BRT awamu ya nne kutumia mabasi ya umeme
Dar es Salaam. Mchakato wa Tanzania kuelekea kwenye mfumo wa usafiri ambao ni rafiki kwa mazingira umeanza kushika kasi huku Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart) ukitangaza kuwa awamu ya nne ya mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) itatumia mabasi ya umeme pekee.
Hayo yamebainishwa na Mtendaji Mkuu wa Dart, Dk Athumani Kihamia wakati akiongea na vyombo vya habari kuhusu msemaji halali wa mradi wa BRT jijini Dar es Salaam kwamba Dart ndiyo mwenye mamlaka hayo.
Akizungumzia ujio wa mabasi, Dk Kihamia amesema jumla ya mabasi ya umeme 390 yanatarajiwa kutoa huduma katika awamu ya nne inayohusisha kilomita 30.1 kutoka Kivukoni – Mwenge kupitia barabara ya Ali Hassan Mwinyi ikihusisha, pia, kipande cha kutoka Mwenge hadi Simu2000.
“Hii ni hatua kubwa kuelekea azma ya Taifa ya kutumia nishati safi katika usafiri wa umma,” amesema Dk Kihamia.
Amesema kwa awamu ya tatu na nne, mabasi yatakua zaidi 1,300 na kwa Dar es Salaam nzima kutakuwa na mabasi 3,000 ifakapo mwisho wa mwaka 2026.
“Nawaomba Watanzania wenye uzalendo na mitaji mikubwa, zikitangazwa kazi kama hizi wazikimbile ili Watanzania wengi ndio wawe wanazimiliki, kuongeza utajiri, vipato na mitaji yao na kuongeza na ajira nyingi za vijana na watu wengine.
“Hivi ninavyoongea, mabasi mengine yamepandishwa kwenye meli, katikati ya Septemba, jumla ya mabasi yatakayokuwa katika njia ya Mbagala yatakuwa mabasi 151 na mengine yakiendelea kuletwa nchini,” amesema mkurugenzi huyo.
Amesema njia ya Mbagala itakuwa na mabasi 755, awamu ya kwanza (Kimara) itakuwa na mabasi mengine 177, kwa hiyo awamu mbili hizi zitakuwa na mabasi 932, yatakuwa yameondoa kabisa tatizo la msongamano na wananchi kuchelewa kutoka kituo kimoja hadi kingine.
Amesisitiza kwamba tatizo la kusubiri katika kituo kimoja kwa muda mrefu linakuwa limekwisha na kwamba sasa hivi nauli zitazokuwa zikikusanywa kwenye mabasi haya, zitakusanywa kwa mfumo wa kadi.
“Hii itapunguza upotevu wa fedha za Serikali hususani kwa watumishi wachache ambao sio waaminifu ambao hawajaanza kutumia kuzichukua fedha hizo kwa kulipa keshi badale yake fedha zisionekane kwenye mfumo.
Kuhusu usemaji wa mradi huo, Dk Kihamia amesisitiza kwamba hakuna mtoa huduma anayeruhusiwa kuzungumza na vyombo vya habari kuhusu masuala ya kifedha wala mikataba ya ununuzi wa mabasi.
Amesema kumekuwa na taarifa zisizo sahihi zilizotolewa na baadhi ya watoa huduma binafsi zikihusisha majukumu ya usimamizi, ununuzi wa mabasi na shughuli za waendeshaji wenzao. Amesema taarifa hizo ni batili na zinakiuka taratibu za mawasiliano zilizowekwa na Dart.
“Wakala unasisitiza kuwa hakuna mtoa huduma anayeruhusiwa kuzungumza na vyombo vya habari kuhusu masuala ya kifedha, mikataba ya ununuzi wa mabasi,” amesisitiza mkurugenzi huyo.
Wakati akieleza hayo, kampuni tatu binafsi za Kitanzania zimesaini mikataba ya kuleta mabasi ambapo Mofat Company Ltd inaleta mabasi 255 ya njia kuu (urefu wa mita 18), Metro City Link Ltd inaleta mabasi 334 ya njia za mlisho kwa njia 13 na YK City Link Ltd inaleta mabasi 166 kwa njia sita za mlisho.
Mabasi 150 ya Mofat tayari yamepakiwa na yanatarajiwa kufika Bandari ya Dar es Salaam Agosti 15, 2025.