Miaka 105 ya CPC, wadau waeleza
Baadhi ya Viongozi wa China na Tanzania wakishiriki maadhimisho ya miaka 105 ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) Katika Ubalozi wa China jinini Dar es Salaam, Mwezi Julai, 2026.
Muktasari:
- Wadau wanasema safari ya China kuwa uchumi mkubwa duniani imejengwa na sera za muda mrefu Kikomunisti Katika uwekezaji kwenye viwanda, teknolojia, rasilimali watu na uongozi wenye dira.
Dar es Salaam. Wadau wa siasa, diplomasia na wasomi nchini Tanzania wamesema safari ya China kutoka taifa lenye changamoto kubwa za kiuchumi hadi kuwa miongoni mwa nchi zenye uchumi mkubwa duniani imechangiwa na uongozi wa Chama cha Kikomunisti cha China (CPC), sera thabiti na mipango ya muda mrefu ya maendeleo.
Kauli hizo zilitolewa Julai 21, 2026 katika mdahalo wa meza ya duara ulioandaliwa na Ubalozi wa China nchini Tanzania wenye kaulimbiu “Karne ya Mafanikio: Chama cha Kikomunisti cha China kwa Mtazamo wa Watanzania, Maadhimisho ya Miaka 105 tangu Kuanzishwa kwa CPC.”
Katika mjadala huo, Balozi wa China nchini Tanzania, Chen Mingjian, alisema CPC ilianza ikiwa na wanachama wapatao 50 na sasa imekua na kuwa chama chenye wanachama zaidi ya milioni 100 kinachoongoza taifa lenye watu zaidi ya bilioni 1.4.
Alisema baada ya kuanzishwa kwa Jamhuri ya Watu wa China mwaka 1949 chini ya Mwenyekiti Mao Zedong, China iliweka misingi ya ujenzi wa taifa, huku mageuzi ya kiuchumi yaliyofuata yakifungua njia ya ukuaji wa viwanda, biashara na teknolojia.
“Miaka 105 ya CPC si mafanikio ya China pekee, bali ni safari yenye umuhimu kwa dunia. Mafanikio haya yamejengwa na umoja wa wananchi na mikakati ya maendeleo,” alisema Chen.
Alisema China imefanikiwa kupunguza umaskini, kujenga miundombinu mikubwa na kuwekeza katika sayansi na ubunifu, hatua zilizoifanya kuwa moja ya mataifa yanayoongoza kiuchumi duniani.
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Idara ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Rabia Abdalla Hamid, alisema uzoefu wa CPC unaonyesha umuhimu wa kuwa na dira ya maendeleo na usimamizi madhubuti wa sera.
“Tunaipongeza CPC kwa mafanikio yake katika kuimarisha viwanda, teknolojia, elimu na afya. Pia ushirikiano wetu umeendelea kupitia mafunzo na kubadilishana uzoefu wa uongozi,” alisema.
Naye Mbunge wa Songea Mjini, Dk Damas Ndumbaro, alisema China ni mfano wa taifa lililoweza kubadilika kupitia mipango ya muda mrefu na uwekezaji kwa wananchi.
“China ni rafiki wa kweli wa Tanzania. Reli ya Tazara ni alama ya urafiki na ushirikiano wetu wa muda mrefu,” alisema.
Kwa upande wake, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Dodoma, Dk Neema Majule, alisema mafanikio ya China yanaonyesha umuhimu wa kuwekeza katika rasilimali watu, sayansi na teknolojia.
Somo kwa nchi zinazoendelea
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sera za Kimataifa Afrika (CIP Africa), Balozi Omary Mjenga, alisema uzoefu wa China ni somo kwa nchi zinazoendelea.
“China imeonyesha umuhimu wa kuwa na mikakati ya kitaifa, kutumia ubunifu na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika kukuza uchumi,” alisema.
Mtazamo huo unaendelezwa na aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini China, Luteni Jenerali mstaafu Abdulrahman Shimbo, aliyesema mabadiliko ya China yanaonyesha namna taifa linaweza kupiga hatua kupitia uongozi wenye dira.
Naye Mkuu wa Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere, Profesa Marcellina Chijoriga, alisema safari ya China ni somo la uongozi na utekelezaji wa mipango ya maendeleo.
“Maendeleo endelevu yanahitaji maono, nidhamu katika utekelezaji na kuzingatia maslahi ya wananchi,” alisema.
Akifafanua historia ya Tanzania na China, Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Julius Nyerere, Joseph Butiku, alisema urafiki wa Tanzania na China uliojengwa na waasisi wa mataifa hayo umeendelea kuwa msingi wa ushirikiano.
Alisema miaka 105 ya CPC inaonesha kuwa uongozi wenye mipango ya muda mrefu unaweza kuibadilisha nchi kutoka katika changamoto za kiuchumi hadi kuwa nguvu kubwa ya maendeleo duniani.