Aina za ulaghai unaoweza kujitokeza mtandaoni
Kadri matumizi ya teknolojia za fedha za kidijitali yanavyozidi kuongezeka, ndivyo mbinu za uhalifu wa mtandao zinavyojibadili sura.
Ingawa huduma hizi zinaendelea kuboreshwa kila siku, wahalifu nao wanatafuta njia mpya za kuwalaghai watumiaji.
Kwa hiyo, ni muhimu kwa kila mtu kuelewa aina na mbinu mbalimbali za ulaghai huu ili kujilinda na kuepuka kunaswa kwenye mitego ya matapeli wa mtandaoni.
Moja ya mbinu hizo ni matapeli kujifanya kuwa watoa huduma, mbinu inayojulikana kama phishing. Katika mbinu hii, walaghai hutuma barua pepe au ujumbe wa uongo unaoonekana kama umetoka kwenye taasisi halali za kifedha.
Kwa mfano, ujumbe unaweza kudai kuwa kuna tatizo kwenye akaunti yako, kama vile kufungwa kwa akaunti, kuingizwa kwa fedha kimakosa au dharura nyingine.
Ili kujinasua, mteja anaweza kuombwa kufuata maelekezo yao au kubonyeza kiunganishi kilichotumwa, ambacho mara nyingi inaweza kuwa mtego wa kimtandao kuiba taarifa zako za siri.
Wahalifu wanaweza kutumia mbinu hiyo kukusanya taarifa za mtumiaji, ambazo baadaye zinawawezesha kupata ufikiaji wa akaunti za kifedha za mtumiaji na kufanikisha uhalifu wao.
Mbinu nyingine wanazotumia walaghai ni udukuzi wa kimtandao kupitia programu hasidi (malware), ambazo zinaweza kuingia kwenye vifaa vya mtumiaji kupitia kupakua faili kiholela mitandaoni, kufungua programu zisizoaminika, au kubofya viungo vilivyotumwa kwenye ujumbe.
Programu hizi zinapoingia kwenye kifaa chako, zina uwezo wa kufuatilia kimya kimya shughuli zako, zikiwemo matumizi ya simu au kompyuta, na kupata taarifa nyeti kama vile akaunti zako za fedha mtandaoni. Mara tu zinapopata taarifa hizo, wahalifu wanaweza kuzitumia kufanya uhalifu kama kuiba fedha au kudukua taarifa nyingine muhimu.
Vilevile, huduma nyingi za kifedha zinategemea ujumbe wa SMS kwa uthibitisho wa usalama.
Hivyo, bila mtumiaji kujua, ikiwa laini yake au kifaa kikiangukia kwenye mikono ya mtu mwingine mwenye nia ovu, wahalifu wanaweza kutumia mbinu hii ili kupokea ujumbe wa uthibitisho au kuidhinisha miamala ya malipo na kusababisha mtumiaji kupoteza fedha zake.
Hali kadhalika, wahalifu wanaweza kutumia mbinu za saikolojia ili kuichezea akili ya mtumiaji wa huduma za kifedha.
Kwa mfano, wanaweza kuwatembelea wateja wakijifanya kuwa wawakilishi wa benki au watoa huduma za simu, na kuwashawishi waathiriwa kutoa taarifa nyeti kama vile anuani zao, taarifa za akaunti na miamala waliyofanya.
Umakini unahitajika kwa wateja ili kuepuka kutoa taarifa zao binafsi bila kuthibitisha uhalali wa mtoa huduma wa kifedha.
Aidha, ili kuepuka ulaghai wa kimtandao, mteja anapaswa kuepuka kupakua programu zisizo rasmi au kutembelea tovuti zisizojulikana, kwa kuwa zinaweza kuwa hatari na zikasababisha kudukuliwa kwa taarifa zake.
Njia bora ya kujilinda ni kupakua programu kutoka vyanzo vinavyotambulika, kuhakikisha programu zako zimeboreshwa na kuwa makini na unachoweka kwenye kifaa chako.
Vilevile, mteja anashauriwa kuepuka kuunganisha kifaa chake na huduma za intaneti za umma, kwani hili linaweza kuwapa wahalifu nafasi ya kupata ufikiaji wa taarifa zako.
Kwa kufanya hivi, mteja anaweza kulinda taarifa zake za kifedha na kuepuka kuwa mhanga wa uhalifu wa mtandaoni.