Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mabadiliko ya uchumi yanavyogusa mtiririko wa fedha za kigeni

Hali ya uchumi hupitia mizunguko mbalimbali ya ukuaji na kushuka, inayojulikana kwa kimombo kama economic cycles. Katika vipindi hivi, shughuli za uzalishaji hubadilika, hali ya ajira huathirika, na kiwango cha uingiaji wa fedha za kigeni kinaweza pia kubadilika.

Kwa ujumla, kiwango cha fedha za kigeni kinachoingia nchini huongezeka endapo mauzo ya bidhaa au huduma kwenda nje ya nchi yanaongezeka. Kinyume chake, ikiwa mauzo hayo yatapungua, kiasi cha fedha za kigeni kinachoingia nchini nacho kitapungua.

Kiashiria muhimu kinachoonesha mwenendo wa uingiaji na malipo ya fedha za kigeni ni mizania ya malipo ya biashara ya kimataifa (balance of payments). Mizania hii huonesha takwimu za uuzaji na uagizaji wa bidhaa pamoja na kiasi cha miamala ya fedha za kigeni kilichopokewa au kufanyika kwa kipindi fulani.

Kiwango cha fedha za kigeni kinachopokewa hubadilika kulingana na misimu ya uzalishaji, hasa kwa bidhaa zinazouzwa nje ya nchi.

Kwa mfano, katika msimu wa mavuno ya mazao ya kilimo kama kahawa, chai, pamba, na korosho, uingiaji wa fedha za kigeni huongezeka kutokana na mauzo ya mazao hayo ghafi nje ya nchi. Vivyo hivyo, ongezeko la uuzaji wa bidhaa nyingine kama madini linaweza kuongeza akiba ya fedha za kigeni.

Sekta ya utalii pia ni chanzo muhimu cha fedha za kigeni. Utalii huwa na msimu maalumu, mathalani, kipindi cha likizo na majira ya joto barani Ulaya, ambapo wageni wengi hutembelea nchi za Afrika kwa ajili ya utalii. Kiasi cha fedha kinachopatikana kutokana na utalii hutegemea mabadiliko ya mahitaji na hali ya biashara katika sekta hiyo.

Chanzo kingine ni utumaji wa fedha kutoka nje ya nchi (remittances), ambapo raia wanaoishi au kufanya kazi nje hutuma fedha kwa familia zao nyumbani. Kwa nchi zilizo na idadi kubwa ya diaspora, kama Nigeria barani Afrika, fedha hizi ni sehemu muhimu ya akiba ya fedha za kigeni.

Nchi zenye uimara kuhimili changamoto ya soko la fedha za kigeni zile ambazo zina sekta kubwa za uzalishaji kuuza kwa wingi kwenda nje ya nchi bidhaa za aina mbalimbali, mfano bidhaa za viwandani, nguo, mashine, vifaa vya ujenzi na mengine.

Kuwa na sekta kubwa ya uzalishaji maana yake ni kuwa na mianya mingi ya kupata fedha za kigeni inayotunisha chungu cha akiba ya fedha hizo ukilinganisha na nchi zenye sekta ndogo za uzalishaji.

Nchi za Kiafrika zinahitajika kujimaarisha katika hili, kwa kutanua wigo wa kuwa na sekta mbalimbali za uzalishaji zinazochangia mauzo kwenda nje ya nchi, kwa kuanzia ni kuongeza thamani ya bidhaa tunazouza nje ya nchi ili kupata faida zaidi kwa kupata fedha nyingi za kigeni na faida za uchumi jumla ambazo tunazikosa kwa kuuza bidhaa ghafi.

Akiba ya fedha za kigeni ni kiashiria muhimu cha mwenendo wa nchi katika biashara ya kimataifa. Ikiwa akiba hiyo inaongezeka, inaweza kuwa ishara ya biashara imara, mauzo mazuri nje ya nchi, na ushindani wa bidhaa za ndani katika masoko ya kimataifa.

Vilevile, akiba ya fedha za kigeni ni nyenzo muhimu katika usimamizi wa sera za fedha, hasa kudhibiti thamani ya sarafu ya nchi dhidi ya nyingine. Wakati sarafu inaposhuka thamani kwa kasi, akiba ya fedha za kigeni inaweza kutumika kuingilia kati na kusaidia kuleta utulivu wa soko la fedha.

Kwa kumalizia, nchi zinapaswa kuimarisha uzalishaji wa ndani, kupanua masoko ya nje, na kuongeza thamani ya bidhaa zao ili kuimarisha akiba ya fedha za kigeni na kudhibiti athari za mabadiliko ya kiuchumi.