Wema Sepetu amrudia Mungu

Muktasari:
- Muigizaji wa Tanzania, Wema Sepetu amesema baada ya mapito ya muda mrefu amebadili mfumo wake wa maisha na kwamba anafanya dua na kumtegemea Mungu katika mambo yote.
Dar es Salaam. Muigizaji wa Tanzania, Wema Sepetu amesema baada ya mapito ya muda mrefu amebadili mfumo wake wa maisha na kwamba anafanya dua na kumtegemea Mungu katika mambo yote.
Wema amesema hayo leo Februari 26 wakati wa hafla ya kutambulishwa kama balozi wa kampeni ya Pikipika inayoendeshwa na kampuni ya Dar Ceramica ambao ni wasambazaji wa vifaa vya ujenzi.
Akizungumza katika hafla hiyo wema amesema pamoja na kubadili mfumo wa maisha yake, Wema ni yuleyule, hajawahi kubadilika na anaamini katika kupata kwa wakati sahihi wa Mungu na sasa anaona huo wakati wake umefika.
“Mimi ni binti wa kiislamu nafanya sana dua. Watu wanamuona Wema wa mtandaoni lakini binadamu tunakuwa na tunajifunza, tunaoamini katika Mungu, Mungu hukupa kwa wakati wake na wakati ambapo hakunipa aliwapa wengine, riziki inaenda kwa mzunguko,” amesema Wema ambaye jana pia alipata dili la ubalozi na kampuni nyingine.
Katika dili lake na Pikipika Wema atakuwa na jukumu la kuwahamasisha wateja wote na mafundi wanaonunua bidhaa za Dar Ceramica kujisajili na kufungua akaunti ya kuweka kumbukumbu ya manunuzi yote wanayofanya jambo ambalo litawapatia zawadi ya kila mwezi.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Dar Ceramica, Ahmed Ndossa amesema mazingira ya ufanyabishara sasa yanavutia na hayana vikwazo vyovyote kinachofanyika sasa ni kupanua wigo wa upatikanaji wa huduma na wao silaha yao ni ubora wa bidhaa wanazouza.