Diaspora kuvutwa uwekezaji kwenye hisa Tanzania
Mkurugenzi hifadhi ya dhamana Tanzania (CSDR), Benito
Kyando akizungumza katika mkutano uliowakutanisha watoa elimu ya fedha na wadau kujadili namna ya kuboresha matumizi ya teknolojia katika kutanua wigo wa soko la hisa na kuboresha mifumo kuendana na ongezeko la wawekezaji.
Muktasari:
- Takwimu za DSE zinaonyesha miongoni mwa maeneo yaliyoshuhudia uwekezaji mkubwa katika mwaka 2025 ni hisa ambazo mauzo yake yalikuwa Sh5.848 trilioni ikiwa ni ongezeko la asilimia 86.04 ikilinganishwa na Sh3.1 trilioni mwaka uliotangulia.
Dar es Salaam. Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) limeshauriwa kuongeza nguvu ili kuwavuta Watanzania wanaoishi nje ya nchi kuwekeza katika soko la mitaji na dhamana.
Kuwekeza kwao kutafanya Tanzania kupata fedha za kutosha kuendesha baadhi ya miradi na kuchochea uchumi wa nchi.
Hayo yamesemwa leo Jumanne, Machi 3, 2026 katika jukwaa la wawekezaji na watoa elimu ya fedha kujadili mustakabali wa soko la hisa, huku wakilenga kuangalia matumizi ya teknolojia yanavyoweza kukuza ushiriki wa wawekezaji na kuboresha mifumo ili kuhimili ongezeko la wawekezaji katika soko la hisa.
Akizungumza katika mkutano huo, Mtaalamu wa Elimu ya fedha, Emilian Busara amesema watu wanaoishi nje ya nchi wana uwezo mkubwa wa kifedha endapo fedha zao zikiletwa nchini zinaweza kuongeza mtaji wa kufanya uzalishaji na uwekezaji nchini.
“Pia wao kama wawekezaji watapata faida, kwani faida inayotoka katika soko la hisa ni kubwa kuliko na ile inayoweza kupatikana nje ya nchi,” amesema.
Ameshauri kuwa ili Watanzania hao waweze kushiriki vyema katika masoko ya hisa na mitaji ni vyema wawe na vitambulisho Taifa na namba za simu za Tanzania, ili waweze kununua hisa na vipande vya hati fungani popote watakapokuwa.
“Ningetamani kuona mamlaka zinazohusika kusimamia hili, kabla mtu hajaondoka kwenda nje ya nchi anakuwa na kitambulisho chake cha Taifa, akaunti ya benki ya Tanzania na namba ya simu ya Tanzania ili waweze kunufaika na fursa hizo,” amesema.
Amesema hilo liende pia kwa wazazi kuhakikisha watoto wanaowapeleka nje kusoma wanakuwa na vitu hivyo muhimu ili wasiwanyime fursa ya wao kushiriki katika uwekezaji watakaotamani kuufanya Tanzania
“Wakileta ndani hizi fedha zitasaidia nchi, simamieni hili, zungumzeni na Wizara ya Mambo ya Nje huwa inayo orodha ya diaspora wa Tanzania sambamba na hizi Benki za NMB, CRDB huwa wana madawati maalumu, tuangalie namna ya kuwafikia kwa kiwango kinachotakiwa,” amesema Busara na kuongeza;
“Pesa inapoingia Tanzania inakuwa na faida, tuwafanye waachane na kumtumia nani pesa amjengee nyumba wanapigwa, tuwape namna ya kuzalisha wakiwa huko, na njia hiyo ni kuwekeza kwenye hisa.”
Takwimu za DSE zinaonyesha miongoni mwa maeneo yaliyoshuhudia uwekezaji mkubwa katika mwaka 2025 ni hisa ambazo mauzo yake yalikuwa Sh5.848 trilioni ikiwa ni ongezeko la asilimia 86.04 ikilinganishwa na Sh3.1 trilioni mwaka uliotangulia.
Hatifungani za kampuni, mashirika ya umma na Serikali za mitaa katika mwaka 2025 zilifikia Sh12.12 bilioni ikiwa ni ongezeko la asilimia 174 ile iliyokuwapo mwaka uliotangulia.
Akizungumzia namna wanavyowavuta diaspora kuwekeza katika masoko ya hisa na mitaji, Mkurugenzi hifadhi ya dhamana Tanzania (CSDR), Benito Kyando amesema wamekuwa wakitoa elimu kwa njia ya mtandao angalau mara mbili au mara tatu kwa mwaka kwa njia ya mtandao.
“Hii imekuwa na matokeo chanya kwani karibu kila mtu anayeshiriki amekuwa akiwekeza baadaye,” amesema.
Akizungumzia mkutano uliokuwa unafanyika leo, Kyando amesema unalenga kuangalia namna ya kuboresha utoaji wa elimu kwa wananchi na kuboresha mifumo ili iweze kuhimili wingi wa wateja wanaojiunga sokoni sasa.
Edmund Munyagia amesema ni vyema elimu ya fedha ichopekwe katika mitaala ili wanafunzi waanze kujifunza kuangalia ngazi za chini ili watoto wakue wakijua namna wanavyoweza kuwekeza katika shule.
Amesema hilo linawezekana kwa sababu watoto wengi wenye umri wa miaka 15 sasa wanamiliki simu janja ambazo wanaweza kuzitumia kufanya uwekezaji katika maeneo tofauti.
“Tutumie teknolojia kukuza uwekezaji katika hisa na masoko ya fedha, siku hizi vijana wanamiliki simu wakiwa na umri mdogo, tukiweza kuwaelimisha katika umri wao tutakuwa na kizazi bora baadaye,” amesema.