na wananchi kwa jumla.
"Tupo kwenye hatua za mwisho kusaini mkataba ili tuweze kununua umeme nje ya nchi, uungwe Kanda ya Kaskazini ili wananchi waweze kupata umeme," alisema.
Kauli hiyo ya Rais Samia iliibua mjadala na ukosoaji kwenye mitandao ya kijamii, wengi wakihoji kuhusu umuhimu wa Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere lililojengwa kwa mabilioni ya shilingi na hivyo kusababisha maofisa hao wa Serikali kujitokeza kutoa ufafanuzi.
Si hasara ni faida
Katikati ya mjadala huo, leo Jumatatu ya Machi 10, 2025 Mramba amewaeleza waandishi wa habari kuwa uamuzi wa Tanzania kuchukua umeme Ethiopia ni kitu chenye faida na si hasara kama watu wanavyodhani.
Mramba amesema ni faida kwa kuwa baadhi ya vyanzo vya umeme hapa nchini vinazalisha uniti moja kwa bei kubwa kuliko bei ambayo umeme huo utanunuliwa kutoka Ethiopia.
"Huo umeme wa Ethiopia tunanunua kwa senti za Marekani 0.077 lakini tuna vyanzo vingi ambavyo vinazalisha kwa gharama ya juu zaidi hivyo hii ni nafuu kwetu," amesema na kuongeza umeme utaonunuliwa Ethiopia ni Megawati 100 tu.
Amesema umeme unaopelekwa mikoa ya kaskazini unapotea kwa kiwango cha megawati 17 ambazo zinatosha kuhudumia Mkoa wa Songwe (unaotumia Mega 14) na zaidi.
"Hata huo wetu unaokuja kutoka Ethiopia utakuwa na hasara lakini hiyo hasara haituhusu, sisi tunanunulia mpakani Namanga, lakini tukipeleka sisi (Namanga) tunatumia gharama kubwa," amesema Mramba.
Ameongeza kuwa "wachumi na wataalamu wote waliofanya tathmini juu ya jambo hilo waliona ni faida kubwa kuliko hasara."
Aidha Mramba amemshukuru Rais Samia kwa kuridhia ununuzi wa umeme huo na kuongeza kuwa ufafanuzi uliotolewa na Msemaji wa Serikali baada kuibuka kwa mjadala huo uko sahihi.
"Maelezo ya msemaji wa Serikali yako sawa, hayana dosari," amesema Mramba na kuongeza kuwa suala la mauziano ya umeme ya nchi na nchi ni la kawaida na mpaka sasa Tanzania inauza na kununua umeme kutoka mataifa tofauti zaidi ya matatu.
Lengo kuokoa gharama
Jana Machi 9 muda mfupi baada ya kauli ya Rais Samia, Msigwa ilitoa ufafanuzi ikisema mpango wa Serikali wa kununua umeme kutoka nje kwa ajili ya mikoa ya Kaskazini, unalenga kuokoa gharama zinazopotea kwa usafirishaji wa nishati hiyo kutoka unakozalishwa.
Taarifa ya Msigwa ilieleza kuwa kwa Kanda ya Kaskazini, upotevu wa umeme unaosafirishwa umekuwa ukisababisha hasara ya zaidi ya Sh32 bilioni kwa mwaka.
"Kutokana na upotevu huo, Kanda ya Kaskazini imekuwa ikikabiliwa na changamoto ya kukatika mara kwa mara kwa umeme, hali inayowaathiri wananchi," ilieleza taarifa hiyo.
Alisema ununuzi wa umeme kutoka Ethiopia kupitia Kenya utasaidia kupunguza changamoto ya kukatika kwa huduma na kuondoa upotevu wa umeme unaokwenda Kaskazini.
Msigwa alisisitiza kuwa gharama ya umeme unaonunuliwa Ethiopia ni nafuu kutokana na Tanzania kuwa mwanachama wa Gridi ya Ukanda wa Kaskazini mwa Afrika ambapo nchi zina makubaliano ya kuuziana umeme kwa gharama nafuu, ambazo zinalingana ama na gharama za uzalishaji au chini yake.
"Utaratibu wa Tanzania kununua umeme nje, umekuwa ukifanyika kwa miaka mingi, hasa kwa mikoa ya Rukwa, Tanga na Kagera," imeeleza taarifa hiyo.
Pia, imesema lengo la kununua umeme katika maeneo ya pembezoni ni kuwezesha gridi ya taifa na kufanya iwe na mbadala wa kupata umeme pale inapotokea changamoto.