Prime
Haya ndio mashirika matatu yanayoongoza kwa hasara

Muktasari:
- Ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) zimewasilishwa bungeni, huku zikibainisha mashirika yanayoongoza kwa kupata hasara.
Moshi. Mashirika ya Umma ya Kibiashahara 12 kati ya 52, yamebainika kupata hasara kwa miaka mitatu mfululizo, huku Shirika la Reli Tanzania (TRC), likiongoza na kufuatiwa na Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) na Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL).
Hii ni kwa mujibu wa Ripoti Kuu ya Mwaka ya Ukaguzi wa Mashirika ya Umma kwa mwaka wa Fedha 2023/2024 ulioishia Juni 30, 2024 uliofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na kukabidhiwa bungeni leo Aprili 16.
Katika ripoti hiyo, CAG ameeleza mbali na mashirika hayo, lakini mashirika matano yalipata hasara kwa miaka miwili mfululizo, huku mashirika mawili yalipata hasara kwa mwaka mmoja wa fedha wa 2023/24 ulioishia Juni 30, 2024.
Kwa mujibu wa CAG, Hasara hizo zinasababishwa na utendaji duni wa uwekezaji na shughuli za biashara, usimamizi usio mzuri wa matumizi ya fedha, pamoja na ukusanyaji mdogo wa mapato kutokana na mikakati isiyofaa ya kibiashara.
Ripoti hiyo inaonyesha mwaka wa fedha 2021/2022, TRC ilipata hasara ya Sh190 bilioni, mwaka 2022/2023 ikapata hasara ya Sh101.66 bilioni na mwaka huu wa fedha wa 2023/2024, hasara hiyo imeongezeka na kufikia Sh224.59 bilioni.
Kulingana na ripoti hiyo, mwaka 2021/2022, ATCL lilipata hasara ya Sh35 bilioni, mwaka 2022/2023 likapata hasara ya Sh56.6 bilioni na mwaka 2023/2024 hasara ya Shirika hilo ikaongezeka karibu mara dufu na kufikia Sh91.79 bilioni.
Kwa upande wa Shirika la Mawasiliano Tanzania wao mwaka wa fedha 2021/2022 walipata hasara ya Sh19.2 bilioni, lakini mwaka uliofuata wa 2022/2023 hasara ilishuka hadi Sh4.3 bilioni lakini 2023/2024 hasara ikapanda hadi Sh27.7 bilioni.
Mashirika yaliyopata hasara kwa miaka miwili ni Kampuni ya Sisalana Tanzania, Kampuni ya Mkulazi, Kampuni ya Kiwanda cha Bidhaa za Ngozi Kilimanjaro, Kiwanda cha Kuzalisha Bidhaa za Kibiolojia Tanzania na Shirika la Posta.
Mashirika mengine yaliyopata hasara ni Kiwanda cha Madawa Keko, Shirika la Masoko Kariakoo, Kampuni ya TTCL Pesa, Kampuni ya Uendelezaji Joto Ardhi Tanzania, Kampuni ya Gesi Tanzania na Kituo cha Uwekezaji APC.
Alichokisema CAG
CAG katika ripoti hiyo inayoishia Juni 30,2024, amefafanua TRC lilirekodi ongezeko la hasara kwa asilimia 120, ikiongezeka kutoka Sh102 bilioni mwaka 2022/23 hadi Sh224 bilioni mwaka 2023/2024 akisema ongezeko hilo ni kubwa.
Mdhibiti na Mkaguzi huyo amesema ongezeko hilo lilichangiwa hasa na kupungua kwa mapato na kupanda kwa gharama za uendeshaji, licha ya kupokea ruzuku ya Serikali ya Sh29.01 bilioni kwa ajili ya uendeshaji na maendeleo ya shirika.
Halikadhalika katika ripoti hiyo iliyokabidhiwa bungeni, amesema mapato ya uendeshaji yalipungua kutokana na huduma za usafirishaji mizigo na abiria kuathiriwa na upungufu wa vichwa vya treni na idadi isiyotosheleza ya mabehewa.
Kutokana na changamoto hizo, CAG amependekeza TRC lijikite kuboresha ufanisi wa utendaji kazi wake ili kuongeza ukusanyaji wa mapato na kutekeleza hatua madhubuti za kupunguza gharama ili kuliondoa katika hasara hizo.
Pia amependekeza shirika hilo kuandaa mpango wa kina wa kupata injini za treni na mabehewa ili kukidhi mahitaji ya usafiri ipasavyo.
Alichokisema kuhusu ATCL
Katika ripoti hiyo, CAG amesema ATCL imeendelea kurekodi hasara za kifedha kwa miaka sita mfululizo, licha ya kupokea ruzuku kutoka serikalini.
Mathalan, alisema mwaka 2023/24, Kampuni hiyo ilipokea Sh70 bilioni kwa ajili ya mishahara ya wafanyakazi na gharama zingine za wafanyakazi, pamoja na Sh57 bilioni kama ruzuku ya maendeleo kwa miradi ya uwekezaji.
Hata hivyo, licha ya msaada wa kifedha, hasara halisi ya Shirika hilo iliongezeka kwa asilimia 62, ikipanda kutoka Sh56.6 bilioni mwaka 2022/23 hadi kufikia Sh91.8 bilioni mwaka 2023/24, huku jumla ya hasara zikifikia Sh534 bilioni.
“Hali mbaya ya kifedha ilichangiwa hasa na gharama kubwa za kodi na matengenezo ya ndege mpya zilizonunuliwa, ambazo ziliongeza gharama kwa Kampuni,” amesema CAG katika ripoti hiyo iliyowekwa mtandaoni na kuongeza:-
“Zaidi ya hayo, kuharibika kwa ndege za Airbus A220-300 kutokana na kutu na hitilafu za injini zinazohusiana na mtengenezaji, ilisababisha usumbufu mkubwa wa safari, upotevu wa mapato, na gharama zisizorejeshwa za bima.”
“Changamoto hizi zinaendelea kuonesha haja ya dharura ya hatua za kudhibiti gharama, kuboresha uhakika wa ndege, na mikakati ya kuongeza mapato ili kuhakikisha uendelevu wa kifedha wa ATCL kwa muda mrefu,” amesema.
CAG amependekeza shirika hilo lishirikiane na Serikali kufanya utafiti kuhusu njia nzuri zaidi ya uendeshaji wa ndege, kwa kuzingatia masuala ya kifedha, kisiasa na kiuchumi ili kuongeza ufanisi wa uendeshaji.
Shirika la Mawasiliano
Kuhusu Shirika la Mawasiliano la Tanzania, CAG katika ripoti yake hiyo amesema Shirika hilo lilipata hasara ya Sh27.78 bilioni mwaka 2023/24, ikiwa ni ongezeko la asilimia 543 kutoka Sh4.32 bilioni mwaka wa fedha uliotangulia wa 2022/23.
“Hii inatokana na kuongezeka kwa gharama za uendeshaji, ambazo ziliongezeka kutoka Sh104.23 bilioni hadi kufikia SH140.73 bilioni,”amesema na kuongeza;-
“Ongezeko hili lilisababishwa na kuhamishwa kwa Mkongo wa Taifa na Kituo cha Taifa cha Data ya Mtandao uliongeza jumla ya mali za Shirika la Mawasiliano”
Hata hivyo, amesema mapato yote yaliyokusanywa kutoka Mkongo wa Taifa kwa mwaka 2023/24, ambayo ni Sh24 bilioni, yalielekezwa Mfuko Mkuu wa Serikali ili kulipa deni la Serikali lililotokana kwa kupata mkongo huo.
Hali hiyo kwa mujibu wa CAG, ililifanya hivyo Shirika hilo kukosa mapato kwa ajili ya uwekezaji na gharama za uendeshaji na hivyo kuathiri sana uendelevu wa kifedha wa shirika na kusababisha hasara kubwa.
CAG amependekeza Shirika hilo liboreshe ufanisi katika utendaji ili kuongeza ukusanyaji wa mapato na liwasiliane na Serikali ili mapato yatokanayo na Mkongo wa Taifa yabaki katika shirika hilo ili kuliwezesha kushindana ipasavyo sokoni.
Shirika la Posta
Shirika la Posta Tanzania lilipata hasara kwa miaka miwili mfululizo ambapo mwaka 2023/24, lilipata hasara ya Sh23.63 bilioni, ikiwa ni ongezeko la Sh22.29 bilioni 22.29 ikilinganishwa na hasara ya Sh1.34 bilioni iliyoripotiwa 2022/2023.
Hali hiyo kwa mujibu wa CAG ilichangiwa zaidi na kupungua kwa mapato kwa asilimia 20, kutoka Sh37.11 bilioni mwaka 2022/23 hadi Sh30.89 bilioni mwaka wa fedha 2023/24, wakati jumla ya gharama pia iliongezeka kwa asilimia 46.
“Pamoja na kupokea Sh2 bilioni kutoka serikalini kama ruzuku kwa shughuli za maendeleo, shirika bado lilishindwa kufikia malengo yake ya mapato na kuendelea kupata hasara,” alieleza CAG katika ripoti yake hiyo iliyowekwa mtandaoni.
CAG alipendekeza Shirika la Posta la Tanzania lijikite katika kuboresha ufanisi wa utendaji kazi ili kuongeza ukusanyaji wa mapato na kutekeleza hatua madhubuti za kupunguza gharama.