Willy Paul 'mtamu' akifanya kolabo na Wabongo

Muktasari:
- Hii ni kutokana na historia ya nyimbo zake alizowahi kufanya na wasanii wa Bongo kufanya vizuri kila alipowashirikisha kuliko nyingine.
Msanii Wilson Radido 'Willy Paul', kutoka nchini Kenya, huenda asipotee kwenye ramani ya muziki kama akiendelea kufanya kolabo na wasanii wa Bongo.
Hii ni kutokana na historia ya nyimbo zake alizowahi kufanya na wasanii wa Bongo kufanya vizuri kila alipowashirikisha kuliko nyingine.
Tukianza na ile ya Nandy waliyoipa jina la ‘Njiwa’ iliyotoka miaka mitano iliyopita, iliweza kufanya vizuri na hadi sasa wimbo huo umeshatazamwa mara milioni 24 huko youtube.
Ukiacha wimbo wa Njiwa, pia wimbo wa ‘Mmmmh’ alioufanya na Rayvany katika mwaka huohuo nao ulikuwa moto wa kuotea mbali ambapo mpaka sasa umeshatazamwa mara milioni 34.
Sasa msanii huyo baada ya miaka hiyo mitano ameamua kumshirikisha mkali wa nyimbo za kulilia mapenzi Marioo, ambapo kibao hicho kilichopewa jina la 'Nanana' kilitoka mwezi mmoja uliopita kinafanya vizuri kwa sasa katika mitandao mbalimbali ya kijamii na redio licha ya kuwa bado video yake haijaachiwa.
Wimbo huu ambao upo kwenye albamu mpya ya Willy aliyoipa jina la ‘Beyond Gifted’ baadhi ya wadau wa muziki wanautabiria kuzidi kufanya vizuri pale utakapoachiwa video kwa kuwa maneno na biti zake zimetulia.
Utofauti wa ngoma alizofanya na Wabongo na wasanii wengine unajionesha kwenye ngoma zake ambazo hazojapita kwenye kiwanda cha Bongo Fleva kupokelewa kwa kawaida kama ilivyokuwa kwenye wimbo wake wa 'I Love You'aliofanya na Daphne umetazamwa mara elfu sabini na mbili, au ule 'Kataa kataa'aliofanya na Denyque umetazamwa mara elfu sabini na tatu.
Willy Paul au ukipenda muite Willy Pozzi kabla ya kuimba muziki wa kidunia awali alikuwa akiimba nyimbo za Injili, na tangu alipoimba kwa kushirikiana na kundi la muziki la Saut Sol kibao cha ‘Take It Slow’ kuanzia hapo akaendelea kuimba nyimbo za kidunia hadi sasa.
Msanii huyu ni kati ya wasanii wa Kenya ambao bado wanapambana katika soko la muziki Afrika Mashariki ambapo upepo wake sasa upo Tanzania.