ZIFF waiomba Serikali kuwaunga mkono

Mkurugenzi wa ZIFF, Profesa Martin Mhando
Muktasari:
Tamasha la ZIFF litafanyika Juni mwaka huu visiwani Zanzibar, likijumuisha filamu za kutazama zaidi ya 3000 zikiwamo ndefu na fupi na za kushindanishwa 85 huku Tanzania ikiingiza filamu nane.
Waandaaji wa Tamasha la Filamu la Nchi za Majahazi, (ZIFF) wameiomba Serikali kuwaunga mkono kwa kuwapa fedha za kujiendesha.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa msimu wa tamasha hilo kwa mwaka 2022, Mkurugenzi wa ZIFF, Profesa Martin Mhando amesema tamasha hilo linatimiza miaka 25, lakini wanapata wakati mgumu kuliendesha kutokana na kutokuwa na fedha.
Amesema kwa kawaida ufadhili wa ZIFF hutolewa kwa ajili ya programu ambazo zinapatikana wakati wa tamasha, lakini hakuna zinazokwenda moja kwa moja kwa uongozi ili kufanya shughuli nyingine za maandalizi.
“Tamasha hili hugharimu wastani wa Dola milioni 10 mpaka kukamilika,kama mnavyofahamu hata tamasha la Sauti za Busara pia lingekufa kwa sababu hapakuwa na fedha za kuliendesha mpaka ilivyofanyika vinginevyo. Tumekuwa tukiiomba Serikali kutambua umuhimu wa kuwa na tamasha hili Visiwani Zanzibar na kuhakikisha linaendelea kuwepo kutokana na umuhimu wake”amesema Mhando.
Profesa Mhando amefafanua kuwa “ZIFF pekee huleta karibu watalii 6000, na kila mtalii hulipa Dola 50 kila mmoja anapoingia nchini, ukijumlisha idadi ya siku wanazotumia wakiwa hapa nchini ikiwamo wanazonunua vitu.
“Watu wanadhani ZIFF imezaliwa na upendo pekee, hapana. Kama vile Yesu alivyosema, watu hawaishi na mkate pekee wanaishi na vitu vingine vingi. Nadhani Serikali zote mbili za Tanzania na Zanzibar zione sasa umuhimu wa kuunga mkono hili,” amesema Mhando.
Mhando amesema kuwa wakati huu tamasha hilo linapotimiza miaka 25 tangu kuanzishwa kwake, wanafanya kitu maalumu kwa washiriki waliowahi kushinda.
“Tutakusanya picha zote zenye kumbukumbu za watu wote waliowahi kufika ZIFF visiwani Zanzibar na kufanya vizuri.
“Tunawaalika watu watutumie picha za kumbukumbu zao wakiwa ZIFF ikiwa na mwaka itapendeza zaidi. Tunasherehekea na tunataka kusherehekea pamoja nao. Tafadhali tunawaomba watume picha zao kwa mratibu Aisha Mussa,” alisema Mhando.
Mhando amesema ikiwa ni sehemu ya kufurahi pamoja na wengine kwa kutimiza miaka 25, wataalika wageni maalumu, “Tutakuwa na siku maalumu kwa ajili ya Kenya, Afrika Kusini na Umoja wa Ulaya, hii yote ni kuhakikisha mwaka huu unakuwa bora zaidi na vitu vingi.
Amesema mbali na filamu nyingine, itakayofungua tamasha hilo ni ‘Vuta nikuvute’, iliyoongozwa na Amil Shivj kutoka Kijiweni Productions.