Madereva wakosa mafuta bei ikitarajiwa kupanda leo usiku

Muktasari:
- Kuwapo kwa matarajio ya kupanda kwa bei imetajwa kuwa moja ya sababu inayofanya baadhi ya vituo kutangaza kuishiwa mafuta ili kusubiri kuuza kwa bei nzuri.
Dar es Salaam. Kukosekana kwa mafuta katika baadhi ya vituo kumeleta usumbufu kwa watumiaji wa vyombo vya moto, huku matarajio ya kupanda kwa bei kesho Jumatano ya Machi 5, 2024 ikiwa sababu.
Kati ya vituo 11 ambavyo Mwananchi ilipita kuangalia upatikanaji wa huduma hiyo, sita kati yake havikuwa vikitoa huduma kwa madai ya kutokuwa na mafuta.
Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), Titus Kaguo amesema wanafuatilia suala hilo ili waweze kubaini tatizo ni nini.
Mwananchi imefanya utafiti katika baadhi ya maeneo jijini hapa na kubaini baadhi ya vituo havina mafuta kwa siku moja, mbili na wengine nne, huku wakiahidi kuwa kuanzia usiku wa leo yataanza kuuzwa au kesho.
Jambo hilo liliwafanya wafanyakazi katika vituo hivyo kukaa bila kazi huku wakilazimika kutoa ishara ya mikono kwa kuashiria kuwa hakuna huduma kwa wamiliki wa pikipiki, bajaji au magari ambao huingia vituoni humo kufuata huduma.
Mwananchi imefanya utafiti huo katika baadhi ya vituo vya Mwenge, Ubungo na Tabata na kubaini kuwa tatizo hilo katika baadhi ya maeneo hujirudia kila bei mpya ya mafuta inapokaribia kutangazwa.
“Tuna siku ya nne hatuna mafuta hapa, hili ni tatizo ambalo hujirudia sana hasa inapokaribia kutangazwa bei mpya, hivyo labda kesho huduma zinaweza kuwapo tena kwa sababu leo watatangaza bei,” amesema muhudumu kutoka moja ya kituo ambacho Mwananchi ilifika.
Katika eneo hilohilo la Mwenge mfanyakazi katika kituo kingine aliliambia Mwananchi kuwa hawatoi huduma kwa sababu kuna tatizo la umeme.
Hata hivyo baada ya kuulizwa kwa muda gani tatizo hilo litakuwa limekwisha ili kwenda kujaza mafuta alijibu. “Hata mafuta pia hakuna, tangu jana labda baadaye au kesho,” amesema.
Kilichoonekana katika eneo la Mwenge kipo pia katika baadhi ya vituo vilivyopo Tabata ambapo kukosekana kwa mafuta kumewafanya wafanyakazi kupiga soga vituoni.
“Hatuna mafuta kaka,” alisema mfanyakazi wa kituo hicho akimuambia dereva wa gari iliyokuwa imebeba waandishi wa Mwananchi.
“Kwa nini” dereva aliuliza na kujibiwa kuwa yamekwisha kwa siku mbili sasa huku akitaja moja ya sababu kuwa ni kusubiri bei mpya.
“Labda mjaribu kwenye vituo vingine (huku akitaja jina la kituo), wale huwa nayo muda wote, sisi hapa labda kesho Jumatano ndiyo uhakika,” amesema.
Ewura hutangaza bei mpya za mafuta kila Jumatano ya kwanza ya mwezi ambayo itatumika kwa mwezi husika, jambo ambalo limetajwa kuwa sababu ya baadhi ya watu kuhodhi mafuta hasa wakiwa na uhakika wa bei kupanda.
“Sasa hii inatuumiza sisi watumiaji wa mafuta ya petroli, wakati mwingine mtu unaweza kuwa na mafuta yako kisoda umepiga hesabu sehemu fulani kuna kituo utajaza unakuta hakuna na sababu hazieleweki, mwisho wa siku uanze kutafuta kidumu ili usije kuzimikiwa na gari barabarani,” amesema Razak Ramjam mkazi wa Tataba.
Maneno yake yanaungwa mkono na bodaboda katika kituo cha Baracuda ambaye ameliambia Mwananchi kuwa jambo hilo imekuwa ni mchezo uliozoeleka.
“Labda nyie hamkujua tu, hili lipo, hasa bei zikianza kupanda kila mwezi, watu wanaficha wanataka wauze kwa faida mzigo walionunua kwa bei ndogo siyo haki,” amesema John Julius ambaye ni bodaboda huku akiongeza “Jambo hili linatuumiza sana sisi watu wa chini maana tunaingia gharama zaidi na tunachokipata ni kidogo.
Katibu Mkuu wa Chama cha Wamiliki na Waendeshaji wa Vituo vya Mafuta Nchini (Tapsoa), Augustino Mmasi amesema changamoto ya mafuta ipo kwa miezi miwili sasa, huku akitaja sababu kuwa shida iliyopo ni upatikanaji wa dola za Marekani.
“Si kwamba tunaficha mafuta kutokana na kesho yatapanda wafanyabiashara wakubwa wakienda kuagiza mafuta wakisema wanataka tani za ujazo lita 40 wanapewa 20 au 15, kwa hiyo si kweli kuwa wafanyabiashara wanaficha mafuta bali dola imeadimika,” amesema Mmasi.