Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mambo manne yanayokwamisha kurejea kwa Mwendokasi Kibaha

Muktasari:

  • Huduma za mwendokasi zilianza rasmi mwaka 2016 kwa kuishia Kimara, baadaye zikaongezewa ruti za Mbezi, Hospitali ya Mloganzila na Kibaha.



Dar es Salaam. Wakati huduma ya mabasi ya mwendokasi kati ya Kibaha na Kimara ikikwama kuanza kama ilivyotangazwa, Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart) umebainisha mambo manne yaliyokwaza kurejea kwa huduma hiyo.

Usafiri huo wa umma katika njia ya Kibaha ulisitishwa tangu mwaka juzi, kabla ya Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha kutangaza Juni 30, 2026 kuwa utarejea tena kuanzia leo, Jumatatu ya Julai 6, 2026.

Juni 30, 2026, Ofisa Habari wa Halmashauri ya Kibaha, Neto Kredo, alisema safari hizo zitaanzia Stendi ya Kibaha na kuishia Kimara pekee.

Kabla ya kusitishwa, njia ya Kibaha ilikuwa pia na safari za Gerezani asubuhi na jioni, ambazo kwa sasa hazitakuwepo hadi zitakapotangazwa baadaye.

Hata hivyo, Julai 4, Mkurugenzi Mkuu wa Udart, Pius Ng'ingo, alipozungumza na Mwananchi kuhusu kuanza tena kwa utoaji wa huduma katika njia hiyo, amebainisha mambo mbalimbali yanayokwaza kuanza kwa safari hizo.

Ng'ingo amesema mambo hayo kuwa ni pamoja na vituo vya mabasi hayo, vibanda vya kukatia tiketi, ufungaji wa mashine kwenye mabasi na suala la nauli.

Amesema kwa kuwa yote hayo yanahusisha taasisi mbalimbali, mengi yako katika mchakato wa kushughulikiwa baada ya wadau hao kufanya vikao mbalimbali na yatakapokuwa tayari, usafiri huo utarejea kama kawaida.

Kutokana na hali hiyo, amewataka wananchi kuwa na subira kwa kuwa wanafahamu uhitaji mkubwa wa usafiri huo katika maeneo hayo.

Katika hatua nyingine, mkurugenzi huyo amesema nauli iliyokuwa ikitumika awali itabadilika na sasa itakuwa Sh2,000, kiwango walichokipendekeza kwa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra), badala ya Sh650 iliyokuwa ikitozwa awali.

“Tumeshapeleka mapendekezo yetu Latra ya kutaka nauli ipande kwa kuwa ile ya awali ya Sh650 ilitufanya tujiendeshe kwa hasara. Katika hili, tunasubiri majibu pia,” amesema.

Amesema matarajio yao ni kwamba watakaporejea kutoa huduma hiyo kuwe na mabasi yanayotoka moja kwa moja Kibaha hadi Kariakoo au Kibaha hadi Kivukoni, badala ya abiria kulazimika kuunganisha usafiri huo Kimara Mwisho.


Walivyozungumza wananchi

Wakitoa maoni yao kwa nyakati tofauti, baadhi ya wananchi wa Kibaha wamesema usafiri huo ni muhimu kwao kwa kuwa ulikuwa ukiwarahisishia kufika mjini kwa haraka.

Mwanaidi Kulwa amesema ipo haja ya taasisi zinazohusika na usafiri huo kuharakisha michakato yao kwa kuwa wanaopata tabu ni wananchi.

Naye Christian Karua amesema kumekuwa na idadi kubwa ya watu wanaoishi nje ya Dar es Salaam katika ukanda huo na kufanya shughuli zao mjini kila siku, jambo ambalo amesema mamlaka zingepaswa kulichukulia kama fursa.

Kuhusu nauli kupanda, Chiku Aluwa amesema walau iwe Sh1,000 au Sh1,500 kwa kuwa huo ni usafiri wa umma, lakini kikubwa mabasi yake yanatumia gesi ambayo si gharama kubwa katika uendeshaji.

Maoni hayo yametofautiana na ya Nsajigwa Andrea, ambaye amesema haoni kama ni shida kwa kuwa wamekuwa wakitumia gharama kubwa zaidi ya hiyo wanapokwenda mjini.

“Ukitoka Kibaha hadi Posta au Kariakoo kwa bajaji au bodaboda, si chini ya Sh7,000 hadi Sh8,000. Utalipia tena kwa kuunganisha usafiri hadi Mbezi Sh3,000 na kisha Mbezi uchukue bajaji nyingine hadi mjini kwa Sh4,000.

“Hivyo, kwa kutozwa fedha hiyo kwa mwendokasi, sioni kama kuna ubaya,” amesema Andrea.

Mkazi mwingine, Felcian John, amesema kupandisha nauli karibu mara tatu kunaweza kuwa changamoto kwa wengi kushindwa kuimudu na kuendelea kutumia daladala.

“Mfano, nikiwa natoka Mathias, nikipanda daladala hadi Mbezi ni Sh1,500, kisha Mbezi nikitumia mwendokasi ni Sh1,500, hivyo nakuwa nimetumia Sh3,000.”


Kauli ya Latra CCC

Wakati wananchi wakisema hivyo, Katibu Mtendaji wa Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Usafiri Ardhini (Latra CCC), Daud Daudi, amesema hata wao wanatamani kazi za kurekebisha miundombinu iliyoharibiwa zikamilike hata kesho.

Kwa mujibu wa Daudi, wamekuwa wakipata malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusiana na kukosekana kwa huduma hiyo kwa muda mrefu sasa, hali inayowasababishia kuingia gharama kubwa za usafiri.


“Kwa kuwa suala la miundombinu ni la Dart, ni vema wakaharakisha kulikamilisha, kwani hata kwa mtoa huduma litawasaidia kupata abiria katika njia zake za mlisho,” amesema Daudi.


Mtazamo wa kiuchumi

Mchambuzi wa masuala ya uchumi na kijamii, Oscar Mkude, amesema usafiri huo ni biashara kama zilivyo biashara nyingine, na huwezi kununua chungwa kwa Sh20 ukauza kwa Sh12. Pia, kuna gharama nyingine za uendeshaji kama mishahara, ukarabati wa magari na mambo mengine.

Hata hivyo, amesema hali hiyo inatokana na baadhi ya miradi inayoanzishwa na Serikali kuchukuliwa kisiasa.

“Kwenye uchumi, biashara hufanyika kutokana na uhitaji, lakini wanasiasa hufanya mambo ili kujipatia umaarufu, hata kama wanajua jambo hilo haliwezekani. Wanaweza kuwa maarufu, lakini mwingine ndiye akajikuta anaumia,” amesema Mkude.

Pia, mchambuzi huyo amesema viongozi lazima wakubali kuwa mradi huo ni wa kibiashara, hivyo ni lazima wananchi wagharamie huduma hiyo.

Kutokana na hali hiyo, amesema anayeendesha mabasi hayo lazima atafute mahali pa kufidia gharama, na hapo ndipo unapokuta wafanyakazi wanalipwa mishahara midogo na mwisho wa siku wengine huingia katika wizi wa vipuri na vifaa vingine ili waweze kuishi.

Pia, Mkude hakuwa mbali na watoa maoni wengine kwamba haikupaswa kuchukua muda mrefu kukarabati miundombinu iliyoharibika ili huduma ziendelee.

Huduma za mwendokasi zilianza rasmi mwaka 2016, ambapo awali mabasi yalikuwa yakiishia Kimara Mwisho, lakini kutokana na uhitaji wa usafiri huo nje ya Kimara, baadaye ziliongezwa ruti za Mbezi, Hospitali ya Mloganzila na Kibaha.