Prime
Gen Z soko muhimu ifikapo 2030, fedha zao utazichuma hivi
Picha na Mtandao.
Gen Z kinatarajiwa kuwa kizazi kinachotumia fedha nyingi kuliko vingi vilivyotangulia na thamani ya manunuzi wanayofanya yakitarajiwa kufikia Dola za marekani 12 trilioni ifikapo mwaka 2030.
Jambo hilo linawafanya kuwa soko muhimu kwa wafanyabiashara duniani miaka ijayo wakati ambao fedha nyingi wanazitumia katika kununua bidhaa za teknolojia ikiwamo simu, urembo, nguo huku wakibadili namna ya kununua bidhaa hizo kidijitali kwenda sokoni hadi kutumia simu na mitandao ya kijamii.
Utafiti wa Consumer Culture Report 2024 uliochapishwa na taasisi ya 5WPR ya Marekani, unaonyesha kuwa asilimia 52 ya waliohojiwa walikiri kununua bidhaa za kielektroniki siku chache zilizopita, asilimia 52 walitumia fedha kwa ajili afya na ustawi binafsi.
Pia asilimia 45 walikiri kutumia fedha zao kufanya safari mbalimbali za kitalii na asilimia 43 wakifanya manunuzi ya bidhaa za urembo.
Wakati bidhaa hizo zikipata soko kubwa, A Global Report on Gen Z Spending Power & Habits inaonyesha kuwa asilimia 53 ya Gen Z hufanya maamuzi ya kununua baada ya kupata taarifa, mapendekezo au kuona bidhaa kupitia majukwaa ya mitandao ya kijamii hususan TikTok, Instagram na majukwaa mengine ya biashara za kidijitali.
Utafiti huo uliofanywa na NielsenIQ (NIQ) kwa kushirikiana na World Data Lab (WDL) umebainisha kuwa uwepo wa biashara kwenye mitandao ya kijamii si tena njia ya kujitangaza pekee, bali imekuwa sehemu muhimu ya mchakato wa kuwashawishi wateja kufanya maamuzi ya kununua.
Licha ya kuwa umefanyika nchini Marekani lakini unaaksi uhalisia wa maisha halisi katika maeneo mengi ya dunia kutokana na maendeleo ya teknolojia na uwepo wa mitandao ya kijamii tabia na karba ya jamii nyingi sasa zinafanana
Nini maana yake?
Akizungumzia suala hili, Mtaalamu wa uchumi, Aurelia Kamuzora anasema tabia za matumizi za Gen Z haziwezi kutazamwa kwa mtazamo wa vizazi vilivyopita pekee, kwa sababu kila kizazi hukua katika mazingira tofauti ya kiuchumi na kiteknolojia.
Anasema mara nyingi kizazi kilichotangulia huamini kizazi kinachofuata hakitumii muda au fedha zake kwa njia sahihi lakini historia inaonyesha kuwa teknolojia ambazo zilionekana kupoteza muda baadaye zimekuwa sehemu muhimu ya maisha na uchumi.
"Kilichopo leo kinaweza kuonekana si cha muhimu lakini kesho kikawa sehemu ya kawaida ya maisha. Kizazi cha millennial (Kizazi kabla ya Gen Z) kilipoanza kutumia simu za mkononi, watu wengi waliona ni anasa leo karibu kila mtu anatumia simu. Hata wakati mashine za kuandikia (typewriter) zilipoanza kutumika, kulikuwa na waliodhani ni upotevu wa muda, lakini baadaye zikawa nyenzo muhimu za kazi," anasema.
Kwa mujibu wa Kamuzora, maendeleo ya teknolojia yamepunguza gharama za kufanya biashara na kuongeza kasi ya upatikanaji wa taarifa, jambo linalowapa vijana fursa kubwa zaidi za kuzalisha na kutumia kipato.
Anasema zamani mfanyabiashara aliyekuwa Kigoma asingeweza kujua mahitaji ya soko la Dar es Salaam au Arusha kwa wakati, hali iliyoongeza gharama na hatari ya kufanya biashara. Leo, kupitia teknolojia, taarifa za masoko, bei na mahitaji hupatikana kwa haraka, hivyo kurahisisha maamuzi ya uwekezaji na biashara.
"Kutokujua biashara inavyoendeshwa katika eneo lingine ni gharama. Teknolojia imeondoa kikwazo hicho kwa kufanya taarifa zipatikane kwa wakati na kupunguza gharama za kubadilishana bidhaa na huduma," anasema.
Anasema maendeleo hayo yamekuwa na manufaa pia kwa sekta ya kilimo, ambapo wawekezaji na wafanyabiashara wanaweza kufikia wakulima waliopo vijijini kwa urahisi zaidi kupitia majukwaa ya kidijitali, hivyo kufungua masoko mapya na kuongeza thamani ya mazao.
Kamuzora anasema changamoto si matumizi ya teknolojia yenyewe, bali namna inavyotumiwa. Anaonya kuwa vijana wanaotumia muda mwingi mtandaoni kwa burudani pekee bila kujifunza au kutafuta fursa za kiuchumi wanaweza kukosa manufaa makubwa ambayo teknolojia imeleta.
"Malezi ya sasa yanapaswa kuwaelekeza vijana kutumia teknolojia kama nyenzo ya kujenga kipato, kufanya biashara, kuwekeza na kuongeza maarifa. Leo karibu kila biashara ipo mtandaoni; ukijua kuitumia vizuri unaweza kujiongezea kipato na kujenga maisha yako," anasema.
Anasema matumizi yasiyo na tija yanaweza kuwa na athari za muda mrefu.
"Mtu akitumia muda mwingi kuangalia maudhui yasiyomjengea uwezo baadaye anaweza kuyaona kuwa ya kawaida na kushindwa kuona fursa zinazomzunguka. Wakati wengine wanatumia mitandao kuongeza ujuzi, kupata elimu na kujenga biashara, yeye anabaki kuwa mtumiaji wa maudhui pekee," anasema.
Kwa mtazamo wake, faida za teknolojia ni kubwa kuliko hasara zake ikiwa kutakuwa na juhudi za wazazi, walimu na Serikali kuwaongoza vijana kuitumia kwa manufaa ya kiuchumi.
"Kinachotakiwa ni kuhakikisha vijana wanatumia mitandao ya kijamii na teknolojia kuzalisha kipato, kuwekeza na kujifunza. Tukifanya hivyo, teknolojia itakuwa chachu ya maendeleo badala ya kuwa chanzo cha kupoteza muda," anasema.
Mtaalamu wa teknolojia, Baraka Mafole anasema moja ya sababu zinazofanya Gen Z kutumia fedha zaidi kuliko vizazi vilivyotangulia ni mabadiliko makubwa ya teknolojia na uchumi wa kidijitali ambao umebadili namna wanavyopata na kutumia kipato.
Anasema tofauti na miaka ya nyuma ambapo vyanzo vikuu vya mapato vilikuwa ajira rasmi, biashara na kilimo, kizazi cha sasa kina fursa nyingi zaidi za kujipatia kipato kupitia majukwaa ya kidijitali.
“Vijana wengi wanapata fedha kwa kutengeneza maudhui kwenye mitandao ya kijamii, kufanya biashara mtandaoni, kazi za kujitegemea uuzaji wa bidhaa za kidijitali na huduma nyingine zinazotegemea teknolojia,”
"Gen Z wanapata fedha kwa kufanya kile wanachokipenda. Mtu anaweza kutengeneza video, kuuza bidhaa kupitia Instagram au TikTok, kufanya kazi mtandaoni au kuwa mtayarishaji wa maudhui na akapata kipato. Hii imeongeza uwezo wao wa kutumia fedha kuliko ilivyokuwa kwa vizazi vya nyuma," anasema.
Mafole anasema wakati huo huo, uchumi wa kidijitali umeongeza pia maeneo ambayo vijana wanatumia fedha zao kupata kile wanachohitaji kupitia ‘subscription economy’, ambapo huduma nyingi sasa zinapatikana kwa malipo ya kila mwezi au kila mwaka.
Anasema vijana hulipia huduma mbalimbali za kidijitali kama majukwaa ikiwamo kusikiliza muziki, kutazama filamu, kuhifadhi taarifa mtandaoni, michezo ya mtandaoni na programu za kuongeza ufanisi wa kazi.
Aidha, baadhi ya mitandao ya kijamii nayo imeanzisha huduma zinazowaruhusu watumiaji kulipia maudhui maalumu kutoka kwa watengenezaji wa maudhui jambo linaloongeza matumizi ya fedha. "Leo karibu kila huduma ina mfumo wa usajili. Ukitaka kusikiliza muziki bila matangazo unalipia, ukitaka kutazama filamu unalipia, hata baadhi ya maudhui ya watu unaowafuata mtandaoni yanahitaji malipo. Hii ina maana matumizi ya fedha yamekuwa sehemu ya maisha ya kila siku ya Gen Z," anasema.
Kwa mujibu wa Mafole, mzunguko huo wa kupata fedha kwa urahisi zaidi kupitia teknolojia na kuzitumia kwenye huduma mbalimbali za kidijitali umeifanya Gen Z kuwa kizazi kinachozungusha fedha kwa kasi kuliko vizazi vilivyotangulia, huku matumizi yao yakiongozwa zaidi na urahisi, uzoefu na huduma za kidijitali.
Mmiliki wa duka la bidhaa za urembo, Neema Mushi anasema Gen Z ndiyo kundi kubwa la wateja wake kwa sasa kutokana na namna wanavyowekeza kwenye mwonekano na kujitunza.
"Miaka michache iliyopita bidhaa zilizokuwa zikiuzwa zaidi zilikuwa vipodozi vya kawaida lakini sasa vijana wanatafuta zaidi bidhaa zitakazowapa mwonekano mzuri bila kujali bei, wanachotaka ni matokeo,” anasema Neema.
Anasema wateja wengi hufika dukani wakiwa tayari wameona bidhaa hizo kupitia TikTok au Instagram na wanajua wanachokitaka huku wakiwa na maswali ya ziada.
Anasema mitandao ya kijamii imebadili kabisa tabia za ununuzi kwa sababu wateja wengi huamua kununua baada ya kuona maoni ya watumiaji wengine au video za waundaji wa maudhui.
"Gen Z hawanunui kwa sababu tu bidhaa ipo dukani. Wanataka kujua faida zake, kuona mtu ameijaribu na kusoma maoni ya wengine kabla ya kutoa fedha hiyo ndiyo imeifanya biashara ya urembo kukua kwa kasi," anasema.
Mfanyabiashara wa nguo, Abdulrahman Hamis anasema vijana wengi hutanguliza mitindo mipya kuliko bei ya bidhaa.
"Wanapenda kuvaa kile kinachoonekana kwenye mitandao ya kijamii, msanii mkubwa akivaa wa ndani au nje ndiyo nao wanahitaji hasa baada ya kuona TikTok au Instagram na msanii akivaa mahitaji ya hiyo nguo yanapaa,” amesema.
“Hivyo sisi pia tunalazimika kufuatilia mwenendo wa mitindo kila siku ili tusipitwe na wakati. Tofauti na vizazi vya nyuma, Gen Z hununua nguo mara nyingi zaidi ili kuendana na mitindo inayobadilika kwa kasi,” anasema.
"Wengi hawasubiri sikukuu kununua nguo. Wananunua kwa ajili ya hafla, safari, kutengeneza maudhui mtandaoni au kubadilisha mwonekano wao. Hiyo imeifanya biashara ya nguo kuwa ya haraka zaidi kuliko zamani," anasema.