Prime
Mkutano wa kahawa utagusa hivi uchumi wetu

Kahawa ni mojawapo ya bidhaa muhimu zaidi duniani, ikiwa ya nne kwa thamani ya mauzo baada ya mafuta, dhahabu na gesi asilia. Soko la kahawa lina thamani ya Dola za Marekani bilioni 500 (Karibu Sh130 trilioni), huku nchi 50 duniani zikijihusisha na uzalishaji wake.
Kati ya hizo, 25 zinapatikana barani Afrika, ikiwemo Tanzania. Hata hivyo, licha ya kuwa na idadi kubwa ya wazalishaji, Afrika inauza kahawa ghafi kwa thamani ya Dola bilioni 2.5 (Sh6.4 trilioni) pekee, huku Tanzania ikichangia Dola milioni 240 (Sh621.8 bilioni).
Katika miaka mitatu iliyopita, Tanzania imeongeza uzalishaji wa kahawa kutoka tani 55,000 hadi tani 85,000. Hata hivyo, changamoto kubwa inabaki kuwa Afrika inauza kahawa kama malighafi na kuagiza kahawa iliyoongezewa thamani kutoka nje, hali inayosababisha upotevu mkubwa wa mapato.
Kwa sasa, kahawa ghafi inauzwa kwa wastani wa Dola nne kwa kilo, wakati kahawa iliyosindikwa huuzwa kwa karibu Dola 20. Ikiwa wazalishaji wa Afrika watawekeza katika viwanda vya usindikaji na kuongeza thamani kabla ya kuuza nje, basi bara hili linaweza kuongeza mapato yake na kuhakikisha wakulima wanapata faida kubwa zaidi.
Wadau wanaamini kuwa wazalishaji wa Afrika wakiunganisha nguvu wanaweza kusaidia katika kujadili mikataba yenye tija na kuhakikisha Afrika inanufaika ipasavyo na zao la kahawa, ambalo limekuwa tegemeo kwa mamilioni ya wakulima barani.
Pia ushirikiano huo unaweza kujikita katika kuboresha mnyororo wa thamani wa kahawa, kubuni mbinu za usindikaji wa ndani, na kujenga masoko ya pamoja yatakayowezesha bidhaa za kahawa zenye thamani kuuzwa kwa bei bora zaidi.
Kutokana na umuhimu wa ushirikiano wa wazalishaji wa zao hilo la biashara ambalo limekuwa likiuzwa kimataifa kwa karne kadhaa, wamekuwa wakifanya mikutano kwa ajili majadiliano na mikakati mbalimbali.
Februari 21 na 22, 2024 mkutano wa tatu wa wazalishaji wa kahawa barani Afrika unatarajiwa kufanyika jijini Dar katika ukumbi wa Mwalimu Julias Nyerere, ambao utakutanisha nchi 25 zote za Afrika zinaozalisha zao hilo na kwa siku ya kwanza itakuwa ni mkutano wa mawaziri na siku ya pili itakuwa ni zamu ya wakuu wa nchi.
Akizungumza kuhusu mkutano huo, Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe anasema watu zaidi ya watu 1,000 wanatarajiwa kukutana ili kujadili na kukubaliana kuhusu zao la kahawa barani Afrika.
Anasema Tanzania imechaguliwa kuwa mwenyeji wa mkutano huo kwa kuwa imepiga hatua kubwa katika uzalishaji wa kahawa ndani ya kipindi cha miaka mitatu iliyopita.
“Miaka mitatu iliyopita bei ya mkulima (wa kahawa) imeendelea kuimarika, uzalishaji umeongezeka na tunaelekea kuwa moja kati ya nchi muhimu sana katika uzalishaji wa kahawa duniani,” anasema.
Anasema mkutano huo utakutanisha watunga sera, wafanyabiashara wa zao la kahawa, pamoja na makampuni makubwa duniani, hivyo hiyo ni fursa kwa nchi kushiriki mkutano huo muhimu.
“Mkutano huu ni msingi mkubwa ambao mataifa ya Afrika yameamua kuufanya Tanzania ili kuendana na Azimio la Kampala ambalo liliona umuhimu wa mataifa ya Afrika kufanya biashara wenyewe, kuongeza thamani ya mazao na kuuziana wenyewe, badala ya kuisafirisha kahawa ikiwa ghafi, tunaweza kuiongezea thamani hapa,” anasema.
Bashe anaongeza kuwa Afrika mataifa ambayo yananunua sana kahawa ndani ya bara na yana matumizi makubwa ya kahawa lakini wanaagiza kwa kiasi kikubwa nje ya nchi miongoni mwa nchi hizo ni Afrika Kusini.
Mwanzoni mwa mwaka huu wakati akielezea kuwepo kwa mkutano huo, Waziri Bashe alisema: "Asilimia 50 ya kahawa inayokwenda kwenye soko la dunia inatoka Afrika, lakini mapato yetu ni madogo kwa sababu tunazalisha na kuuza kahawa ghafi, tofauti na nchi nyingine zinazoongeza thamani kabla ya kuuza".
Alisema licha ya mapato hayo duni, nchi za Afrika zinaagiza kahawa iliyoongezwa thamani kwa gharama ya Dola 6 bilioni za Marekani kwa mwaka, kiwango ambacho ni kikubwa kuliko mapato yanayotokana na kuuza kahawa ghafi.
Mojawapo ya ajenda kuu za mkutano huo ni kuweka mikakati ya kuongeza thamani ya kahawa inayozalishwa barani Afrika kwa miaka kumi ijayo ili kuongeza mapato na kunufaisha wakulima na nchi zinazolima kahawa.
Waziri Bashe anasema ushirikiano na sekta binafsi ni muhimu katika kufanikisha mabadiliko haya, kwa kuwashirikisha katika mnyororo wa thamani na kuwapa fursa za kuongeza thamani kwa kutumia masoko ya kimataifa.
"Serikali ya Tanzania, kwa upande wake inaendelea kuimarisha sekta ya kahawa kwa kuwasaidia wakulima," anasema Bashe na kuongeza kuwa tayari miche milioni 20 ya kahawa imetolewa bure kwa wakulima kupitia ruzuku, ikiwa ni moja na mikakati ya kuongeza uzalishaji na ubora wa kahawa nchini.
Mchambuzi wa masuala ya uchumi, Aziz Rashid alisema kwa kuzingatia kaulimbiu ya mkutano huo isemayo "Kufungua Fursa za Ajira kwa Vijana Kupitia Uboreshaji wa Sekta ya Kahawa Afrika”, Bara la Afrika linaweza kunufaika zaidi na zao hilo.
Rashid, ambaye ni mkufunzi wa Chuo Kiku Ardhi anasema awali nchi za Afrika, ikiwemo Tanzania zilikuwa zikizalisha zao hilo kwa wingi, lakini hapo kati zilishindwa kwendana na mwenendo wa soko, hivyo kujikuta zikipata manufaa kidunchu.
“Kilimo cha kawa kilirithiwa kwa wakoloni, hivyo kimekuwepo kwa muda mrefu, lakini ufanisi wake siyo mzuri, mikutano kama hii inaweza kutoa mwanga mpya endapo kutakuwa na mijadala ya kisera ambayo inaweza kuchangia uendelevu wake,” alisema Rashid.
Aidha, anasema mataifa ya Afrika yanapaswa kuboresha eneo la utafiti, kama ambavyo wazalishaji wakubwa wanafanya, lakini pia kuongeza thamani hapa nchini ili kunufaika na mnyororo wa thamani.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Kahawa Bora za Afrika (AFCA), Gilbert Gatali anasema maonyesho hayo yataitangaza nchi kutokana na sifa walizonazo Watanzania za ukarimu wa kipekee na uzalishaji wa kahawa.
"Tanzania tunayo furaha kurudisha tukio hili muhimu katika nchi hii nzuri, wahudhuriaji watapata fursa ya kushiriki katika safari ya kahawa, kuchunguza mashamba ya kahawa maarufu nchini Tanzania na mandhari ya asili ya kuvutia, ikiwa ni pamoja na Bonde la Ngorongoro na Ziwa Manyara," anasema Gatali.
Anasema, dhamira ya AFCA ni kukuza maarifa na uhusiano wa kibiashara ndani ya sekta ya kahawa na mkutano ujao unaahidi kuwa jukwaa muhimu la mitandao, kujifunza na ukuaji wa biashara.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB), Primus Kimaryo anasema mkutano huo unalenga kuimarisha sekta ya kahawa kwa manufaa ya wadau wote, kuanzia wakulima hadi watumiaji.
"Wakulima nchini, wakisaidiwa na vyama vya ushirika na huduma za ugani, wamejitolea kudumisha na kuimarisha urithi huu," anasema Kimaryo.
Anaongeza kuwa bara la Afrika limekuwa muhimu katika historia ya uzalishaji na uuzaji wa kahawa duniani, Tanzania, Ethiopia, Uganda, Ivory Coast na Kenya zikiwa miongoni mwa wazalishaji wakuu wa zao hilo.
Kimaryo anasema Tanzania inajivunia urithi mkubwa wa aina mbalimbali za kahawa za ubora wa juu, ikiwa ni pamoja na Arabica na Robusta.
Hata hivyo, tukio hilo linatoa fursa ya kipekee kwa wadau nchini kujifunza kutoka kwa wataalamu wa kimataifa na kutumia mbinu bora za kuimarisha uwepo wao katika soko la kimataifa.
Anasisitiza mahitaji ya mbinu shirikishi na bunifu ili kushughulikia changamoto kubwa, kama vile mabadiliko ya hali ya hewa na soko.
Kwa mujibu wa takwimu za TCB, zaidi ya asilimia 93 ya kahawa inayozalishwa nchini inategemea soko la nje, huku asilimia saba pekee ikitumika ndani ya nchi.